Arusha. Wanafunzi watatu; Doreen Mshana, Wilson Tarimo na Sadia Awadh walionusurika katika ajali iliyoua wenzao 32, walimu wawili na dereva mmoja wamerejea darasani jana.
Mkuu wa Shule ya Lucky Vincent Efraim Jackson alisema jana kuwa wanafunzi hao waliokuwa wakitibiwa nchini Marekani, wameonyesha ari ya masomo na wamewaandalia programu maalumu itakayowawezesha kusoma kwa haraka na kuelewa sehemu kubwa ya mtalaa ambao hawakuusoma wakati wakiwa kwenye matibabu.
“Hivi ninavyoongea na wewe wapo kwenye jaribio la kuwapima. Wapo darasani na wenzao lakini tutakuwa tunawatenga na kuwafundisha kwa saa nne hivi kwa siku ili waweze kufidia sehemu waliyoikosa awali,” alisema.
Lazaro, Lema wampinga RC
Wakati watoto hao wakirejea shule kuendelea na masomo, viongozi wa kisiasa wameendelea kuzozana kuhusu rambirambi za ajali hiyo.
Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuzikabidhi familia tatu za watoto hao Sh23.2 milioni ambazo awali zilikuwa za rambirambi, Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wamepinga hatua hiyo.
Juzi, Gambo alikabidhi fedha hizo na kusema Serikali na wadau walichangia kwa ajili ya shughuli nzima za mazishi ya marehemu 35 waliofariki kwenye ajali hiyo na hivyo kukabidhi kiasi kilichobaki kwa familia hizo ili ziwasaidie.
Katika mapokezi ya watoto hao kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Agosti 18, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghirwa kwa niaba ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu aliagiza Serikali mkoani Arusha kutoa Sh20 milioni ambazo ni sehemu ya michango hiyo kwa ajili ya mfuko wa elimu wa Stemm kusomesha watoto hao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika eneo la Sanawari, Meya Lazaro alisema badala ya Gambo kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais, amekabidhi fedha zilizobaki kwa familia jambo ambalo ni kinyume.
Alisema yeye (Lazaro) alikamatwa na kuwekwa mahabusu baada ya kumtaka Gambo arejeshe rambirambi na kusisitiza kwamba kinyume chake kiongozi huyo amerejesha fedha hizo sehemu ambayo si sahihi.
“Niliwekwa ndani wakati wa rambirambi, Makamu wa Rais ameagiza Gambo arejeshe fedha za rambirambi alizokusanya badala ya alivyoelekezwa yeye amewaita watoto ofisini kwake,” alisema Lazaro.
Wakati Lazaro akisema hayo, Lema alisema alichofanya Gambo ni funzo kwa viongozi wengine kuacha kupokea maagizo ya mdomo kutoka kwa viongozi wa Serikali.
“Viongozi wamekuwa wakitoa maagizo, kamateni wapinzani na kuwapiga, sasa kumbe kama hamjapewa maandishi ipo siku yatawarudia,” alisema.
Alisema kilichofanywa na Gambo ni kupingana na maagizo ya Makamu wa Rais aliyesema fedha ziwekwe mfuko wa elimu, yeye Gambo amezigawa.
Hata hivyo, Lema alisema hayo yanatokea kutokana na msiba huo tangu ulipotokea ulitawaliwa na mgawanyiko na hila za kisiasa na sasa Mungu anafanya miujiza viongozi kugongana.
No comments:
Post a Comment