Monday, July 24

Neno La Leo: Tumbili Hata Akizeeka Haachi Hulka Yake!


Image may contain: 1 person, standing, tree and outdoor
Ndugu zangu,

Katika ulimwengu huu kuna tabia na hulka. Hivi viwili vina tofauti. Kuna sifa na uwezo, navyo ni viwili tofauti.

Tabia ya mwanadamu yaweza kubadilika, lakini si hulka yake. Na mwanadamu anaweza kuwa na sifa za kufanya jambo lakini akakosa uwezo, na kinyume chake. 

Na kibaya zaidi ni pale majungu na fitna yanapogubika sifa na uwezo wa mtu. Kwamba badala ya mwanadamu kupimwa kwa sifa na uwezo wake, majungu na fitna dhidi ya mwanadamu huyo yanawekwa mbele, na hivyo kufanywa kuwa kipimo.

Ndio, kuna wanadamu wenye kuishi kwa kupika majungu na fitna dhidi ya wanadamu wenzao. Tofauti na tabia, hizo ni hulka za wanadamu hao, haziwezi kubadilika.

Mwone tumbili alivyo, tumbili hata akizeeka, haachi hulka yake. Kupalamia miti ni hulka ya tumbili. Hivyo, tumbili hata akizeeka, hafikiri hata siku moja kukaa chini ya mti na kupumzika. Atahakikisha anapalamia hata mti mfupi wa mpapai, alimradi tu akae juu ya mpapai. Hapo atajiona ametimiza utumbili wake. 

Nini adili ya jambo hili?

Tumbili limekuwa neno maarufu sasa. David Kafulila alipata kuitwa tumbili Bungeni. Kumbe, Kafulila hakuwa tumbili, waliomwita Kafulila tumbili ndio tumbili wenyewe.

Bahati mbaya, nchi yetu ina tumbili wengi na wamepewa nafasi za uongozi na maamuzi. Ni jambo jema kwa Rais wa Jamhuri kalitambua hilo. Kazi yetu ni kumsaidia Rais na watendaji wake wasio tumbili, kuwaonyesha waliko tumbili kwenye nafasi za kuwatumikia Wananchi na kwa maendeleo ya nchi.

Ni Neno La Leo.
Maggid.
Iringa.

No comments:

Post a Comment