Tuesday, August 29

Hoteli kuvunjwa kupisha makazi ya Waziri Mkuu



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa 
Dodoma. Viwanja zaidi ya 22,000 na hoteli za kifahari katika Manispaa ya Dodoma zinatarajiwa kuondolewa ili kupisha makazi ya ofisi ya Waziri Mkuu.
Hali hiyo inakuja ikiwa ni miezi 11 tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipohamia rasmi mkoani Dodoma.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi alisema jana kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuboresha mji huo ambao kwa sasa umebeba jukumu la makao makuu.
Alisema mpango wa kuzivunja hoteli hizo ni kawaida kwa kuwa hawawezi kuruhusu zikaendelea wakati zipo karibu na makazi ya Waziri Mkuu eneo la Mlimwa.
Hoteli zilizopo karibu na makazi hayo ni African Dream, Royal na nyingine mpya.
Pia, Kunambi alitoa nafasi ya mwezi mmoja watu waliopewa barua za viwanja wawe wamekamilisha kuvilipia kabla ya maeneo hayo kutwaliwa.
Naibu Meya wa Manispaa, Jumanne Ngede, alisema mipango ya sasa ndani ya manispaa hiyo ni tofauti na zamani hivyo wanaweza kuamua jambo na kulitekeleza mara moja.
Ngede alisema kuondolewa kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kumeiwezesha manispaa kuvuka lengo la makusanyo ya ndani kutoka Sh3.9 bilioni walizolenga hadi kufikia Sh4.6 bilioni.
Alisema mwaka wa fedha 2017/18 wanatarajia kukusanya zaidi ya kiwango hicho.
Mkazi wa Manispaa ya Dodoma, Rehema Yobwa, alisema mikakati inayowekwa na kutekelezwa na viongozi hao, inashindwa kutofautisha kati ya CDA na manispaa katika masuala mazima ya ardhi.

No comments:

Post a Comment