Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema jana kuwa: “Jana tumekamata malori mawili yaliyokuwa yanasafirisha sukari isiyo na vibali kutoka Bagamoyo kwenda Dar es Salaam. Mapambano dhidi ya magendo yanaendelea nchi nzima.”
Alisema bidhaa zinazoingizwa nchini kinyume na taratibu ni hatari kwa afya za walaji kwa kuwa hazijakaguliwa na mamlaka husika na huikosesha Serikali mapato.
“Hatutaki kuona viwanda vyetu vinaathirika kwa ushindani usio sawa,” alisema.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kati ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira na wafanyabiashara, kujadili fursa za uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi, Ofisa Mtendaji wa Utawala wa TPC, Jaffar Ally alisema kiwanda hicho kimepoteza soko kutokana na biashara za magendo.
“Kwa miaka 10 mfululizo, bei ya Kenya ilikuwa juu kulinganisha na sisi, lakini baada ya kuruhusu sukari ya bei rahisi kutoka Brazil mambo yamebadilika,” alisema Ally.
Alifafanua kuwa inaaminika zaidi ya tani 250,000 ziliingizwa Kenya kupitia Bandari ya Mombasa na kusababisha soko lake kufurika kiasi cha kuathiri mikoa ya Kaskazini ambako TPC inauza bidhaa zake.
Mtendaji huyo alimuomba Mghwira na kamati yake ya ulinzi na usalama kulitizama jambo hilo kwa kuwa lina athari katika soko la sukari nchini.
Sukari hiyo inayodaiwa kuingizwa nchini kwa usafiri wa pikipiki, imekuwa ikiuzwa kati ya Sh95,000 na Sh98,000 kwa mfuko wa kilo 50 wakati ya TPC inauzwa Sh110,000.
Hata hivyo, Mghwira alisema Serikali itawezesha mazingira rahisi ya biashara na kuondoa vikwazo kwa wawekezaji. Alisema anataka mkoa wake uwe mfano katika maendeleo ya kiuchumi.
No comments:
Post a Comment