Taarifa iliyotolewa na chama hicho inasema baada ya uchunguzi hupo, kitachukua hatua kulingana na kile kitakachobainika.
Waandishi hao wa TBC alizongwa na kufanyiwa vurugu wakati alipokwenda katuika mkutano na waandishi wa habari uliomhusisha mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, Alhamisi iliyopita.
Tundu Lissu aliitisha mkutano wa waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, saa chache baada ya kuachiwa kwa dhamana na mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu, ambako anakabiliwa na kesi ya uchochezi.
Katika mkutano huo, waandishi wa TBC1 walizuiliwa kuchukua habari na baadhi ya wafuasi waliokuwa kwenye mkutano huo, tukio lililokemewa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) jana.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, amesema katika taarifa aliyoitoa leo Jumamosi kuwa baada ya uchunguzi huo kukamilika watatoa taarifa kamili.
Amesema uchunguzi utaeleza watakachokuwa wamebaini na taarifa watakayoitoa itaeleza hatua watakazochukua.
“Tunapenda kuweka wazi Kuwa tukio hili halikufanywa kwa maelekezo ya kiongozi yeyote na kama Chama hatujawahi na hatuna Sera wala msimamo wa kubagua chombo chochote cha habari,” amesema Mrema katika taarifa hiyo.
Kuhusu muda wa uchunguzi, amesema itategemea na ushirikiano watakaoupata kutoka kwa wahusika lakini lengo lao ni kutochukua muda mrefu.
Amesema chama hicho hakijawahi na hakina sera wala msimamo wa kubagua chombo chochote cha habari.
Taarifa hiyo imewahakikishia waandishi wote wa habari kuwa salama katika matukio yote ambayo yatakuwa yakifanywa na Chadema na watapatiwa ushirikiano unaostahili.
"Imani yetu hiyo tumekuwa tukiidhihirisha kwa vitendo hadharani, mfano, Chadema ni taasisi ya kwanza ya kisiasa iliyotia saini na kukubaliana na 'Azimio la Dar es Salaam Juu ya Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji',” amesema Mrema.
No comments:
Post a Comment