Hata hivyo, kamati hiyo ililazimika kuahirisha kikao kilichokuwa kikipitia hesabu za chuo hicho hadi kesho baada ya mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Peter Ngumbullu kutofika katika kikao hicho.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka alimuhoji makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala kwanini mwenyekiti wa baraza hilo hayupo.
Akijibu Profesa Mukandala alisema kuwa barua ambayo waliipata ya wito iliwaelekeza waje na mhasibu, ofisa ugavi na wakuu wengine wa idara ambao anaona watamsaidia kujibu hoja za ukaguzi.
"Kwa hiyo naomba msamaha wako mheshimiwa mwenyekiti labda sikuelewa vizuri lakini mimi nilifuata maelekezo ambayo tulikuwa tumepewa,"alisema Profesa Mukandala.
Kufuatia majibu hayo, Kaboyoka alihoji ofisa masuhuri ni nani ambapo Profesa Mukandala alijibu kuwa anachofahamu yeye ndio ofisa masuhuri(Makamu Mkuu wa Chuo).
Hata hivyo makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hillaly alisema ni lazima mwenyekiti huyo kufika kwenye kamati hiyo.
“Sijui kama ulikuwa umejipanga. Lakini aliyekuwa anatakiwa kujibu hapa ni maofisa masurufu ambaye ni mwenyekiti, sasa sijui kama uliamua kuja mwenyewe ili kutukomoa sisi ama ulipata barua yenye maelekezo haya,”alisema Aeshi.
Alisema kikao hicho kisingeweza kuendelea kwa sababu mwenyekiti hayupo.
Mbunge wa Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula alihoji katika utambulisho wa watendaji hao ameona kuna makaimu wengi hivyo ni vyema watakapofika tena kwenye kamati hiyo waje wakuu wa vitengo husika.
Akijibu Profesa Mukandala aliwahakikishia wabunge hao kuwa na kwamba katika utendaji wake wa kazi za kuongoza chuo kikuu hicho amekuwa akitii mamlaka na hasa pale amuamriwa kufanya jambo kwa maandishi.
“Kwa hiyo nikiri kwamba hata mimi nilishangaa barua haikumtaja mwenyekiti kwa sababu mara zote nimeitwa katika kamati hii nimekuja na mwenyekiti na hata wakati mwingine nilifikiria kumwambia makamu mwenyekiti,” alisema.
Hata hivyo, alisema kuwa alipata ujumbe mfupi wa kuwataja watu ambao wanatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo.
Baada ya malumbano, Kaboyoka alisema kuwa UDSM wanafahamu kuwa si mara yao ya kwanza kufika katika kikao cha kamati hiyo.
“Mnajua kuwa kuna mambo ambayo hayaendi sawa, sikuona sababu yoyote kwamba mmekuja bila mwenyekiti wa baraza. Mnajua hapo nyuma kuna mambo mengi sana mmekiuka ambayo mlipewa na kamati hii ya Bunge, sijui kama mnajua mamlaka ya kamati hii,”alihoji.
“CAG ndio jicho letu akileta hapa sie ni sehemu ya Bunge kwa sababu tumepewa dhamana ya kukaka kupitia na kutoa maelekezo na wahusika wanapaswa kutekeleza.”
“Kutokana na hayo tunawapa hadi keshokutwa mje kwenye kamati na mwenyekiti ndio tutaweza kujadiliana,”alisema.
Pia Kaboyoka aliagiza kuagiza maofisa wote watakaofika kesho wawe mwenyewe sio makaimu kama walivyofanya jana.
“Hesabu zenu zimekaa ndivyo sivyo kwa hiyo tunataka kufanyia kazi, kamati ipate muda wa kujikita zaidi siku ya kesho (leo) na kesho kutwa (kesho),”alisema.
Miongoni mwa miradi ambayo imeibua hoja nyingi katika ripoti ya ukaguzi wa CAG ni mradi wa ujenzi wa maduka wa Mlimani City, hoja ambazo hazijatolewa majibu na baraza la chuo.
No comments:
Post a Comment