Sunday, September 10

Askofu mkuu KKKT atoa tamko Lissu kupigwa risasi




Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo amewataka watu waovu watambue kumuondoa Tundu Lissu mmoja kutazalisha Lissu wengine maelfu.
Kauli ya Askofu Shoo inatokana na kuchukizwa na jaribio lililoshindwa la kumuua Lissu Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, ambapo watu waliokuwa na silaha walishambulia gari lake kwa risasi 32.
Katika shambulizi hilo, kati ya risasi hizo 32 zilizofyatuliwa, risasi tano zilimpata Lissu maeneo mbalimbali ya mwili wake, na sasa anatibiwa katika hospitali ya Aghakhan ya Jijini Nairobi,Kenya.

Akizungumza  kutoka Bonn Ujerumani leo , Askofu Shoo ametoa  wito maalum kwa Serikali ya Rais John Magufuli, kuhakikisha wote waliohusika na unyama huo wanakamatwa.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na taarifa za kupigwa risasi Mheshimiwa Tundu Lisu. Watanzania tunapaswa kukataa na kulaani kwa nguvu zote vitendo kama hivi,”amesema na kuongeza;-
“Mimi ninaamini kuwa nguvu zile zile za uovu zilizokuwepo tangu awamu zilizotangulia ndizo zinazoendeleza unyama kama huu. Ninamwomba Mungu ampe (Lissu) uponyaji wa haraka”.
“Tundu Lissu amekuwa mstari wa mbele kufunua ufisadi unaoendeshwa na wababe wachache. Hawa wanaona sasa wameanza kutikiswa, na kwa kuwa kwao wingi wa mali na pesa ndio mungu wao”
“Hatushangai wakitumia kila njia kuzuia  ufisadi wao usianikwe hadharani. Watajaribu kila njia kuzuia ukweli  lakini wanasahau kuwa ukweli hauzuiliki milele kuna siku utajitokeza tu”.
“Kumwondoa Lissu mmoja kutazalisha Lissu maelfu. Wito wangu kwa serikali ya Dr Magufuli ni huu,  kwamba watu wote waliohusika wasakwe na wafikishwe mbele ya sheria,”.
Dk Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT amesema Serikali yoyote makini inajua namna ya kuulinda upinzani kwani ukitumika vizuri unakuwa kioo cha serikali cha kujitazama.
Mara kadhaa, kiongozi huyo amekuwa akitoa hotuba zenye hisia kali akitaka Serikali na vyombo vyake vya usalama kuchukua hatua, kutokana na kuongezeka kwa matukio ya ajabu ya kihalifu.

No comments:

Post a Comment