Friday, August 25

Tanroads yadai kutopata zuio la mahakama, yaendelea kubomoa

Tingatinga la Wakala wa Barabara Tanzania

Tingatinga la Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) likiendelea na kazi ya kubomoa nyumba zinazodaiwa kujengwa katika hifadhi ya Barabara ya Morogoro eneo la Kimara Stop Over jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace 
Dar es Salaam. Wakati Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kikilaani Kitendo cha Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es Salaam (Tanroads) kubomoa nyumba ambazo zina kinga ya mahakama, taasisi hiyo ya Serikali imeendelea na kazi hiyo kwa kuwa haijapewa zuio.
Lakini meneja wa Tanroads wa Dar es Salaam, Julius Ndyamkama amesema hatua hiyo ya kuendelea kubomoa haimaanishi kuwa wameidharau mahakama.
Akizungumza jana na Mwananchi, Ndyamkama alisema wanaiheshimu mahakama na wanaiogopa, lakini kinachowafanya waendelee kubomoa ni kutopewa taarifa ya zuio hilo na mahakama na badala yake habari hizo wanazisikia tu kwenye vyombo vya habari.
“Hivi unategemea mimi nidharau mahakama kweli?” alihoji Ndyamkama.
“Ndiyo nakwambia kweli. Mimi siogopi kweli? Mimi nasikia tu kwenye magazeti kwamba tarehe 18 ndiyo (amri ya zuio) ilitoka. Kwa nini tukaidi agizo la mahakama bwana?
“Jumatatu tulikuwepo ofisini, kwa nini hawakutuletea taarifa au kuja kubandika zuio hilo ofisini kwetu? Hatujaambiwa chochote, hatuwezi kupingana na sheria, kwani sisi tumekuwa nani? Wakituletea taarifa tutatii amri ya mahakama lakini kama hawajaleta tutaendelea.”
Hata hivyo, kazi ya ubomoaji jana iliendea na ilizikumba nyumba za wakazi wawili; Marawa Lyimo na Tedy Marko ambazo ni miongoni mwa majengo yaliyowekewa zuio.
“Niliwaonyesha hati hiyo (ya zuio la mahakama), lakini wakanijibu kuwa ‘sisi hatujui kusoma, tunachojua ni kutekeleza agizo tulilopewa,” alisema Lyimo.
Meya wa jiji la Tanga alia ubomoaji
Sakata la ubomoaji kupisha ujenzi wa reli, pia limeshika kasi mkoani Tanga, ambako Meya wa Jiji, Mhina Mustapha amelaumu wataalamu kuingia eneo lake na kufanya kazi bila kuitaarifu halmashauri hiyo.
Mhina alisema hayo jana jioni alipokutana na wamiliki wa nyumba zilizowekewa alama ya “X”.
“Sisi kama wawakilishi wenu tumefadhaishwa sana na kitendo cha wataalamu wa Rahco kutoka Dar es Salaam na kuja hapa kufanya shughuli za kuweka alama ya “X” kwenye nyumba bila kututaarifu,” alisema Mustapha.
Alisema katika kuonyesha kuwa halmashauri haiungi mkono kazi hiyo, itawasiliana na uongozi wa ngazi za juu serikalini kuona jinsi ya kuwasaidia wakazi.
Wakati Meya akizungumza hayo, wamiliki wa nyumba hizo wamejigawa katika makundi mawili ambayo yatafanya kazi ya kufuatilia haki za wamiliki wa hoteli na wenye nyumba za makazi.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela aliwaomba waandishi wa habari kuwa na subira na kuahidi kulitolea maelezo suala hilo mara baada ya kujiridhisha kuhusu hatua zilizochukuliwa na Rahco kuweka alama hizo.
“Kimsingi kuna dosari ambazo tumeziona katika zoezi zima la uwekaji wa alama za ‘X’ kwenye majengo ya Tanga. Inaonyesha kuna kuchanganya kati ya nyumba za mijini na za vijijini. Haiwezekani ziwekwe alama sawa kwani kwa vyoyote kama itafanyika hivyo basi Tanga itabakiwa na nyumba chache mno,” alisema Shigela.    

No comments:

Post a Comment