Thursday, August 31

Masharti mikopo elimu ya juu inavyosumbua wanafunzi

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakifanyiwa
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakifanyiwa uhakiki na Bodi ya Mikopo nchini wakati wa zoezi la uhakiki wa wanafunzi kwenye taasisi za elimu ya juu nchini ili kubaini kama kuna uwepo wa wanafunzi wasiostahili kupata mikopo. Picha na Maktaba 


Dar es Salaam. Wanafunzi wanaotaka mikopo kwa ajili ya kuwezeshwa kupata elimu ya juu wanalazimika kuzunguka ofisi za serikali za mitaa, wanasheria, Wakala wa Vizazi na Vifo (Rita), wafadhili na sehemu nyingine kabla ya kukamilisha maombi yao.
Juu ya safari hizo, wanatakiwa kuwa na fedha za kutosha kugharimia huduma hizo muhimu kukamilisha maombi yao, lakini hawatakuwa na uhakika wa kupata mikopo hiyo.
Safari na fedha hizo zimegeuka kuwa mzigo mkubwa kwa waombaji kiasi cha kusababisha wengi kushindwa kutimiza masharti na hivyo maombi yao kukosa sifa.
Na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ililazimika kutoa ufafanuzi jana kueleza hali halisi ya waombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2017-18, ikieleza kuwa imelazimika kuongeza muda kutoa nafasi kwa waombaji kutimiza masharti hayo.
“Inavyoonekana waombaji wengi wameshindwa kuwa watulivu wakati wanaposoma masharti haya maana unakuta baadhi ya fomu zao zina mapungufu mengi, kama kutosainiwa na wahusika waliotajwa,” alisema mkurugenzi mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alipozungumza na waandishi wa habari jana.
Alisema juzi bodi hiyo ilikuwa imepokea maombi ya wanafunzi 49,282, lakini ni 15,473 tu ndiyo walikuwa wamekamilisha maombi yao kwa njia ya mtandao wakiwa wamefuata taratibu zote za uombaji kama zilizotolewa hivi karibuni na bodi hiyo. Wengine 33,809 walikuwa katika hatua mbalimbali kukamilisha maombi yao.
Badru alisema baadhi ya kasoro walizobaini ni fomu za waombaji wengi kutosainiwa na kamishna wa viapo au mwanasheria.
“Ili fomu ya mwombaji itambulike kuwa imekamilika, inapaswa kupitia hatua hiyo, lakini jambo la kushangaza wengi wameshindwa kutekeleza kigezo hicho,” alisema.
“Kwenye vigezo vya vyeti pia tulitaka kama mwombaji ni yatima basi aambatanishe cheti au vyeti vilivyothibitishwa na Rita, na ikiwa alifadhiliwa basi aambatanishe nakala ya barua kutoka kwa taasisi iliyomfadhili masomo.”
Alisema kutokana na kujitokeza kwa kasoro hizo, bodi hiyo imesogeza mbele muda wa kuwasilisha maombi yao ambao sasa utakuwa Septemba 11 badala ya tarehe ya awali ya Septemba 4.
“Kwa waombaji ambao hawajakamilisha maombi yao tunawakumbusha watumie muda uliosalia kufanya hivyo na wakizingatia kutimiza vigezo vyote. Tunawaomba wasome kwa makini vigezo vilivyowekwa ili wakamilishe kwa wakati maombi yao ya mkopo,” alisema.
Hivi karibuni bodi hiyo ilitangaza vigezo vipya vinavyopaswa kuzingatiwa na waombaji huku akisema kuwa waombaji ambao wazazi wao au walezi wameshika nyadhifa fulani serikalini hawaruhusiwi kuomba.
Awali vyeti vya kitaaluma vilikuwa vinathibitishwa na mamlaka inayotoa, lakini HESLB sasa inataka vithibitishwe na kamishna wa viapo au mwanasheria, ambao kwa kawaida hutoza kiasi cha fedha kwa ajili ya huduma hiyo.
Kigezo kingine ambacho kimeonekana kuwavuruga wanafunzi wengi ni ulazima wa mwombaji kuwa na nakala ya cheti cha kuzaliwa ambacho kimethibitishwa na Rita.
Licha ya Rita kuwataka waombaji hao kuwasilisha vyeti vyao katika ofisi zake zilizopo katika kila wilaya, baadhi ya waombaji wanadaiwa kushindwa kuzingatia hilo na hivyo kujikuta fomu zao zikiwa na kasoro wakati wa uwasilishaji.
Wasiwasi wa waombaji
Mlolongo huo wa masharti na gharama zake umewafanya baadhi ya wahitimu wa elimu ya juu ya sekondari kuhofia kutuma maombi.
“Kwanza kuna mlolongo mwingi, yaani niende intaneti huko nitatumia fedha, kisha niende Rita tena nitatumia fedha badala hapo kuna kwenda kwa hakimu au mwanasheria na maeneo mengine mengi,” alisema muhitimu aliyejitambulisha kwa jina la Brenda Frank.
“Kote kunahitaji fedha. Hapo pia bado sijatoa ada ya Sh30,000. Yaani mpaka tunajaza fomu hiyo nimetumia fedha nyingi na huenda mwisho wa siku na mkopo wenyewe nisipate kabisa.”
Mwanafunzi mwingine, Mustapha Ismail Faki alisema anafikiria suala la kuomba mkopo.
“Bado naendelea kufikiria kama nikajaze fomu au la kwa vile cheti changu cha kidato cha nne ni cha Kenya hivyo kadri ninavyosikia kutoka kwa marafiki zangu, napata wasiwasi kama kweli nitakubaliwa mkopo,” alisema Faki.
Katika ofisi za makao makuu ya Rita kulikuwa na wanafunzi wengi wakipanda na kushuka ghorofa moja baada ya jingine kupata huduma, huku wafanyakazi wakishirikiana na walinzi kutoa maelekezo.
“Waliniambia siku tatu, nikaamua nikae hadi nne, nashangaa leo wamesema bado, ” alisema muombaji aliyejitambulisha kwa jina la Jane Joshua.
Mwingine Skolastika Malesi alisema alituma maombi yake mtandaoni siku saba zilizopita lakini hadi jana hakuwa amepata majibu.

No comments:

Post a Comment