Visiwa vya Zanzibar na Mauritius vina fursa ya kubadilishana uzoefu katika miradi ya Maendeleo ili kujiongezea ujuzi na maarifa yanatayowawezesha Wananchi wake kuimarika zaidi kiuchumi hali itakayosababisha Mataifa yao kuongeza mapato.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Kimataifa ya Ushauri kutoka Kisiwa cha Mauritius { Moneo Consulting } Bwana Devanand Virahsawmy akiuongoza ujumbe wa viongozi wa Kampuni hiyo alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Devanand Virahsawmy alisema Sekta ya elimu ambayo ndiyo mama katika Taifa lolote Duniani inaweza kuwa mwanzo wa ushirikiano huo unaoweza kutoa nafasi kwa vijana wa pande hizo mbili kujipatia Elimu ya Msingi, Sekondari hadi vyuo Vikuu .
Alisema mpango huo wa pamoja kupitia Kaisheni ya pamoja kwa Nchi zilizozunguukwa na Bahari ya Hindi utaongeza chachu ya uchumi kwa Vijana waliobobea Kitaaluma sambamba na ongezeko la ajira.
Bwana Devanand alisema Visiwa vya Mauritius tayari vimeshapiga hatua kubwa ya maendeleo hasa katika Sekta ya Utalii kiwango ambacho wanaweza kusaidia Taaluma kwa Nchi zilizo jirani na Visiwa hivyo.
Mwenyekiti huyo wa Kampuni ya Moneo Consulting alimueleza Balozi Seif pamoja na Mawaziri, Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa SMZ Kwamba Uongozi wa Kampuni yake upo Zanzibar kuitika wito Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuangalia fursa za Uwekezaji.
Alieleza kwamba Kampuni hiyo tayari imeshijengea uwezo wa kuendesha miradi mbali mbali ya Kiuchumi na Maendeleo akiitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na Miradi ya Umeme, Bara bara, Utalii, Benki ya Ufukweni { Off show Bank } Viwanda vya vidogo vidogo pamoja na Uvuvi wa Bahari Kuu.
Akitoa ufafanuzi wa mipango ya Uwekezaji Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} Nd. Salum Nassor Khamis alisema Zanzibar imeanza kufanya mabadiliko ya uchumi wake katika Miaka ya 90 ili kutoka nafasi kwa Taasisi yenye uwezo wa uwekezaji kushiriki kwenye mabadiliko hayo.
Ndugu Salum alisema ushirikishwaji wa Sekta binafsi katika kuchangia uchumi wa Taifa umezingatiwa ili kujenga jamii itakayokwenda sambamba na mabadiliko ya Kiuchumi Duniani.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe huo wa Kampuni ya Ushauri ya Moneo kwamba Zanzibar ina mtazamo wa kuwekeza katika sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu.
Alisema Rasilmali ya Bahari ni eneo linaloweza kujenga uchumi imara utakaoweza kuongeza mapato ya Taifa sambamba na kupunguza ufinyu wa ajira uliowakumba Vijana wengi wanaomaliza masomo yao Nchini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/7/2017.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Kimataifa ya Ushauri kutoka Mauritius (Moneo Consulting) Bw. Devanand Virahsawmy Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif na Baadhi ya Mawaziri wa SMZ, Makatibu Wakuu na Watendahi Wakuu wa SMZ akizungumza na Ujumbe wa Kampuni ya Moneo Consulting kutoka Mauritius.
No comments:
Post a Comment