Friday, September 15

Kamanda Lyanga akerwa na wananchi wa Rufiji


Rufiji. Kamanda wa Kanda Maalum ya Rufiji, Onesmo Lyanga ameeleza kukerwa na tabia ya wananchi ya kutokutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kutowaonyesha mahali walipokuwa wakiishi wauaji baada ya polisi kutoa orodha ya majina ya watuhumiwa wanaowatafuta.
Kamanda Lyanga ameonyeshwa kusikitishwa na tabia hiyo wakati wananchi wanajua wanapoishi.
Akizungumza na wananchi leo Ijumaa mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kumaliza kuhutubia na kumtaka azungumze na amesema ilinasikitisha sana kuona wananchi hawatoi ushirikiano.
Amesema polisi ililazimika kutumia nguvu kubwa sana kuwatafuta wahalifu mahali walipokuwa wakiishi huku baadhi ya wananchi wakijua wanapoishi.
"Inasikitisha sana kuona hadi polisi tunatumia nguvu kubwa kuwatafuta wahalifu Shabani Ngunyamlile na na Hassan Njami huku mkijua walikuwa wanaishi katika Kijiji cha Rungungu, lakini mlikuwa  na mioyo migumu sana, sasa kawaoneni chumba cha kuhifadhia maiti Muhimbili, sisi tumewamaliza," amesema.
Amesema polisi na vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama wataendelea kuwakamata watu wote waliojihusisha na utekelezaji wa mauaji hayo popote pale walipo na kuwaonya watu wanaowasingizia wenzao ili waadhibiwe.
Amesema mkono wa dola ni mkubwa na wao wapo wengi kila mahali kama mbwa mwitu hivyo hawatashindwa kukabiliana na hali yoyote ile hapa nchini.

No comments:

Post a Comment