Friday, August 25

Serikali yamwaga ajira 52,000 waombaji wakionyesha udhaifu



Rais John Magufuli 

Rais John Magufuli  
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikimwaga ajira 52,000 nchini kwa mwaka wa fedha 2017/18, waombaji wameendelea kuonyesha udhaifu ikiwamo namna ya kutuma maombi yao.
Tayari Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa umma imemwaga ajira hizo, lakini tatizo limeonekana kwa baadhi ya waombaji kutokukubaliwa maombi yao kutokana na udhaifu waliouonyesha katika utumaji maombi yao.
Ajira hizo ni kwa ajili ya watumishi wa kada mbalimbali ikiwamo walimu wa Sayansi, sekta ya afya na maeneo mengine kulingana na mahitaji husika.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha sekretarieti hiyo, Riziki Abraham alisema jana kuwa, baadhi ya vibali ambavyo mchakato wake umeshakamilika ni pamoja na kile cha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambayo imepokea maombi ya kazi 6,852, lakini walioitwa kwenye usaili kutokana na kukidhi vigezo walikuwa 2,949.
Kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), maombi yaliyopokewa ni 9,022 na walioitwa kwenye usaili ni 1,550 ambapo kwa sasa waliochaguliwa wako kwenye vituo vyao vya kazi.
Alisema taasisi ambazo michakato inaendelea ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas) ambacho maombi yaliyopokewa ni 2,273 huku waliokidhi vigezo vya usaili wakiwa watu 144.
Riziki alisema maombi ya Wakala wa Serikali Mtandao (e-GA) yaliyopokewa yako 5,732 na walioitwa kwenye usaili ni 4,054, huku Mamlaka ya Mapato (TRA) ikiwa na nafasi za kazi 400 na maombi yaliyopokewa na sekretarieti hiyo ni 56,815 ambapo waombaji waliwasilisha kwa njia ya kielekroniki na waliokidhi na kuitwa kwenye usaili ni 29,674.
“Pamoja na nia njema ya Serikali katika sekta ya ajira, lakini bado waombaji wameonyesha udhaifu katika kujua namna ya kutuma maombi ya kazi ambayo yamesababisha kutokukubaliwa kutokana na sababu hizo,” alisema.     

No comments:

Post a Comment