Watu wasiojulikana walimshambulia rais huyo wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kwa risasi zipatazo 32 akiwa ndani ya gari lake baada ya kuwasili katika makazi yake eneo la Area D, na ni risasi tano zilizompata na kumjeruhi vibaya.
Lissu, ambaye ameibukia kuwa mwanasiasa aasiyeogopa kusema analoamini, amelazwa Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi ambako amewekwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu.
Taarifa zilizopatikana jana zinasema mbunge huyo, bado anaangaliwa kwa karibu na madaktari.
Habari za shambulio dhidi yake zilitapakaa kwa kasi Ijumaa mchana, na juzi watu walikuwa wakitoa salamu za pole na kumuombea arudi katika hali yake, lakini jana kukaibuka maswali.
Gazeti hili limeyachambua maswali machache kati ya mengi ambayo yamejitokeza katika mijadala mbalimbali.
Miongoni mwa maswali hayo ni kwa nini Jeshi la Polisi halikuchukua hatua baada ya Lissu kutangaza kuwa kuna watu wanamfuatilia kwa muda mrefu.
Agosti 18, Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa anafuatiliwa na watu anaowashuku kuwa ni maofisa usalama kwa takriban wiki tatu mfululizo.
Lissu alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro pamoja na mkurugenzi wa idara ya usalama wa Taifa (TISS) kuwaeleza wakubwa wao kuhusu watu hao kwamba wapambane na wahalifu badala ya kutumia rasilimali za nchi kufuatilia raia wasio na hatia.
Hata hivyo, juzi IGP Sirro aliwaambia waandishi wa habari mjini Dopdoma kuwa Lissu, ambaye amekuwa akikamatwa mara kwa mara na polisi kutokana na kauli anazotoa katika mikutano na waandishi wa habari, hakutoa taarifa hizo katika kituo chochote cha polisi.
“Hili ni swali ambalo lingefaa zaidi aulizwe yeye. Hivyo tunaomba apone halafu mumuulize kama alitoa taarifa kituo chochote cha polisi,” alisema Sirro.
Swali hapo ni, kama iliwezekana kumkamata kutokana na anachokisema kwenye vyombo vya habari, ilishindikana vipi kufuatilia madai anayoyatoa katika mikutano hiyo?
Hata hivyo, mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi amesema jana kuwa walishamuandikia IGP Sirro kuhusu tishio dhidi ya Lissu na hajawajibu.
Jibu hilo la IGP Sirro limeibua swali jingine; kwa nini Lissu hakutoa taarifa hizo polisi?
Swali jingine ni kitendo cha polisi kutochukua hatua za haraka kuhoji wahusika wa karibu na tukio. Jana, polisi ilitangaza kuwa inamsaka dereva wa Lissu ambaye tangu wakati wa tukio alikuwa akionekana na viongozi wa Chadema na alikuwepo Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Ilikuwaje, polisi walishindwa kumchukulia kama ni mtu muhimu kumuhoji mara baada ya tukio badala ya kusubiri hadi siku tatu baadaye?
Swali jingine ni mazingira ya tukio hilo. Dereva wa Lissu alieleza kwamba kuna gari jeupe lilikuwa linawafuatilia kutoka bungeni mpaka nyumbani kwa Lissu, eneo ambalo wanakaa wabunge na mawaziri.
Kwa maelezo yake ni kwamba yeye ndiye aliyemzuia Lissu asishuke ndani ya gari na kumtaka alaze kiti wakati risasi zikipigwa kwenye gari lao.
Watu hao walikuwa wakimfuata kila siku hadi nyumbani? Na kama siku hiyo pekee walimfuata hadi anaanza kuelekea nyumbani, dereva hakuona hali ni tofauti na kuamua kupeleka gari sehemu salama au kutumia mbinu ambayo ingemthibitishia kuwepo kwa nia ovu?
Kingine kinachozua utata ni kufuatiliwa kwa gari la Lissu tangu bungeni. Hii ina maana kuwa watu hao wenye nia mbaya walikuwepo kwa muda mrefu kwenye viunga au eneo la jirani na Bunge wakimsubiri waliyemtaka.
Je, askari wanaolinda hapo na madereva wengine wa wabunge hawakuliona na kulitilia shaka gari hilo kwa siku zote kama Spika Job Ndugai alivyolieleza Bunge kuwa maeneo ya chombo hicho yako salama?
Swali jingine ni kuhusu hali ya usalama katika eneo la makazi ya wabunge na mawaziri. Je, viongozi hao wako salama? Kama washambuliaji walimudu kufyatua risasi takriban 32 na kufanikiwa kuondoka, bado wabunge na mawaziri wako salama?
Eneo wanalokaa vigogo hao lina ulinzi na wafanyakazi wa ndani. Wote hao hawakuona tukio hilo.
Kama kuna ulinzi au walinzi, walifanya juhudi gani kusaidia kudhibiti washambuliaji au kutoa taarifa ambazo zingewezesha polisi kuwabana mapema?
Hata hivyo, Jeshi la Polisi jana lilisema linawahoji baadhi ya majirani kuhusu tukio hilo.
Spika Ndugai alisema watu hao walifyatua risasi kati ya 28 na 32, kwa nini walitumia idadi hiyo kubwa kumshambulia mtu asiye na silaha?
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema shambulio hilo ni la kisiasa kwa kuwa Lissu hana adui nje ya siasa.
Hao maadui ndani ya siasa ni nani? Ni wanasiasa wa chama kingine au walio ndani ya Chadema? Ni maadui katika ngazi gani ya kisiasa ambayo inaweza kufikia kiwango cha kutaka kumuua mpinzani?
Katika hatua nyingine, taarifa zilizopatikana jana jioni kabla ya kwenda mitamboni zilisema Lissu alikuwa bado kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu wa madaktari katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi.
Hakuna kiongozi wa Chadema wala ndugu aliyekuwa tayari au kupatikana kuzungumzia maendeleo ya hali yake.
Lissu, mwanasheria wa kujitegemea na mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira, amejipatia umaarufu zaidi katika miaka ya karibuni, hasa kutokana na misimamo yake mikali na matukio ya kukamatwa kila mara na polisi na wakati mwingine kufunguiliwa mashtaka, hasa ya uchochezi.
No comments:
Post a Comment