Kairuki amesema hayo leo Ijumaa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ritta Kabati aliyetaka kufahamu kaya masikini za walemavu zinasaidiwaje wakati wa utekelezaji wa miradi ya Tasaf.
"Kule kwetu kuna kaya masikini ambazo pia ni za walemavu hawawezi kutembea kufika maeneo ya ajira. Serikali ina mpango gani wa kuwajengea hata kisima ili wauze maji wakiwa walipo?" amehoji.
Kairuki amesema katika miradi hiyo kuna walemavu wenye umri wa zaidi ya miaka 18 ambao hubebwa kupelekwa maeneo yenye ajira za muda.
Amesema amepokea ushauri wa mbunge na wataangalia nini kifanyike katika awamu nyingine za miradi ya Tasaf.
Katika swali la msingi, Kabati alitaka kufahamu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango wa Tasaf.
Waziri Kairuki amesema Tasaf awamu ya tatu ilianza kutekelezwa Januari mwaka 2013 katika halmashauri 159 za Tanzania Bara na wilaya zote za Zanzibar.
Amesema kaya masikini 1.01 milioni zenye jumla ya watu takriban 5 milioni zimeandikishwa katika vijiji, mitaa na shehia 9,986.
"Hadi kufikia Agosti, kaya masikini zilishapokea ruzuku ya Sh521.9 bilioni," amesema.
Amesema kaya hizo zimetekeleza miradi ya kutoa ajira kwa walengwa 354,648 kutoka katika halmashauri 42 nchini.
No comments:
Post a Comment