Dar es Salaam.Bunge la Seneti la Marekani limemuidhinisha Balozi Mark Green kuwa Kiongozi Mkuu mpya wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Akiwa Kiongozi Mkuu wa USAID, Balozi Green atasimamia taasisi kubwa za Serikali ya Marekani inayojihusisha na misaada ya maendeleo, inayoendesha shughuli zake katika zaidi ya nchi 100 kwa lengo la kukabiliana na umasikini uliokithiri na kuzisaidia jamii imara na za kidemokrasia kupata maendeleo kwa kadri ya upeo wa uwezo wao.
Balozi Green anaingia katika wadhifa huu akiwa na hazina kubwa ya uzoefu kutokana na kuwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania.
Pia aliwahi kuwa Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Chama cha Republican (International Republican Institute) ambayo imekuwa ikitekeleza programu kadhaa za USAID nchini Tanzania na katika nchi mbalimbali duniani.
Katika kipindi chake akiwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania kuanzia mwaka 2007 hadi 2009, Balozi Green aliwezesha kuwepo kwa ushirikiano rasmi baina ya nchi hizi mbili katika baadhi ya programu kubwa zaidi za maendeleo zilizowahi kufadhiliwa na Marekani.
No comments:
Post a Comment