Saturday, August 26

Wamiliki wa baa zilizobomolewa waendeleza biashara kwenye magofu yao



Dar es Saalam. Wamiliki wa baa zilizobomolewa kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro eneo la Kimara Stop Over wameendelea kufanya biashara kwenye masalia ya majengo yao, wakitundika miamvuli kwa ajili ya kuwakinga wanywaji.
Baa zaidi ya saba zimebomolewa na kati ya hizo tano pia imo Hoteli ya 5N iliyopo eneo la Suka kutokana na majengo hayo kuwa ndani ya mita 121.5 za hifadhi, kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Kuu.
Waandishi wa Mwananchi walishuhudia baadhi ya wafanyakazi wa baa na vibanda vya biashara wakiwa wametundika miamvuli kwa ajili ya kivuli kwa wateja wao.
Msimamizi wa Tulivu Bar aliyekataa kutaja jina lake, alimwambia mwandishi kuwa wataendelea na biashara eneo hilo.
“Hata hatujui. Sisi tunaendelea tu kufanyabiashara hapa mpaka (Rais John) Magufuli aje mwenyewe,” alisema mfanyakazi huyo.
Alisema hawawezi kuacha kufanya biashara kwa kuwa inawasaidia kuendesha maisha na hawana pa kwenda, hivyo wanawasubiri Tanroads waende kutoa vifusi na mabati ili wajenge vibanda kwenye magofu ya baa zao.
Pia, wamiliki wa baa hizo huendelea na biashara hata nyakati za usiku wakitumia taa ndogo za betri na wengine kandili, baada ya huduma ya umeme kukatwa kutokana na bomoabomoa.
“Biashara inaendelea japo tunawahi kufunga, lakini tunafanya biashara chini ya miamvuli kama unavyoona,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa baa ya Tulivu.
Baa nyingine ambayo inaendelea na biashara ni Bliz Pub ambayo mbali na jengo kubomolewa, wateja wao hujisitiri kwenye magofu yaliyosalia nyakati zote za mchana na usiku.
Mbali na baa, wamiliki wa maduka ya huduma mbalimbali kama za fedha, vinywaji, mama lishe na wauza chipsi waliobomolewa, nao wameendeleza biashara kwenye majengo yaliyobolewa, wakidai wanafanya hivyo kwa kuwa hawana sehemu ya kwenda.
“Tunafanyia nje biashara maana vibanda vimebomolewa na hatuna pa kwenda,” alisema Hamisi Juma ambaye alikuwa na kibanda cha kukaanga chipsi eneo la Stop Over.
Mfanyabiashara mwingine ambaye alikutwa akifanya biashara nje eneo la Kimara Suka, Juma Seleman, alisema amesikitishwa na kitendo cha kubomolewa kibanda chake.
“Kwa sasa sina sehemu maalumu ya kwenda hivyo nimeamua kuendelea na biashara hapa nje,” alisema.
“Kwa kweli mpaka sasa sijui nitaenda wapi maana sina eneo jingine. Hapa ndipo nilipopategemea.”
Alisema mbali na kufanyia nje hali ya biashara kwa sasa si nzuri kwa sababu walikuwa wanategemea wafanyabiashara wengine waliokuwapo maeneo hayo kama wateja wao.
Lilian Michael anayefanya biashara ya chakula Kimara Stop Over alisema kwa sasa anafanya biashara yake katika mazingira magumu baada ya kibanda chake kubomolewa.
Alisema ataendelea na biashara yake kwenye mabaki hayo ya kibanda chake.
“Nimelipa kodi hapa hata miezi mitatu haijaisha, nitaendelea na biashara yangu hapa katika mazingira haya hadi hapo nitakapopata pesa ya kulipia sehemu nyingine,” alisema.
Alisema juzi Tanroads walivyokwenda kubomoa na baadhi ya vitu vyake viliharibika, hasa vyakula.
“Walikuja tukiwa tayari tumeshaanza kupika, vyakula vyetu vikamwagika. Kwa kweli kwangu jana (juzi) ilikuwa hasara, lakini sina jinsi. Ndio nchi yetu hii,” alisema.
Wakati Lilian akilalamikia biashara yake ya chakula kuwa ngumu, hali hiyo pia ipo kwa muuza duka la vinywaji baridi aliyejitambulisha kwa jina la Richard Nkwasi aliyesema hajui aende wapi kuendelea na biashara yake.
“Nilipanga hapa tangu Januari Mosi na nililipa mwaka mzima. Sasa leo naenda kupanga wapi? Na kwa pesa ipi?” alihoji.
“Jana(juzi) walikuja tu hapa ghafla wakaanza na zoezi lao kama unavyoona chupa zimevunjika na baadhi ya mayai hapa yamevunjika. Lakini sina jinsi, siwezi kupingana nao ila mimi hapa siondoki,” alisema.
Majengo hayo, yanayohusisha nyumba za makazi na biashara, yanabomolewa kupisha upanuzi wa barabara ya Ubungo Kiluvya ambayo inatumiwa na magari mengi yanayoingia jijini Dar es Salaam.
Imeandikwa na Jackline Masinde, Asna Kaniki na Hidaya Nyanga.

No comments:

Post a Comment