Hayo yameanishwa kwenye kitabu kiitwacho Tanzania’s Industrialisation Journey, 2016-2056 kilichoandaliwa na Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi (CEOrt) na kuzinduliwa leo Agosti 29 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.
Mmoja wa waandishi wa kitabu hicho na Mwenyekiti wa CEOrt, Ali Mufuruki amesema wamekiandika kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuifanya Tanzania nchi ya viwanda.
Amesema ili kufikia dhamira hiyo, lazima kuwepo vipaumbele ili kuondoa uwezekano wa kutumia fedha nyingi kuwekeza katika maeneo mengi bila kuwa na tija.
“Ipo haja ya kuchagua maeneo machache ya kuanzia kwa kuweka nguvu kubwa ili kupata mafanikio,” amesema.
Amesema ili kuwa na viwanda vinavyofanya uzalishaji ni lazima kuwepo umeme wa uhakika na si wa kubahatisha.
Pia, amesema ndani ya kitabu hicho wameelezea umuhimu wa kuwa na mitaji ya uhakika katika miradi inayoratibiwa na nchi kuliko kutegemea kutoka nje.
“Tukiwa na uhakika wa mitaji tunaweza kuendesha miradi yetu vizuri, kwa sababu mtu wa nje anaweza asione umuhimu wa mradi hivyo akaamua asitoe fedha lakini wenyewe tukiwa na uhakika tutakuwa na mahali pa kuanzia,” amesema.
Akizungumzia kitabu hicho, Waziri wa Fedha, Dk Mpango amesema kimewasaidia watunga sera kubaini na kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda.
“Kumekuwepo na ombwe kwa muda mrefu kati ya Serikali na sekta binafsi ambao ndiyo waendeshaji wakubwa wa viwanda. Mara nyingi tumekuwa tunaandika wenyewe watunga sera lakini inakosekana sauti ya sekta binafsi ambao wanaweza kusema tufanye nini ili tufanikiwe kwa nguvu na haraka zaidi,” amesema.
No comments:
Post a Comment