Utafiti mpya wa asasi ya kiraia ya Twaweza uliozinduliwa leo Agosti 30 unabainisha idadi ya wananchi wanaosubiri kumuona daktari kwa zaidi ya saa moja imeshuka kutoka asilimia 25 mwaka 2014 hadi asilimia 20 mwaka huu.
Hii ina maana kuwa, kwa sasa ni mtu mmoja kati ya watu watano wanaoenda kituo cha afya ndio husubiri zaidi ya saa moja kupata huduma kulinganisha na mtu mmoja kati ya wanne miaka mitatu iliyopita.
“Upo ushahidi unaoonyesha kuwa, muda wa kusubiri huduma katika vituo vya afya umepungua kidogo kulinganisha na miaka ya nyuma ambayo wananchi saba kati ya 10 (asilimia 70) walisubiri chini ya saa moja mwaka 2014,” inasomeka sehemu ya ripoti ya utafiti huo unaoitwa, “Afya kwanza! Wasemavyo wananchi kuhusu huduma za afya. Muhtasari unatokana na takwimu za Sauti za Wananchi”.
Mbali na mafanikio hayo, utafiti huo wa toleo la 19 la Sauti za Wananchi unabainisha kuwa, wananchi sita kati ya 10 (asilimia 61) wanapata huduma za afya katika vituo vya afya vya Serikali, kiwango ambacho kimesalia kama ilivyokuwa mwaka jana.
Mwaka 2014, idadi ya wananchi waliokuwa wakipata huduma za afya kwenye vituo vya umma ilikuwa ni takriban watano kwa kila 10 sawa na asilimia 45.
Utafiti huo uliohusisha sampuli ya wananchi 1,801 unaeleza kuwa, ni asilimia 16 hadi 20 ya waliohojiwa huenda hupata matibabu kwenye vituo vinavyomilikiwa na watu binafsi, makanisa au mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Idadi hii haijabadilika sana kati ya mwaka 2014 na 2017,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo iliyofanywa kwa njia ya simu kati ya Mei 11 hadi 25 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment