Monday, August 14

Lukuvi: Teknolojia changamoto upimaji wa ardhi


Morogoro.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameitaja teknolojia kuwa changamoto kubwa katika mpango wa matumizi bora ya ardhi, hivyo kutoharakisha upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi nchini.
Lukuvi ameyasema hayo leo Jumatatu mjini Morogoro alipokuwa akipokea rasimu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto za matumizi bora ya ardhi nchini, iliyoainisha mapendekezo katika uandaaji, utekelezaji na usimamizi.
“Tunaweza kufikiri fedha si tatizo lakini teknolojia ni tatizo kubwa, kuna haya kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na tushirikiane kuangalia ni teknolojia gani rahisi kupungua gharama za upimaji na upangaji wa ardhi vijijini badala ya kusubiri ndege za anga, hatuwezi ni gharama kubwa,” alisema Lukuvi.
Lukuvi aliyashauri mashirika hayo yanayounga mkono mpango huo kuangalia ni vifaa na nyenzo gani zinaweza kutumia ili kutekeleza mpango huo.
“Tunahitaji teknolojia rahisi ambayo hata ninyi mkiondoka Serikali inaweza kuhimili, hatupendi mtuambukize teknolojia ambayo itakuwa ni ngumu kwetu, kwa kuwa serikali inapopanga gharama kubwa zinajitokeza kwenye picha za anga na zile za chini,” alisema Lukuvi.
Alisema Serikali inapenda kuwa na uratibu wa haraka, ulio rahisi ambao wananchi wanaweza kupanga maeneo yao na kuongeza, lakini pia kuondokana na migogoro.
Mratibu wa Miradi ya Ardhi kutoka Oxfam, Naomi Shadrack alisema kupitia rasimu hiyo wadau wamefanya kazi kwa pamoja kuhakikisha sekta ya ardhi ambayo inatambuliwa na wengi wakiwemo  wakulima na wafugaji wadogo wadogo inafanyiwa kazi.
“Tungependa wadau mbalimbali washirikiane kuhakikisha  ardhi inapangwa na kila mtu anakuwa na uhakika wa ardhi, kupitia mpango mkakati huu tungependa  kujua Serikali imejidhatiti vipi katika bajeti, kuona ni jinsi gani inapanga kwa dhati pamoja na kukabili migogoro na changamoto mbalimbali,” alisema Naomi.

No comments:

Post a Comment