Ni usemi unaotosha kueleza kitendo cha Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele cha kujifungia ofisini kwake kwa zaidi ya saa tano baada ya maofisa ya Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA) kufika eneo hilo kwa mahojiano, kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imezipata.
“Profesa Manyele hakuamini macho yake pale kiongozi wa timu ya DCEA alipobisha hodi ofisini kwake kumueleza kuwa wanahitaji kuondoka naye kwa ajili ya mahojiano,” alisema mmoja wa DCEA baada ya mwandishi wetu kufika muda wa tukio hilo lililotokea Jumatano saa 7:00 mchana na kukuta wameshaondoka naye.
Maofisa hao wa DCEA walikuwa wakitaka kuanza mahojiano na Mkemia Mkuu kuhusu uingizwaji holela wa shehena za kemikali bashirifu, ambazo mamlaka hiyo inahisi zinatumika pia kutengenezea dawa za kulevya, tofauti na matumizi yanayokusudiwa.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, Profesa Manyele alionyesha kuhamanika na kuchanganyikiwa na wito huo na kuwaomba maofisa hao wamruhusu aingie ofisini kwake ili ashauriane na mwanasheria wake nini cha kufanya.
Kitendo cha kumruhusu aingie ofisini kwake peke yake kilimpa ofisa huyo mkubwa serikalini nafasi ya dhahabu ya kujaribu kukwepa ‘watesi’ wake wasiondoke naye.
Mwananchi ilimshuhudia Profesa Manyele akiwa na hali ya hofu na wasiwasi wakati akiingia chumba cha ofisi yake iliyopo ghorofa ya chini ya jengo lililo jirani kabisa na Ikulu jijini Dar es Salaam. Huo ukawa mwanzo wa mvutano mkali kati yake na maofisa wa DCEA.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, baada ya kuona muda unakwenda bila kutoka, maofisa ya DCEA walijaribu kufungua mlango na kugundua ulikuwa umefungwa kwa ndani huku Profesa Manyele akiapa kutoufungua. Baada ya maofisa wa DCEA kujaribu mbinu zote ikiwamo kumuomba katibu mukhtasi wake ampigie simu, Mkemia Mkuu aliendelea kukataa kutoka.
Hali hiyo ilisababisha hali ya sintofahamu kwa wafanyakazi wachache waliokuwapo ofisini hapo wakati maofisa hao wa DCEA wakiendelea na juhudi za kumtaka afungue mlango.
Badala yake aliwaeleza kwa njia ya simu kuwa hawezi kwenda popote kwa sababu hata ofisa mmoja mwandamizi wa Wizara ya Afya amemtaka asitoke.
Baada ya saa mbili, kwa mujibu wa habari hizo, alifika mwanasheria mmoja wa Ofisi ya Mkemia Mkuu na kumpigia akimtaka atoke, lakini pia akakataa. Tangu wakati huo hakupokea tena simu za ndani wala za nje.
Muda ulipozidi, mwanamama mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mwanasheria wa Wizara ya Afya, alifika ofisi hizo na kushauriana na maofisa wa DCEA na baadaye kumpigia Profesa Manyele akimuomba atoke nje kwa ombi la Katibu Mkuu.
Wito huo haukutosha kumshawishi Profesa Manyele aliyemwambia mwanasheria huyo kwa njia ya simu kuwa haamini kama ametumwa na Katibu Mkuu.
Ilibidi zifanyike juhudi za ziada kuepusha watendaji wa DCEA kuvunja mlango ili waondoke naye. Saa 11:00 jioni yalifanyika mawasiliano yaliyoonyesha kuwahusisha wakuu wa wizara ya afya na viongozi wa DCEA ambayo hatimaye yalimshawishi Mkemia Mkuu afungue mlango na kutoka nje, akionekana kujawa hofu, kwa mujibu wa shuhuda huyo.
Aliruhusiwa kuondoka na dereva wake hadi makao makuu ya DCEA Upanga jijini Dar es Salaam ambako alihojiwa hadi saa 4:00 usiku kuhusu utoaji holela wa vibali vya kuingiza kemikali bashirifu nchini kabla ya kuachiwa na kuhojiwa tena siku iliyofutia.
Kwa nini alihojiwa
DCEA ilimhoji Profesa Manyele kwa siku mbili mfululizo tangu Jumatano ikitafuta ukweli kuhusu ukiukwaji wa utaratibu wa utoaji vibali vya kuingiza kemikali bashirifu nchini.
Hili limekuja wakati kukiwa na wimbi la ukamataji wa maelfu ya lita za kemikali bashirifu zinazoingizwa nchini kinyume cha utaratibu.
Mwezi uliopita DCEA ilikamata lita 200,000 za aina tofauti za kemikali hizo hatari katika Bandari ya Dar es Salaam zilizoingizwa kinyume cha sheria kutoka Swaziland.
Taarifa ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa kampuni ya Diana Rose Spare Parts iliyoagiza shehena hiyo haijawahi kuomba usajili wa kufanya biashara ya kemikali wala kukaguliwa na kuthibitishwa, lakini Mkemia Mkuu mwenyewe aliwathibitisha kuwa ndio waingizaji na watumiaji wa kemikali hizo.
Mkemia huyo pia anadaiwa kutoa hati ya kufanya biashara ya kemikali kwa kampuni ijulikanayo kwa jina la Hamid Ibrahim Saambaya ambayo haitambuliwi na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela). Kampuni hiyo pia haikuwahi kuomba kibali cha kufanya biashara ya kemikali.
Mwananchi pia imepata taarifa za uhakika kuwa kampuni za Hamid Ibrahim Saambaya na Diana Rose Spare Parts ni mali ya mfanyabishara wa jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa kwa sasa).
Kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali za Viwanda na Walaji (Udhibiti na Usimamizi) ya mwaka 2003, ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ndiyo yenye jukumu la kisheria kufanya uchunguzi wa kina kwa kampuni zote zinazotaka kufanya biashara ya kemikali kabla ya kuzithibitisha na kutoa vibali.
Ufuatiliaji wetu umebaini pia kuwa wakati nyaraka zikionyesha kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu ilitoa kibali cha kufanya biashara ya kemikali kwa kampuni ya Diana Rose Spare Parts Julai 7, 2017 wakati shehena ya lita 200,000 zilizokamatwa, iliingia nchini Juni 22, 2017.
“Wakati kontena ziko bandarini ofisi yake ikatoa import permit (kibali cha kuagiza). Hii ni mara ya kumi na moja kwa kampuni hii kuingiza mzigo kama huo. Hawa hawana hati ya usajili, lakini import permit walipewa,” anasema ofisa mmoja wa DCEA aliyekuwapo wakati wa ukamataji.
Ingawa kampuni hiyo haikidhi vigezo vya kuagiza, na maghala yake yaliyopo eneo la Mbezi Louis ni yadi ya magari, Ofisi ya Mkemia Mkuu iliipa alama 96 za ubora kupitia fomu maalumu ya ukaguzi wa eneo la kuhifadhiwa kemikali.
Mapungufu hayo yaliilazimu DCEA kumuandikia Mkemia Mkuu atoe maelezo kuhusu Diana Rose Spare Parts.
Katika barua yake ya Agosti mosi, 2017, Profesa Manyele anaeleza kuwa mchakato wa kuisajili kampuni hiyo ulisitishwa Juni 2017.
Siku sita baadaye, DCEA ilimwandikia tena Mkemia Mkuu ikiomba hati ya kampuni hiyo, ndipo alipotuma hati inayoonyesha ilisajiliwa Juni mosi, 2016 tofauti na barua ya kwanza kuwa mchakato wa kuisajili kampuni hiyo ulisitishwa.
Asimamisha wasaidizi wake
Katika hatua nyingine, Profesa Manyele aliwasimamisha kazi maofisa watatu waandamizi wa ofisi yake kwa madai ya kumshauri vibaya. Taarifa zinawataja maofisa hao kuwa ni Evenlight Matinga, ambaye ni meneja usajili wa kemikali na Msigara Mkama na Kagera Mwishemi (wakaguzi waandamizi).
No comments:
Post a Comment