Thursday, August 31

Watoto waliotekwa waeleza yaliyowakuta kwa watekaji


Arusha. Wakati hofu ya matukio ya utekaji watoto ikianza kutanda mkoani Arusha, watoto wawili walioetekwa na baadaye kupatikana wamezungumzia yaliyowakuta wakati wakiwa kwenye makazi ya watekaji.
Wakati watoto hao wakirejea, wengine wawili; Moureen David, mwenye umri wa miaka sita na anayesoma darasa la kwanza Shule ya Msingi Lucky Vincent, na Ikram Salim (3) wote wakazi wa Kata ya Olasiti hawajapatikana.
Watoto waliopatikana, Bakari Seleman (3) na Ayoub Fred (3), walisema wakati wakiwa nyumbani kwao eneo la Olasiti walichukuliwa na mtu na kuwapeleka mbali, kisha aliwapa wali na soda.
“Alituchukua kaka akatupeleka mbali na alitupa wali na soda,” Bakari alisema huku akizungumza kwa taabu.
Bakari, hata hivyo alisema hakumbuki sehemu waliyopelekwa, lakini ni mbali na nyumbani.
Akizungumzia tukio hilo, Aisha Shaaban, ambaye ni mama yake Bakari, alisema watoto wao ambao wanakaa jirani, walichukuliwa Agosti 28 saa 6:00 mchana na watu wasiojulikana.
Alisema walichukuliwa wakiwa wanacheza nje ya nyumba na walibaini wamechukuliwa jioni baada ya kupata ujumbe kutoka kwa watu wasiojulikana kuwa watoto wao wapo salama na kama wanataka kila mmoja alipiwe Sh4.5 milioni.
“Walimpa mtoto karatasi atuletee ndipo tukasoma na kuona ujumbe huo, ambao ulituonya tusitoe taarifa polisi na kama tungefanya hivyo tungechinjwa,” alisema.
Alisema baada ya ujumbe huo, walikwenda kutoa taarifa kwa balozi wa eneo hilo ambaye aliwapigia simu watekaji hao na wakamsisitizia kuwa wanataka fedha.
“Hiyo fedha ilikuwa nyingi, sisi hatuna uwezo ndio tukaondoka na kumuacha balozi akiendelea kuwaomba na baada ya kuwaeleza sisi hatuna fedha walitaka tutoe laki moja,” alisema.
Alisema kutokana na kukosa fedha, walirejea nyumbani na kwenda kutoa taarifa polisi lakini balozi wao aliendelea kuongea na watekaji na ndipo majira ya saa 1:00 usiku walirejeshwa.
“Hawa watoto waliletwa na dereva wa bodaboda ambaye anajulikana kwa jina la Nemesi na ndipo alikamatwa,” alisema.
Alisema baada ya kumuhoji dereva huyo, alisema amepewa watoto hao barabarani awapeleke kwa Kimaro na hawajui watu waliomtuma.
Naye Agness Hussein, ambaye ni mama wa Ayoub, alisema baada ya kuwapata watoto wao walikwenda polisi na jana wamefanyiwa vipimo vyote na kukuta hawajaathiriwa na jambo lolote.
“Tunashukuru Mungu watoto wetu wamerudi salama, tunaomba hawa watekaji wawarudishe na watoto wengine,” alisema.
Akizungumzia utekaji mwingine, David Njau alisema mtoto wake anayeitwa Moureen alitekwa saa 11:00 jioni Agosti 21, akiwa anacheza na wenzake nje ya nyumba kijana mmoja, alimuita kwa jina na kumchukua.
“Tangu Agosti 21 hadi leo hatujui mtoto kama yupo salama kwa kuwa walitaka tuwape Sh4.5 milioni ili wamrejeshe. Nilipowaambia sina walitaka Sh2 milioni,” alisema.
Alisema juzi alipokea nguo za mtoto wake alizokuwa amevaa pamoja na ujumbe ulioandikwa kwenye kalenda ya zamani, kuwa kama wanamtaka mtoto, watume fedha hizo.
Alisema watekaji hao walimtumia ujumbe ulioandikwa kwenye katarasi unaosema: “Mourine kesho ndio mwisho wake kwa sababu hamjatupatia kitu tunachokitaka. Hatukutaka kumdhuru huyu mtoto, lakini mmeyataka.”
Ujumbe mwingine, unasema: “Kama mkishirikisha polisi na majirani, mtakuta kichwa cha mtoto kwenye Rambo.”
Kuhusua kutekwa mtoto mwingine, Kassim Salum alisema mtoto wake, Ikram alitekwa Agosti 26 na watu wasiojulikana ambao walitaka Sh4.5 milioni.
Kama ilivyokuwa kwa Moureen, watekaji walishusha kiwango cha fedha hadi Sh2 milioni, lakini walitumiwa Sh300,000 waliyotaka. Hata hivyo, hawajamrejesha.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkerian, Daudi Safari alisema matukio hayo yanatisha na tayari wameanza kuchukuwa tahadhari.
Naye kamanda wa polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema tayari watu watatu wamekamatwa katika tukio hilo na uchunguzi unaendelea.
“Tumekamata watu watatu ambao ni vijana. Hatuwezi kuwataja kwa kuwa uchunguzi unaendelea, lakini pia tunatoa wito kwa wananchi kutupa taarifa wanapoona watu wasiowafahamu katika maeneo yao,” alisema.
Alisema kutokana na matukio hayo wazazi na watoto wanapaswa kuchukua tahadhari ili kuepuka matukio ya kutekwa watoto.

No comments:

Post a Comment