Dar es Salaam. Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele amehojiwa na Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa siku mbili mfululizo kuanzia juzi kuhusu utoaji kiholela wa vibali vya kuingizia nchini kemikali bashirifu.
Uingizaji na usambazaji wa kemikali bashirifu hufanyika chini ya udhibiti wa hali ya juu wa mamlaka za kitaifa na kimataifa kuzuia uwezekano wa kuchepushiwa katika utengenezaji wa dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine.
Taarifa zinasema Profesa Manyele, ambaye juzi alihojiwa kwa siku nzima, alichukuliwa tena jana mchana kwa mahojiano zaidi yaliyofanyika makao makuu ya DCEA, Upanga jijini Dar es Salaam.
Hadi tunakwenda mitamboni Profesa Manyele alikuwa bado mikononi mwa DCEA, kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi ilizipata, na kuna taarifa zaidi kuwa huenda akaendelea kushikiliwa hadi leo.
Kuhojiwa kwake kwa siku mbili kumetokea sambamba na uamuzi wa Rais Magufuli kumuondoa Mihayo Msikhela kutoka katika nafasi yake ya kamishna wa oparesheni wa DCEA, na kumteua Luteni Kanali Frederick Milanzi kushika wadhifa huo.
Juzi, Rais John Magufuli alifanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam na Kamishna Mkuu wa DCEA, Rodgers Siyanga aliyemhakikishia kuwa mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini yanapata mafanikio makubwa.
Taarifa iliyotolewa juzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa, inasema Siyanga alimueleza Rais mikakati inayotumika kupambana na tatizo la dawa za kulevya. Haikueleza kwa kina masuala mengine ambayo Rais Magufuli alizungumza na Siyanga.
Ingawa mamlaka haziko tayari kuthibitisha, kuhojiwa kwa Profesa Manyele kunahusishwa kwa kiasi kikubwa na wimbi la kukamtwa kwa kemikali bashirifu ambazo uagizaji, uhifadhi na usambazaji wake husimamiwa na ofisi yake.
Katika miezi ya karibuni, DCEA ilikamata mamia ya tani za kemikali bashirifu katika Bandari ya Dar es Salaam, bandari kavu na kwenye maghala ya watu binafsi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka DCEA, waagizaji wengi walikiuka utaratibu na kushindwa kueleza wanakosambaza kemikali hizobaada ya kuingizwa nchini.
Tukio la kwanza la kukamatwa kwa kemikali hizo lilitokea Mei baada ya maofisa wa DCEA kukamata lita zaidi ya 5,000 za aina mbalimbali za kemikali bashirifu, mali ya mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Benedict Assey.
Baada ya kukamatwa kwa shehena hiyo iliyokuwa katika maghala yaliyopo Mwenge (Dar es Salaam), Bagamoyo (Pwani) na Kilimanjaro (Moshi), iligundulika kuwa kibali cha kughushi kilitumika kuagiza mzigo huo, huku kibali cha usajili cha kampuni iliyoagiza mzigo huo ya Techno Net Solution kikionekana kimekwisha muda wake.
Maghala hayo yalionekana kutokidhi viwango vilivyowekwa kisheria, kama umbali kutoka makazi ya watu.
Mathalani, licha ya ghala la Mwenge kuwa katikati ya makazi ya watu, ofisi ya Mkemia Mkuu haikuchukua hatua pamoja na ukweli kuwa ilikuwa ikifanya ukaguzi mara kwa mara.
Mwezi uliofuata mamlaka hiyo ilikamata tena makontena mawili yaliyokuwa na lita zaidi ya 6,000 za kemikali hizo hatari ndani ya bandari kavu iliyopo Tabata Relini, Dar es Salaam. Shehena hiyo iliyoagizwa kutoka Ufaransa na India, ni mali ya Assey.
DCEA inadai kuwa ilimtaka mmiliki huyo atoe nyaraka na orodha ya watu au taasisi zilizouziwa kemikali hizo, lakini alishindwa kufanya hivyo.
Na mwezi uliopita tu, DCEA ilikamata makontena mengine 10 yenye zaidi ya lita 200, 000 za aina tofauti za kemikali bashirifu katika Bandari ya Dar es Salaam zilizoagizwa kinyume cha sheria kutoka Swaziland.
DCEA ilisema imebaini kampuni inayotuhumiwa kwa uingizwaji huo, ilianza kazi hiyo tangu mwaka 2016 na tayari ilishaingiza lita milioni 1.5 za kemikali hizo na kupelekwa kwa kampuni moja iliyoko Mbezi Luis.
Mamlaka ilisema pia kuwa baada ya uchunguzi zaidi, iligundua kuwa kampuni hiyo inajihusisha na kuuza magari na si kutunza wala kuchakata kemikali, jambo lililowastua na kufanya uchunguzi wa kina.
Kamishna wa ukaguzi na sayansi jinai wa DCEA, Bertha Mamuya aliwahi kuiambia Mwananchi kuwa kwa kawaida kemikali hizo hutumika kutengenezea dawa za binadamu, za wadudu na mbolea lakini magenge ya wahalifu huzitumia kutengeneza heroin na cocaine katika maabara za ufichoni.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali za Viwanda na Walaji (Usimamizi na Udhibiti) ya mwaka 2003, Ofisi ya Mkemia Mkuu ndiyo yenye mamlaka ya kutoa vibali vyote vya uingizaji wa kemikali bashirifu, kufanya ukaguzi katika maghala kuona kama yanakidhi viwango na kufuatilia matumizi yake.
Kuna tuhuma kuwa ukwasi wa baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo unatokana na kutoa vibali vya uingizaji wa kemikali kinyume cha sheria.
“Imefika wakati watu wanaagiza kiasi kikubwa cha kemikali bashirifu na shehena inapowasili bandarini ndipo wanaanza ku-process (kutafuta) vibali kwa Mkemia Mkuu,” alisema mtaalamu mmoja wa kemikali DCEA aliyeomba kutotajwa jina.
Mapema mwaka jana, Ofisi ya Mkemia Mkuu iliingia katika kashfa kubwa baada ya kontena za kemikali bashirifu aina ya aceti anhydride zenye thamani ya Sh28 bilioni kukamatwa nchini Pakistani likitokea Tanzania.
Inadaiwa kuwa kontena hilo lilitokea China huku wamiliki wake wakipewa vibali vya kuingiza kemikali hizo baada ya kuzieleza mamlaka kuwa zingezitumika katika kiwanda cha korosho. Hata hivyo, habari zinadai kuwa kontena hilo lilihifadhiwa Kurasini jijini Dar es Salaam kabla ya kupata vibali kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu na kupelekwa Pakistan ambako lilikamatwa.
Maofisa wawili wa ofisi ya mkemia mkuu waliwahi kukamatwa na kuhojiwa kuhusiana na utoaji vibali kwa shehena hiyo, lakini kesi dhidi yao ilishindwa kuendelea katika mazingira yasiyoeleweka.
Machi mwaka huu, maofisa wengine wawili wa ofisi hiyo hiyo walikamatwa na DCEA na kuhojiwa kwa saa kadhaa kwa madai ya kusaidia usafirishwaji wa kontena hilo kwenda Pakistan.
Kutokana na wimbi la ukamataji wa kemikali hizo hatari, Profesa Manyele alijitokeza kwenye vyombo vya habari hivi karibuni akionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara wanaokiuka utaratibu wa uingizaji, usafirishaji na uhifadhi wa kemikali bashirifu.
Alikuwa akifafanua kukamatwa kwa tani zaidi ya 6,000 za kampuni ya Tecno Net Scientific.
Profesa Manyele alifanya tena mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni na kukiri kwamba ofisi yake imelemewa na kiwango kikubwa cha kemikali za matumizi ya nyumbani na viwandani zinazoingizwa nchini kila siku.
Alisema ongezeko hilo linatokana na watu wengi kuagiza mzigo wa kemikali bila kufuata sheria.
Alisema kabla ya kutoa onyo hilo, waingizaji walikuwa wakifanya hivyo kinyume cha sheria na walikuwa wakiagiza kwanza mizigo na inapowasili au kukaribia kuwasili, ndipo wanaanza kuomba kibali au usajili kwa mara ya kwanza.
No comments:
Post a Comment