Mahujaji hao wapo Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakisubiri safari hiyo.
Wakizungumza na Mwananchi jana, baadhi ya mahujaji hao walisema kuwa kila mmoja wao alilipa kati ya Sh 8.5 milioni hadi Sh10 milioni kwa kampuni hiyo ambayo jina tunalihifadhi kwa sababu za kimaadili.
Mmoja wa mahujaji hao, Ummy Sekibo kutoka jijini Dar es Salaam alisema kila mmoja alikuwa akilipa fedha hizo kwa vipindi tofauti na kwamba wapo waliolipa tangu mwishoni mwa mwaka jana.
“Tulikuwa tunalipa fedha kidogo kidogo, tukafanya hatua zote za kupata passport (hati ya kusafiria) ambazo tuliwakabidhi wao kwa sababu kwenda kuhiji ni kwa kundi, hivyo tulilazimika kujikusanya,” alisema.
Ummy alisema alilipa Sh10 milioni na kwamba hana uhakika kama watafanikiwa kusafiri.
Hujaji mwingine, Hussein Said Seif alisema awali waliambiwa kwamba wangesafiri Agosti 23 lakini tarehe hiyo ilipofika hawakuweza kuwaona viongozi wa kampuni iliyokuwa ikitaka kuwasafirisha.
Alisema siku ya pili walilazimika kwenda ofisi zao zilizopo maeneo ya Kariakoo na kufanikiwa kuwakuta baadhi ya viongozi ambao waliwaahidi kwamba, wangesafiri jana na hivyo kutakiwa kuripoti uwanja wa ndege saa 8:00 mchana.
“Leo (jana) imefika hatuwaoni, tumejaribu kuwapigia simu hakuna hata kiongozi mmoja aliyepatikana. Kwa hiyo tupo hapa tumejikusanya na hatujui tufanye nini,” alisema Hussein.
Alisema walichofanikiwa kupewa ni mabegi yenye nguo na vifaa kwa ajili ya hija, lakini hakuna kitu kingine chochote.
Kwa upande wake, Mariam Suleiman, ambaye pia alilipa Sh8.5 milioni, alisema hali hiyo inawakosesha raha na kwamba wamelazimika kutoa taarifa kwa mufti ili awasaidie.
“Tupo hapa na hatujui hatma yetu, tupo wengi zaidi ya 100 na wote tumeshalipa fedha kwa watu hawa ambao kwa kweli hatuna uhakika kama kweli watatusafirisha au la,” alisema.
Alisema kuna watu wamewaeleza kwamba safari hiyo haiwezekani.
No comments:
Post a Comment