Lissu alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi tano Alhamisi wiki hii nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu jijini Nairobi, Kenya.
Kaimu Katibu Mkuu wa umoja huo, Shaka Hamdu Shaka amesema hayo leo Jumapili, akilitaka Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) lisione kwamba wao ndio wameguswa na tukio la Lissu kupigwa risasi kuliko Watanzania wengine.
“Ukweli ni kwamba sote tumeguswa na tukio hilo, jambo la msingi ni kuviachia vyombo vya Dola vifanye upelelezi,” amesema.
Shaka amesema kuna viongozi wengine walikufa kwa kupigwa risasi na uchunguzi ukafanyika kupitia vyombo vya ulinzi na usalama.
Kauli ya UVCCM imetolewa baada ya Bavicha kukaririwa ikiitaka Serikali kuunda tume huru itakayochunguza matukio ya uvunjifu wa amani likiwemo la kupigwa risasi Lissu.
Bavicha imesema tume hiyo inapaswa kuihusisha Chadema kwa kuwa viongozi wake wengi wamekumbwa na vitendo hivyo. Shaka amesema Bavicha iache kuingilia utaratibu wa upelelezi.
Amesema Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume aliuawa kwa kupigwa risasi.
Kiongozi mwingine aliyeuawa kwa risasi amesema ni naibu waziri katika Serikali ya Awamu ya Pili, Nicas Mahinda.
Katika duru za kimataifa, Shaka alitoa mfano wa aliyekuwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy na Rais wa Misri, Anuar Saadat ambao waliuawa kwa kupigwa risasi.
“Matukio ya ujambazi yanayofanywa na watu wasiojulikana hutokea hata katika mataifa makubwa na mara nyingi upelelezi wake huchukua muda mrefu kwa wahusika kukamatwa,” amesema.
Amesema Bavicha waache kuyahusisha matukio makubwa yanayochukua uhai wa watu na masuala ya kisiasa.
Shaka amesema UVCCM inamuunga mkono Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliposema huu si wakati wa kunyoosheana vidole vya lawama bali viachiwe vyombo vya usalama vitimize wajibu wake.
“Mbowe ametamka matamshi yaliyopevuka kifikra, kiupeo na kisiasa,” amesema Shaka.
Amsema Bavicha wasitumie tukio la Lissu kupigwa risasi kama jukwaa lao la kufanya siasa.
Shaka amesema umoja huo unashauri wananchi wakaongozwa kwa busara kuliko ushabiki ambao unaweza kuliingiza Taifa katika machafuko.
No comments:
Post a Comment