Saturday, September 23

Asilimia 75 ya kadi za mwendokasi hazitumiki


Mtendaji Mkuu wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Lwakatare amesema kati ya kadi 200,000 zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumika katika Mfumo wa Mabasi Yaendayo haraka ni kadi 50,000 hadi 60,000 ndizo zinazoonekana kutumiwa na wananchi katika mfumo huo.

Amesema kadi ambazo zinatumika kwa sasa ni sawa na asilimia 25 tu huku asilimia 75 zikiwa  ziko mifukoni mwa wateja ambao wamechukua kadi mara mbili.

Mhandisi Lwakatare amesema  kwamba kutotumika kwa kadi  hizo nyingi kumechangia kuwepo kwamisururu ya abiria kwenye vituo vya mabasi yaliyopo kwenye mfumo huo.
“Kusudi ni kwamba kadi moja kwa mtu mmoja, lakini inaonekana mtu mmoja anamiliki kadi zaidi ya moja, jambo ambalo si sahihi,” ameeleza.
Amefafanua kwamba wakati utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo Serikali ilinunua kadi 200,000 kutokana na makadirio iliyoyafanya kabla ya kuanza kutoa huduma.
Amesema  kadi hizo zilipaswa kutumiwa na wananchi wanapohitaji kusafiri lakini imebainika kwamba nyingi ya kadi hizo hazitumiki.
“Takwimu zinaonyesha kati ya kadi 200,000 zilizonunuliwa ni asilimia 25 hadi 30 zinazotumika, hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa kadi katika mfumo,” amesema.
Kufuatia hali hiyo Mtendaji Mkuu amewataka Wananchi wanaozimiliki kadi hizo wazitumie ili kurahisisha usafiri kwani ndizo zilizokusudiwa kutumika katika mradi.

Mhandisi Lwakatare aliongeza kuwa kulingana na takwimu zilizopo  wananchi 200,000 hadi 250,000 ndiyo  wanaotumia huduma hiyo kila siku ni dhahiri kuwa endapo kadi hizo zingekuwa zinatumika kusingekuwa na msururu wa abiria kupanga foleni ya kukata tiketi.
Kuhusu suala la kuongeza kadi nyingine katika mfumo huo ili ziendane na mahitaji ya sasa ya ongezeko la watumiaji wa huduma hiyo, Mhandisi Lwakatare alisema kuwa Serikali inalipa kipaumbele suala hilo ambapo kufikia sasa utaratibu wa kumpata mtoa huduma wa kukusanya nauli unaendelea vizuri.
Amesema kuwa mtoa huduma huyo atakapopatikana ndiye atakuwa na jukumu la kuongeza kadi, kuzisimamia na kukusanya nauli.
Hata hivyo , Mhandisi huyo alisema kwamba kuna wananchi wengi ambao wanaishi  nje ya mkoa wa Dar es Salaam ambao hawatumii usafiri huu na wamechukua kadi hizo.

“Nawashauri nyie ambao hamtumii kadi hizi mrudishe ofisi za Udart au muwape hata ndugu zenu wazitumie kwani haziharibiki  zaidi ya kuoengezewa pesa tu’’alisema

No comments:

Post a Comment