Sunday, September 10

Gwajima alaani Lissu kupigwa risasi




Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema hatasita kukemea uhalifu nchini likiwemo tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Gwajima amesema hayo leo Jumapili wakati wa ibada maalumu ya kumuombea Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi Alhamisi wiki hii nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na watu ambao hawajajulikana.
Lissu hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan iliyopo mjini Nairobi, Kenya.
"Naomba tusimame kidogo nizungumze jambo, nimesema leo nitakuwa na ibada maalumu ya kumuombea Lissu. Somo langu la leo linasema damu isiyo na hatia," amesema akizungumza na waumini.
Gwajima amesema kama kiongozi wa dini hatasita kukemea tukio lililomfika Lissu na kwamba, anashangaa viongozi wenzake wa dini kukaa kimya.
Amesema neno la Mungu linasema atakayemwaga damu ya mwanadamu mwenzake naye damu yake itamwagika vivyo hivyo.
“Damu inayomwagika chini ya ardhi ina sauti, inamlilia Mungu," amesema.
Awali, wanakwaya wa kanisa hilo waliimba wimbo maalumu wa kumuombea Lissu wakihamasisha Taifa lote kufanya hivyo.
"Amani ya Tanzania inapotea, wasione tuko kimya... kwa nini haya yanatokea na watu wasiyojulikana... Watanzania wote tumuombee Lissu," haya ni baadhi ya maneno katika wimbo huo.

No comments:

Post a Comment