Saturday, August 26

Manji kutumia mashahidi 15 kumtetea


Dar es Salaam. Mfanyabiashara Yusuf Manji atatumia mashahidi 15 kujitetea dhidi yake katika kesi inayomkabili ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin.
Mfanyabiashara huyo, ambaye katika hati ya mashtaka ametajwa kwa jina la Yusufali Manji sasa atatakiwa kupeleka mashahidi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana kutoa uamuzi kuwa ana kesi ya kujibu ikiwa ni siku mbili tangu upande wa mashtaka ufunge ushahidi wake uliotolewa na mashahidi watatu.
Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka ameridhika mshtakiwa ana haki ya kujitetea na kuita mashahidi.
Wakili Hudson Ndusyepo anayemwakilisha Manji katika kesi hiyo alisema mteja wake atajitetea kwa njia ya kiapo na ana mashahidi 15.
Pia, aliiomba Mahakama kutoa hati ya wito (samansi) kwa ajili ya mashahidi hao.
Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 30 na 31 itakapoendelea kusikilizwa kwa Manji kuanza kujitetea.
Upande wa mashtaka ambao awali ulisema ungeita mashahidi wasiozidi 10, ulifunga ushahidi wiki hii kwa kuwaita watatu kutoka Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mashahidi hao walieleza namna sampuli ya mkojo wa Manji ilivyochukuliwa, uchunguzi uliofanyika na matokeo yake.
Manji alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 16 akidaiwa kati ya Februari 6 na 9 katika eneo la Sea View, Upanga wilayani Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.
Katika ushahidi wa upande wa mashtaka, ilielezwa mahakamani kuwa dawa aina ya benzodiazepines ilikutwa kwenye sampuli ya mkojo wa Manji, na ikadaiwa kuwa dawa hiyo pia hutumika hospitalini kutuliza maumivu makali au kumpatia mtu usingizi.
Katika ushahidi huo, ilielezwa kuwa hatua ya pili ya uchunguzi wa sampuli hiyo ya mkojo kwa kutumia mashine ya HPLS, ulionyesha una dawa aina ya morphine ambayo ni metabolites (metaboli) ya heroin.
Mmoja wa mashahidi hao alieleza ni vigumu kupata heroin kwenye mkojo kwa sababu inapokuwa mwilini ndani ya dakika 20 au 60 hubadilika na kuwa morphine, dawa aliyosema pia hutumika hospitalini.
Manji ambaye baada ya kusomewa shtaka alikana, alipewa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya Sh10 milioni katika kesi hiyo, lakini kwa sababu ana kesi nyingine aliyonyimwa dhamana hivyo bado yupo mahabusu.
Katika kesi nyingine ya uhujumu uchumi inayomkabili Manji na wenzake watatu mahakamani hapo, upande wa mashtaka Agosti 31 utaeleza hatua iliyofikiwa katika upelelezi.
Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alidai jana kuwa upelelezi haujakamilika na siku itakapotajwa wataeleza hatua iliyofikiwa.
Hakimu Simba aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi mapema ili matokeo ya kesi yajulikane. Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambaye jana hakuwapo ikielezwa kuwa amefiwa.
Manji na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa Taifa wakidaiwa kukutwa na vitambaa vinavyotengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni na mihuri. Washtakiwa wengine ni Deogratius Kisinda (28), Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43). Washtakiwa wote wako mahabusu kwa kuwa kesi yao haina dhamana.

No comments:

Post a Comment