Tuesday, August 29

Lori laua watu sita, lajeruhi 42 katika ajali mkoani Singida


Singida. Lori aina ya Scania, mali ya Abdallah Mussa (39) ambaye ni mfanyabiashara wa mjini Singida limepinduka na kusababisha abiria sita kufariki dunia na kujeruhi wengine 42.
Lori hilo lililokuwa likiendeshwa na Juma Jumanne (32) lilikuwa likitokea mnadani katika Kijiji cha Mtinko, Singida Vijijini likielekea Singida Mjini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 1.30 usiku katika kijiji hicho.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Haji Jumanne (35), Mikidadi Mohammed (40) wote wakazi wa Kijiji cha Mrama na Musa Salimu (30) mkazi wa Kijiji cha Mwakiti.
Magiligimba aliwataja wengine kuwa ni Allen Mwangu (38) mkazi wa Wilaya ya Ikungi, Lucas Stephano (40) mkazi wa Kijiji cha Mrama na Sharifa Omari (19) mkazi wa Kijiji cha Ilongero.
Kamanda Magiligimba alisema majeruhi 20 wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa Mjini Singida, 10 wamelazwa wamelazwa Hospitali ya Misheni ya Mtinko na wanne ambao hali zao ni mbaya, wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Hydom, Manyara.
“Majeruhi hawa baadhi wamevunjika mikono, wengine miguu na sehemu mbalimbali ya miili yao,” alisema na kuongeza:
“Hawa wenye hali mbaya ni Fadhili Jumanne (33) mkazi wa Kibaoni mjini Singida, Mikidadi Hamisi, Jafari Hamisi na Idrisa Ibrahimu wote wamevunjika miguu. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali Misheni Mtinko,” alisema.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kutokuwa makini akiwa anaendesha lori hilo lililokuwa limesheheni abiria na mizigo.

No comments:

Post a Comment