Tuesday, December 25

"MZIKI WA BONGO FLEVA NI WA KIJINGA"....TID


Inaonekana bado mambo hayamwendei poa Top In Dar licha ya kuwa na hit ya ‘Kiuno’ hewani ambayo imeendelea kufanya poa.Hiyo ni baada ya nyota huyo ambaye jina lake halisi ni Khalid, kuamua kutumia Facebook kutoa maoni yake jinsi muziki huo unavyoenda.
“This Bongo Fleva Music is so stupid yaani kiasi kwamba we don’t even sell it only adios get sponsorship to play it lakini sisi tuko majalala,” aliandika TID.
Ujumbe huo ulivuta hisia za Chidi Benz ambaye aliamua kuchangia kwa kuandika: "Uoga. Unazaa vijana wanataka ustaa so wanakubali chochote. Wakongwe wanataka maisha so wanahitaji kuongezwa chochote. Vitu vinagongana vitu havieleweki."
Chidi aliongeza,”Watangazaji na wadau wamekua mameneja. Haikatazwi. Ila kama wewe si line yake atakupa vipi na asimpe msanii wake. We utapita vipi? Ujinga unajizaa kwa style ya mapacha."
TID naye aliongeza, “now watangazaji sasa hivi wanatutukana and they can do anything to anyone wanaweza wakasema TiD amecopy wimbo bila ya research yoyote yaani anaweza kufanya kila kitu hana limit.”

Mume wa ofisa wa Takukuru ampa jukumu Dk Hoseah

MUME wa aliyekuwa Ofisa Uchunguzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), marehemu Bhoke Ryoba ambaye aliuawa juzi kwa kupigwa risasi amesema kifo cha mkewe kimegubikwa na utata mwingi.
Akizungumza na jana, mumewe huyo, Charles Gibore, pamoja na mambo mengine alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo kubaini ukweli.
“Mke wangu aliuawa na mfanyakazi mwenzake na tukio hilo limegubikwa na utata ambao Takukuru na Polisi ndiyo pekee wanaoweza kutupa ukweli,” alisema Gibore nje ya chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
Gibore alieleza kuwa mkewe huyo aliuawa usiku wa kuamkia Jumapili katika tafrija ya kuagana na kupongezana na baadhi ya wafanyakazi wenzake wa Takukuru waliokuwa wamepandishwa vyeo, tafrija ambayo Bhoke alipewa zabuni ya kupika chakula.
Alisema pia mkewe aliombwa pia awapatie wenye sherehe hiyo, vijana wawili wa kuwachomea nyama... “Vijana hao walikwenda asubuhi ukumbini ili kuandaa eneo la kuchomea nyama, huku Bhoke akiwa bado nyumbani akiandaa chakula,” alisema Gibore na kuongeza:
“Wale vijana walinieleza kwamba baadaye saa 8:30 mchana, Bhoke na wenzake walifika ukumbini na kuwakuta vijana wawili wanaofanya nao kazi wakinywa pombe, huku wakichezea silaha aina ya bastola kujaribu shabaha.”
“Vijana hao walifyatua risasi juu na ndipo muuaji alipompiga kichwani marehemu katika jicho na mauti yalimfika muda mfupi,” alisema.
Alisema baada ya hapo muuaji huyo alitoweka kisha kujisalimisha mwenyewe katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Temeke, Chang’ombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo alithibitisha mtuhumiwa huyo kujisalimisha na kisha kushikiliwa kituoni hapo na kueleza kuwa amekuwapo hapo Jumamosi iliyopita.Kamanda Kiondo alisema pamoja na mtuhumiwa huyo kujitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Takukuru, polisi wanaendelea kuchunguza ili kubaini ukweli wa taarifa hizo.
“Tunaendelea kumshikilia hapa na uchunguzi utakapokamilika tutamfikisha mahakamani kwa taratibu nyingine za kisheria,” alisema Kiondo.
Marehemu Bhoke Ryoba alizaliwa Juni 18, 1978 katika Kijiji cha Kiterere, Wilaya ya Tarime mkoani Mara na anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwao.
Ameacha watoto watatu; Doloresy (10), Dolrisy (4) na Dolrick Gibore ambaye ana mwaka mmoja.

Mwekezaji atiwa mbaroni kwa ujangili

MENEJA wa Hoteli ya Kitalii ya Tree Top, iliyoko katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, wilayani Monduli ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kukutwa na ngozi za chui nyumbani kwake, akiwa katika harakati za kuisafirisha kinyemela kwenda nje ya nchi.
Habari zilizothibitishwa na Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete, zilisema mtuhumiwa huyo anayeaminika kuwa ni raia wa Afrika Kusini alikotarajia kupeleka ngozi hiyo, alikamatwa saa 11 jioni ya Desemba 21, mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari hizo, kabla ya kutiwa mbaroni, Kikosikazi kinachoundwa na askari kutoka Tanapa, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA), kilifanya upekuzi nyumbani kwa meneja huyo baada ya kupokea taarifa za siri kuwa anajihusisha na ujangili na kuuza isivyo halali, nyara za Serikali.
“Ni kweli mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kikosikazi chetu kupata taarifa kuwa anamiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria na kweli baada ya upekuzi alikutwa na ngozi ya chui,” alisema Shelutete kwa njia ya simu jana.
Alisema suala hilo tayari limefikishwa polisi katika Kituo cha Mto wa Mbu, wilayani Monduli kwa ajili ya uchunguzi na hatua zaidi za kisheria kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani.
Habari zaidi zilidai kuwa mtuhumiwa aliyepelekwa katika Kituo cha Polisi cha Karatu ambako ndiko yalipo makao makuu ya Kikosikazi cha kupambana na ujangili katika Hifadhi za NCAA, Manyara na Tarangire.
Inasemekana hata hivyo aliachiwa kwa dhamana baada ya kudhaminiwa na mfanyakazi mmoja wa Hoteli za Sopa Lodges inayomiliki msururu wa hoteli kwenye mbuga za wanyama katika Mikoa ya Arusha na Mara.
Katika nyumba ilimokutwa nyara hizo za Serikali, inasemekana nyara zilikutwa zikiwa zimefungwa kwenye mfuko maalum tayari kusafirishwa huku jina na anwani ya mpokeaji ikiwa pia imeandikwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas aliyezungumza kwa njia ya simu akiwa njiani akitokea Moshi kwenda Arusha, aliahidi kulifualia suala hilo na kulitoa ufafanuzi suala hilo baada ya kufika ofisini.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la matukio yanayohusishwa na vitendo vya ujangili hatua ambayo inahatarisha usalama wa baadhi ya nyara za Serikali. Wiki iliyopita Serikali ilitangaza kutia mbaroni mtandao wa ujangali uliokuwa ukijihusisha na biashara haramu ikiwemo wa pembe za ndovu

JWTZ: Tunamsaka askari aliyepiga picha na Lema

WAKATI Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), likihaha kumtafuta aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akiwa amevaa sare za jeshi hilo, mtu huyo ameibuka na kusema yuko tayari kufukuzwa kazi kuliko kuacha kuishabikia Chadema.
Kauli hiyo ya JWTZ imekuja baada ya jana, gazeti la mwananchi kuchapisha picha ya mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa JWTZ akiwa amepiga picha na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, huku akiwa amenyoosha vidole viwili alama inayotumiwa na Chadema.
Baada ya taarifa hiyo, JWTZ lilitoa taarifa likieleza kushtushwa na tukio hilo na kusema kwamba linamtafuta mtu huyo kwa udi na uvumba ili kujiridhisha kama kweli ni askari wake.
‘‘Kimsingi Jeshi linafanya uchunguzi wa kumtambua mtu huyo kama kweli ni askari,’’ ilisema sehemu ya taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya jeshi hilo ambayo iliyatilia shaka mavazi aliyokuwa amevaa mtu huyo kama ndiyo yanayotumiwa na jeshi hilo sasa.
Taarifa hiyo ya JWTZ, ilisema ingekuwa rahisi kumtambua mtu huyo kwa kuangalia paji la uso lakini alilifunika ili asitambulike.
‘‘Pamoja na hayo, jeshi linamtafuta ili kumchukulia hatua za kinidhamu kutokana Kanuni za Majeshi ya Ulinzi likisema Sheria namba Nne ya Mabadiliko ya Nane katika Katiba ya Nchi ya mwaka 1992, Ibara ya 147(3), mwanajeshi yeyote hatakiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa,’’ ilisema taarifa hiyo.
Mbali ya taarifa hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema endapo itabainika kuwa aliyevaa sare hizo ni mwanajeshi, moja ya hatua dhidi yake ni kufukuzwa kazi mara moja.
Mbali na hatua hiyo, Kanali Mgawe alisema kuanzia sasa, Jeshi limepiga marufuku mtu yeyote kuvaa sare zake katika mikutano yote ya siasa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Kuhusu kitendo cha askari huyo kupiga picha na Lema, Kanali Mgawe alisema moja ya masharti muhimu ya askari anapiojiunga na jeshi ni kutambua na kutii sheria inayomzuia kujihusisha na masuala ya siasa na kwamba kitendo cha mtu huyo kimemshangaza na kumfanya amtilie shaka kama kweli ni askari aliyekamilika.
Msimamo wa mtuhumiwa
Kwa upande wake, mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa Kikosi cha Chuo cha Mafunzo Monduli (TMA), mkoani Arusha, alisema ni bora afukuzwe kazi kuliko kunyimwa kujiunga na Chadema.
Akizungumza jana kwa sharti la kutotajwa jina akiwa Mirerani, Simanjiro mtu huyo alisema Chadema ni chama makini chenye uwezo wa kuongoza nchi kwani kinatetea wanyonge na kujali masilahi ya jamii.
Alisema kwa kuwa Katiba ya nchi hairuhusu wanajeshi kujihusisha na vyama vya siasa, yuko tayari kufukuzwa kazi ili aendelee kukishabikia chama hicho.
Alisema ruhusa ya kikatiba kwa wanajeshi ya kupiga kura kuchagua madiwani, wabunge na Rais haitoshi na kwamba ameamua kujiunga kabisa na chama. Askari huyo alipiga picha na Lema baada ya mbunge huyo kuhutubia mkutano uliofanyika huko Mirerani. Katika mkutano huo wa hadhara, Lema alisema: “Ninapoongoza maandamano ya makamanda ninakuwa natetea masilahi yenu mkiwamo polisi ambao mnanipiga mabomu.
Sisi hatuangalii wake zetu wamevaa hereni za dhahabu ila tunaandamana kudai haki, mishahara mizuri kwa madaktari, walimu, askari na maisha bora kwa Watanzania.”
Raymond Kaminyoge, Patricia Kimelemeta, Dar na Joseph Lyimo, Simanjiro.

Friday, December 21

Lema ashinda rufaa

Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Godbless Lema amerudishiwa ubunge wake baada ya kushinda katika rufaa ya kesi yake ya kupinga matokeo iliyosomwa jijini Dar es Salaam leo.

Matokeo Darasa la Saba hadharani

Beatrice Moses na Ibrahim Yamola
SERIKALI imetangaza matokeo ya darasa la saba mwaka huu, huku takwimu za matokeo hayo zikionyesha kuwa zaidi ya nusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 ni wale waliopata asilimia 40 ya alama kwenda chini katika matokeo hayo.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa wananfunzi 294,833 sawa na asilimia asilimia 52.58 waliopata daraja ‘D’ wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Hao wanaungana na wenzao 265,873 waliopata madaraja ya A,B na C ambao ni sawa na asilimia 47.41. Kwa mujibu wa taratibu za mitihani ya darasa la saba, jumla ya alama zote ni 250 ambazo zimegawanywa katika madaraja matano ambayo ni A mpaka E.
Mchanganuo wa madaraja hayo ni alama 201 hadi 250 kwa daraja la A, alama 151 – 200 kwa daraja B, alama 101 hadi 150 kwa daraja C, alama 51 – 100 kwa daraja D na alama 0 – 50 kwa daraja E.
Waziri Kawambwa alisema wanafunzi 560,706 walichaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari kati ya 865,534 waliofanya mtihani huo wa siku mbili; Septemba 19 na 20 mwaka huu na kwamba mwaka huu wasichana wamefanya vizuri katika mtihani huo kuliko wavulana.
“Wasichana waliofaulu ni 281,460 sawa na asilimia 50.20 ya wanafunzi 560,706 wakati wavulana waliofaulu ni 279,246 sawa na asilimia 49.80,” alisema Kawambwa alipokuwa akitangaza matokeo hayo na kuongeza:
“Matokeo yanaonyesha kuwa jumla ya wahitimu 3,087 walipata daraja A, wakati 40,683 walipata daraja la B. Wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja C wakati 526,397 walipata daraja D. Watahiniwa waliobaki 73,264 walipata E”.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013, imeongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na wanafunzi 515,187 waliochaguliwa mwaka jana.
“Mtihani wa mwaka huu, kwa mara ya kwanza watahiniwa walifanya kwa kutumia teknolojia mpya ya Optical Mark Reader (OMR) na ulisahihishwa kwa kutumia kompyuta,” alisema.
Alisema matokeo haya yanaonyesha alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana.
Kabla ya matokeo, wasichana waliofanya mtihani walikuwa 456,082 sawa na asilimia 52.68 na wavulana ni 409,745 sawa na asilimia 47.32,” alisema Dk Kawambwa.
“Watahiniwa 29,012 sawa na asiliamia 3.24 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, vifo na ugonjwa,” alisema.
Dk Kawambwa alisema, kati yao, ambao hawakufanya mtihani wasichana walikuwa 12,501 sawa na asilimia 2.67 na wavulana ni 16,511 sawa na asilimia 3.87.
Waziri huyo alisema, udanganyifu katika mitihani kwa mwaka huu umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na idadi ya mwaka jana.
“Waliofutiwa matokeo mwaka huu ni watahiniwa 293 ikilinganishwa na watahiniwa 9,736 waliofutiwa matokeo yao kwa udanganyifu mwaka jana,” alisema Dk Kawambwa.
Hata hivyo, itakumbukwa serikali ilionya mwaka jana kuwa mwanafunzi atakayebainika kujiunga na kidato cha kwanza bila kumudu stadi hizo, Mwalimu Mkuu wa shule alikotokea mwanafunzi huyo na Msimamizi wa Mtihani wakumaliza elimu ya msingi watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Katika mkutano huo wa jana na Waandishi wa Habari, Dk Kawambwa hakutaja viwango vya ufaulu kwa kila somo kama ambavyo imezoeleka katika mitihani iliyotangulia wala mkoa uliofanya vizuri au vibaya.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo alipotangaza matokeo ya mwaka jana aliweka wazi viwango vya ufaulu wa masomo ya Kiingereza, Sayansi na Hisabati, ikilinganishwa na mwaka juzi.
Mulugo alisema viwango hivyo vilikuwa vimepanda kwa mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2010 ambavyo ni Kiingereza kutoka asilimia 36.47 hadi asilimia 46.70, Sayansi asilimia 61.33 kutoka asilimia 56.05 na Hesabu asilimia 39.36 kutoka asilimia 24.70.
Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo akizungumzia matokeo hayo jana alisema: “Hili janga, kwa sababu ukifanya uchambuzi wa haraka utabaini kuwa wanafunzi waliopata alama za daraja la A ni asilimia 0.35 tu”.
Lyimo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), alisema upo uwezekano mkubwa kukawa na idadi kubwa ya wanafunzi wasiojiweza waliochaguliwa kwenda Sekondari, hivyo akashauri iandaliwe program maalum ya kuwawezesha wanafunzi hao kumudu masomo ya kidato cha kwanza.
“Kama wanafunzi zaidi ya nusu waliochaguliwa kwenda sekondari ni wale wa daraja la D, hapo kuna kazi kubwa sana, tunaweza kuwa na mbumbubu wengi Sekondari kwahiyo nashauri Serikali iandae walau mpango wa wiki mbili kabla ya shule kufunguliwa ili kuwasaidia hawa watoto,”alisema.
Lyimo alisema ofisi yake itaendelea kufanya utafiti ili kubaini sababu za kufanya vibaya kwa wanafunzi katika mtihani huo na kwamba itatoa taarifa baada ya kupata matokeo ya kitaalamu kuhusu suala hilo.

Thursday, December 20

Kesi ya viongozi wa Uamsho Zanzibar yatupwa

MAHAKAMA Kuu ya Zanzibar ,imetupilia mbali kesi ya viongozi wa Uamsho waliokuwa wanadai kunyimwa huduma muhimu wakiwa mahabusu.
Jaji Mkusa Isaack Sepetu jana aliitupa kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2012 iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim.
Jaji Sepetu alisema kesi hiyo iliyofunguliwa na mawakili Abdallah Juma Mohammed, ilifunguliwa kinyume na kifungu cha 4 sura ya 28 cha Sheria za Mawakili na Wanasheria wa a Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Alisema pamoja na mambo mengine, nyaraka zimekosa, jina la mtu aliyekula kiapo kwa niaba ya washtakiwa nalo halipo.
Alisema kimsingi mambo hayo hayakukidhi hoja za kisheria kwa hivyo anaitupa kesi hiyo iliyofunguliwa na viongozi wa Uamsho. Viongozi wa Uamsho walifungua kesi hiyo wakidai kwamba hawatendewi haki katika Mahabusu ya Kiinua Miguu, iliyopo Zanzibar, kwa kunyimwa haki za kubadilisha nguo, kuabudu, kuonana na jamaa zao na zingine.
Wakili wa washtakiwa hao, Salum Toufioq alisema kwamba wateja wake sasa wanapewa huduma hizo lakini hawajaruhusiwa kuonana na jamaza zao tangu kesi hiyo ilipoanza.
Jaji Mkussa alisema kwa mujibu wa sheria ya vyuo vya mafunzo Zanzibar, washtakiwa wana haki ya kupewa huduma zote sawa na mahabusu wengine.
Kesi ya msingi inayowakabili viongozi hao itaendelea Januari 3, mwakani.
Viongozi hao ni Masheikh Farid Hadi Ahmed, Msellem Ali Msellem, Azzan Khalid Hamdan, Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman na Hassan Bakari Suleiman.

Arfi atupa kadi ya Chadema kikaoni

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezidi kuandamwa na migogoro baada ya jana kuibuka mwingine mkubwa katika kikao chake cha ndani mkoani Katavi kiasi cha kumfanya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Said Arfi, kutupa kadi yake ya uanachama.
Huu ni mgogoro wa pili mkubwa kuripotiwa katika kipindi cha juma moja lililopita baada ya ule wa wilayani Karatu ambako pamoja na mambo mengine uliishia kwa Kamati Kuu kuusimamisha uongozi wote wa chama hicho wilaya.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa Arfi ambaye ni Mbunge wa Mpanda Mjini, alitishia kujitoa Chadema jana, katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya chama hicho Mikoa ya Katavi na Rukwa kilichoketi Namanyere, Nkasi na kufikia uamuzi wa kumsimamisha Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Mkoa wa Rukwa, Laurent Mangweshi.
Katika kikao hicho, Arfi anadaiwa kuichukua kadi yake ya Chadema na kumtupia Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Rukwa, John Mallack akitangaza kuachia nyadhifa zote alizonazo, kisha kuondoka ukumbini, kabla ya kufuatwa na wazee wa chama hicho na kumsihi aichukue kadi yake hiyo.
Alifikia hatua hiyo baada ya kutokea sintofahamu kati ya wajumbe wa kikao hicho katika uamuzi huo uliofikiwa kwa kupiga kura za ndiyo na hapana.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho vilifafanua kuwa Arfi alikerwa na kauli iliyotolewa na Mangweshi kuwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alipokea rushwa kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Vyanzo hivyo vya habari vimeeleza kuwa kutokana na hali hiyo, Arfi alipandwa na hasira na kuamua kumrushia kadi Mallack kisha kutoka nje ya ukumbi.
“Hatua hiyo ilifanya wajumbe wa kikao hicho nao kutoka nje ya ukumbi na kuanza kumbembeleza ili asichukue uamuzi huo na kisha wakamwekea kadi yake ya uanachama katika mfuko wake wa shati,” alisema mmoja wa makada hao.
Arfi mwenyewe hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo baada ya simu ya mkononi kuita muda wote bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe, hakujibu.
Mallack akizungumza na gazeti hili kwa simu alikiri Arfi kurusha kadi mezani kisha kutoka nje ya ukumbi, lakini akasema suala hilo lilishughulikiwa na wazee na kumalizwa.
“Ni kweli unajua huyu ni Makamu Mwenyekiti wetu wa Taifa, sasa inapotokea vijana wadogo wakamtuhumu kwa tuhuma za uongo na ambazo hazipo inatia hasira, ndiyo maana huyo kijana tumemvua uongozi,” alisema Mallack.
Tuhuma za Mangweshi
Mangweshi alisimamishwa uongozi baada ya kutuhumiwa kwa mambo mbalimbali ya kiutendaji ndani ya chama hicho ikiwamo kumkashifu Arfi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mallack alisema kuwa Magweshi amevuliwa uongozi baada ya chama hicho kujiridhisha kuwa alitenda makosa hayo.
Alisema kamati ya ushauri ilimwita ili kujibu tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili ikiwamo kutoa taarifa zisizo rasmi bila kufuata taratibu za chama.
“Pia amepatikana na hatia ya kuandika barua za kashfa na kuzipeleka makao makuu ya chama kumkashifu Arfi pamoja na viongozi wengine wa chama akiwamo Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.
Katibu Mwenezi wa Chadema Mikoa ya Rukwa na Katavi, John Matongo alisema kabla ya kupewa adhabu ya kusimamishwa, amewahi kuonywa mara kadhaa lakini ameshindwa kujirekebisha.
“Hali hiyo ya mwenyekiti ingeachwa iendelee, ingeweza kuleta mgawanyiko na uchonganishi kwa viongozi wa kitaifa,” alisema.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kikao hicho hakikuendeshwa kwa amani baada ya pande mbili zinazovutana kutofautiana waziwazi kuhusu uamuzi wa kumsimamisha mwenyekiti huyo kiasi cha kulazimu hatua hiyo ifikiwe kwa kupiga kura.
Kura hizo zilipigwa na wajumbe 36 na matokeo yakaonyesha kuwa 24 waliafiki uamuzi huo na 12 kuukataa.
Akizungumza na mwandishi wetu, Magweshi alisema “Sina taarifa yoyote juu ya tukio hilo kwani sina barua rasmi.”
Alipoulizwa kama alishiriki kikao hicho, alikubali na kusema kilikuwa kikijadili mambo mbalimbali ya chama hicho.
Tanga nako si shwari
Uongozi wa Chadema mkoani Tanga umeapa kumshughulikia Katibu wa Baraza la Vijana mkoani hapa, (Bavicha), Deogratias Kisandu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Akizungumza na waandishi wa habari, katibu wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Saidi Mbwete alisema kitendo cha Katibu huyo kumtaka Dk Slaa ajiuzulu kwa kumiliki kadi ya CCM ni utovu wa nidhamu.
“Kurudisha kadi ya chama cha awali, ni hiari ya mwenye kumiliki kadi hiyo kwani ni yake kwa sababu ameinunua na kuilipia,” alisema Mbwete.
Mgogoro wa Karatu
Wakati hayo yakiendelea mgogoro wa Wilaya ya Karatu, umechukua sura mpya baada ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji Wilaya hiyo kugoma kujiuzulu kwa maelezo kuwa Kamati Kuu ya Chadema haina mamlaka ya kuwaondoa.
Wakati viongozi hao wakitoa tamko hilo jana, tayari Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila ametua Karatu jana, kufanya maandalizi ya mikutano ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuanzia Jumamosi hadi Jumapili ili kukutana na viongozi wa chama hicho wadau wake katika kile kinachoelezwa kuweka “mambo sawa.”
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Moshi Darabe na Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse walisema jana kwamba wamesikitishwa na uamuzi ya kamati kuu ya kutangaza kusimamisha kamati hiyo yenye wajumbe 17 bila kuwasikiliza.
Darabe alisema awali, Kamati ya Utendaji ya Karatu, ndiyo ilikuwa inawatuhumu baadhi ya viongozi kwa kudhoofisha chama hicho na kushauri wachukuliwe hatua ambao ni Diwani wa Karatu Mjini, Jubilate Mnyeye, Katibu wa Wilaya hiyo, Raurence Bortha, Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya, Joseph Mtui na Katibu wake, Melkiori Mao.
“Sasa kamati kuu iliwaita na kuwahoji, tulitarajia wangetoa uamuzi kuhusiana na tuhuma tulizowapa lakini kusimamisha kamati nzima tunadhani si sahihi na pia ni ukiukwaji wa katiba ya chama,” alisema Darabe.
Natse alisema kikatiba, wanaamini kamati ya utendaji inaweza kuwajibishwa na mkutano mkuu wa wilaya na siyo kamati kuu.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema jana kuwa kimsingi, uamuzi uliofanyika ni wa kuisimamisha kamati ya utendaji kufanya kazi na si kuivunja au kuifukuza.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo alisema wakati huu ambao kamati hiyo imesimamishwa, Kamati Kuu ya chama ndiyo inayofanya uangalizi wa moja kwa moja kwa Wilaya ya Karatu kupitia mfumo itakaouweka hadi uamuzi mwingine utakapotolewa.

Washikiliwa Kwa Wizi Wa Kwenye Mitandao

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 20/12/2012

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kujihusisha na shughuli za wizi wa mtandao hususani katika maduka yanayotoa huduma za M-PESA,Tigo Pesa na Airtel Money katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Dodoma.
Watu hao ambao wanadaiwa kujipatia zaidi ya shilingi 1,730,000 /= kwa Mawakala wanne tofauti wanaotoa huduma hizo walikamatwa jana tarehe 19/12/2012 majira ya saa 12:00 hrs mchana.
Watuhumiwa hao ambao wanatokea Jijini Dar es Salaam majina yao ni Mohamed s/o Dotto @ Sefu, mwenye umri wa miaka (30) Mnyamwezi mkazi wa Kigogo, Mohamed s/o Pazi, Mzaramo Miaka (28) na Ally s/o Mohamed miaka (25) ambao ni wakazi wa Ilala.

Wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kufanikisha wizi huo, moja ya mbinu ni kwenda kwenye maduka yanayotoa huduma hizo na kumwambia wakala kuwa wanaharaka na kutaka kuweka Pesa kiasi fulani ambacho wanakuwa nazo mkononi na kuanza kuzihesabu.
Mara meseji ya pesa toka kwa wakala zinapoingia katika simu zao, simu zao huita wakati huo huo na kujifanya wanapokea simu huku wakisogea pembeni wakiongea na simu na kuondoka julma kwenda kuzitoa mahala pengine kwa haraka.

Wakala walioathirika na Wezi hao mpaka sasa ni Consolata d/o Martini ambaye duka lake liko eneo la Kuu Streetu shilingi 300,000/=, Perndo d/o Martin qambaye Duka lake liko eneo la CBE Tsh. 860,000/= Mlay s/o Felix eneo la Makole Tsh. 300,000/=, Masala s/o Mabula wa eneo la Changombe Tsh. 70,000/= na Duka la Lazia Shop ambalo liko Mtendeni Street Tshs 200,000/=.
Natoa wito kwa wamiliki na wakala wote wanatoa huduma hizo kuwa makini wanapoendesha shuguli zao, kwa kutoa taarifa za watu wanaowatilia shaka wanaofika kutaka huduma katika maduka yao mara moja ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

[D. A. MISIME – ACP]
KAMANDA WA POLISI [M] DODOMA

CONTACT:
POLISI MKOA WA DODOMA
DAWATI LA HABARI, ELIMU NA MAHUSIANO,
Phone: 0715 006523 – Luppy Kung’alo – Mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP)
Phone: 0712 360203 – Silyvester Onesmo – Police Konstebo (PC)

Saturday, December 15

Kadi ya Bima ya Afya yazua utata jijini Dar

HOSPITALI ya Hindu Mandal, Dar es Salaam imeuzuia mwili wa Marystela Alfonce aliyefariki juzi baada ya kubainika kuwa alikuwa akitumia kadi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ya mtu mwingine aliyetajwa kwa jina la Honorata Magezi ili kupata matibabu.
Hospitali hiyo jana ilikataa kutoa mwili wa marehemu Marystela hadi ilipwe Sh7.2 milioni ambazo ni gharama za matibabu tangu alipolazwa hospitalini hapo, Novemba 12, mwaka huu.
Mwandishi wetu alishuhudia gari la kubeba maiti aina ya Marcedes Benz lililofika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kuchukua mwili wa Marystela likiondoka bila kubeba mwili huo.
Ilielezwa kuwa, marehemu alikuwa akitumia kadi ya ndugu yake kupata matibabu katika hospitali hiyo hadi kifo kilipomkuta.
kutokana na tukio hilo, mume wa Honorata, Jovis Magezi anashikiliwa na polisi.
Magezi ambaye ni Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, alikamatwa jana baada ya kufika Hindu Mandal kwa lengo la kuchukua mwili wa marehemu kabla uongozi wa hospitali hiyo na Bima ya Afya kushtuka.
Daktari huyo alikamatwa baada ya maofisa hao kumbana kwa maswali.
Mahojiano ya daktari huyo na kikosikazi hicho yalikuwa kama ifuatavyo:
Ofisa wa Bima: Mna uhusiano gani na marehemu.
Magezi: Ni mke wangu.
Ofisa wa Bima: Mke wako alilazwa lini hapa hospitalini?
Magezi: Wiki mbili zilizopita.
Ofisa wa Bima: Huyo siyo mkeo ina maana hufahamu hata siku aliyolazwa mkeo hapa hospitali?
Magezi: Kimya.
Ofisa wa Bima: Tunaomba namba ya simu ya marehemu mkeo.
Magezi: Siikumbuki kwa sasa.
Ofisa wa Bima: Tueleze ukweli ili tujue namna ya kukusaidia. Sisi sote tunafahamu matatizo, usitufiche kwa sababu huonyeshi kama umefiwa na mke wako.
Magezi: Ukweli ni kwamba marehemu ni shemeji yangu. Alikuwa akitumia kadi ya bima ya dada yake ambaye ni mke wangu Honorata Magezi… jina halisi la marehemu ni Marystela Alfonce.
Baada ya kukiri, maofisa upelelezi wa Kituo cha Polisi Kati, walifika na kumweka chini ya ulinzi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marieta Komba alisema Magezi alikamatwa na kufikishwa katika kituo hicho lakini akaagiza aachiwe huru mara moja na atafutwe mkewe ambaye ndiye mwenye kadi iliyotumiwa na marehemu.
“Hatuwezi kumkamata Magezi kwa kosa la mkewe. Nimeagiza aachiwe na akamatwe mkewe ambaye ndiye mhusika,” alisema.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa (NHIF), Raphael Mwamoto alisema baada ya kubaini kadi hiyo kutumiwa na mtu ambaye si mwanachama, mfuko huo hautalipa deni hilo la Sh7.2 milioni.
“Tumemfikisha Magezi polisi ili asaidie kupatikana kwa mkewe Honorata ambaye kadi yake ndiyo ilitumika kutoa matibabu,” alisema na kuongeza:
“Kuhusu utata uliopo wa mwili wa marehemu tunawaachia Hospitali ya Hindu Mandal na ndugu wa marehemu, wao wataangalia namna ya kulitatua tatizo hilo.”
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Hindu Mandal, Dk Ramaiya Kaushik alisema mwili huo unashikiliwa na hospitali yake kutokana na matumizi yasiyo halali ya kadi ya Mfuko wa Bima ya Afya.
“Ni kweli tumepata tatizo hilo. Hii ni changamoto kwetu kuhakikisha kwamba tunaimarisha ukaguzi wa kadi hizi ili tatizo hili lisijirudie tena,” alisema Kaushik.
Alisema mgonjwa anaweza kufika mapokezi na kuonyesha kadi ya Mfuko wa Bima ya Afya na kwamba akijiandikisha mapokezi hadaiwi kadi hiyo katika idara nyingine yeyote.
“Sasa tutaanza kupokea kadi mapokezi na mgonjwa atatakiwa kuionyesha kila eneo la huduma atakapokuwa akienda ili kuimarisha zaidi usimamizi,” alisema Dk Kaushik.
Alipoulizwa mwili huo utashikiliwa hadi lini alisema: “Ninawasiliana na viongozi wengine wa hospitali hii ili tukae na ndugu wa marehemu tuone tutafanya nini, hili ni suala ambalo tunatakiwa kulimaliza kibinadamu bila upande wowote kuathirika,” alisema.
Waombolezaji
Nje ya hospitali hiyo kulikuwa na idadi kubwa ya waombolezaji, wengi wao wakiwa wanawake.
Mmoja wa waombolezaji ambaye alikataa kutaja jina lake alidai kwamba marehemu hakuwa na uhusiano wa kindugu na waliompa kadi hiyo na kuongeza kuwa ni watu wanaofahamiana lakini siyo ndugu.
Mwingine atiwa mbaroni
Mkazi wa Kigamboni, Andrew Mjetu anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Kati, Dar es Salaam akidaiwa kumpatia, Elias Jones kadi yake ya NHIF ili aitumie kupata dawa zenye thamani ya Sh1.2 milioni kinyume na sheria.
Mwamoto alidai kuwa Elias alikuwa akitibiwa katika Hospitali ya Saratani Ocean Road na aliandikiwa dawa za kununua kwenye maduka lakini hakuwa na kiasi hicho cha fedha.
“Ndipo akakutana na Andrew ambaye alikubali kumsaidia kwa kumpa kadi yake ili akachukulie dawa,” alisema Mwamoto.
Alisema alipopata kadi hiyo alikwenda katika ofisi za NHIF ili kupata dawa bila kujua kwamba kufanya hivyo ni kosa.
Akizungumza tukio hilo, Elias alisema ni bora angekamatwa yeye kwa sababu ugonjwa wake ndiyo uliomponza `msamaria mwema’.
“Yule si ndugu yangu lakini ameniona ninavyohangaika na maumivu akaamua kunisaidia, sasa cha ajabu yeye anawekwa ndani mimi nikiwa nje,” alisema huku akilia kwa sauti.

Pengo asema Shule TZ zimekuwa vitega uchumi

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema elimu inayotolewa nchini ni ya kibaguzi.
Kardinali Pengo alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akiwasilisha ujumbe wa maaskofu wa Kanisa Katoliki walioutoa katika mkutano wao uliofanyika Oktoba 7 hadi 28, mwaka huu huko Roma, Italia.
Alisema watu wote wenye mapenzi mema na nchi hii wanapaswa kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa elimu bora kwa kila Mtanzania.
Kardinali Pengo alisema hapendezwi na namna elimu inavyotolewa nchini kwani kimfumo, baadhi ya shule zimekuwa vitegauchumi, hivyo kuwa kikwazo kwa watu wenye kipato cha chini.
“Wenye vipato vya chini hawawezi kusoma katika shule hizi kwa sababu zinatoza ada kubwa ambayo maskini hawezi kumudu gharama zake,” alisema.
Askofu Pengo alionya kuwa endapo hali hiyo itaachiwa, inaweza kuwafanya wale waliokosa elimu kuwa chanzo cha vurugu kwa kuwa watasimama kidete kudai haki yao.
Maoni ya Katiba
Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo alizungumzia mchakato wa Maoni ya Katiba unaoendelea nchini, huku akiwaonya baadhi ya wanasiasa na taasisi mbalimbali za dini kuacha kuwashinikiza wananchi kutoa maoni kwa ajili ya masilahi yao binafsi.
“Kila mtu aruhusiwe kutoa maoni yake, lakini lazima tukubaliane kuwa kila mtu ana maoni yake na maoni yote hayawezi kuingizwa katika Katiba Mpya,” alisema Pengo.
Alisema kwa kuwa Katiba inagusa masilahi ya nchi, ni vyema kila mwananchi akatumia fursa yake ya kuwasilisha maoni yake mwenyewe.
Alitahadharisha kuwa wananchi wasiposhirikishwa katika mchakato wa Katiba Mpya, wanaweza kuja kuikataa kwa sababu maoni yao hayakuzingatiwa.
Suala la udini
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ameitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi kwa wale wote watakaobainika kusababisha uharibifu wa mali za dhehebu la dini yoyote hapa nchini, kama wanavyofanya pindi kunapotokea uhalifu katika benki au wizi katika maeneo ya viongozi na sehemu nyingine.
Alisema nchi imegawanyika katika madhehebu mbalimbali, hivyo inapotokea dhehebu moja kulitukana na kuharibu mali za jingine, Serikali haipaswi kukaa kimya.
Alisema Serikali inapaswa kuwa makini, ikiwamo kuwafuatilia na kuwachukulia hatua wale wote wanaoonyesha dalili za uvunjifu wa amani.
Aliwataka viongozi wenye dhamana kuacha kushabikia udini katika kusimamia haki za jamii kwa Watanzania.
Kardinali Pengo pia aliitaka Serikali kuchukua hatua juu ya mihadhara isiyofaa majukwaani.
“Mungu ametuumba ili tumwabudu kila mtu kwa dini yake, huna sababu ya kumtukana mwenzako au kuikashifu dini ya mwenzako, tunachotakiwa ni kufuata misingi na mema yote,” alisema.
Alisema kama Serikali inashindwa kuwakemea na kuwachukulia hatua wale wanaowatukana wenzao, hali hiyo ikiachwa inaweza kuvuruga amani na mshikamano na hivyo nchi kuingia kwenye mgogoro wa kidini.
Kardinali Pengo alisema haoni tatizo kama mtu atasema Yesu si mwana wa Mungu katika nia na mtazamo wake na mwingine akasema Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na siyo kutupiana maneno ambayo mwisho wa siku inakuwa ni chuki kubwa.

Thursday, December 13

Nelson Mandela making progress


JOHANNESBURG (AP) — South Africa's former President Nelson Mandela "has made progress" in getting better after contracting a lung infection, officials said Wednesday.
A short statement issued by current President Jacob Zuma's office announced Mandela's status, as the 94-year-old leader's stay in a military hospital near South Africa's capital, Pretoria, stretched into a fifth day Wednesday.
"Doctors attending to former President Mandela have reported that he has made progress during the past 24 hours and they are satisfied with the way he is responding to treatment," the statement by presidential spokesman Mac Maharaj said.
The statement offered no other details.
Mandela was admitted to 1 Military Hospital on Saturday for tests. It was several days before authorities announced that Mandela was ill. Each day he spends hospitalized has caused growing concern in South Africa, a nation of 50 million people that largely reveres Mandela for being the nation's first democratically elected president who sought to bring the country together after centuries of racial division.
In January 2011, Mandela was admitted to a Johannesburg hospital for what officials initially described as tests but what turned out to be an acute respiratory infection. The chaos that followed Mandela's stay at that public hospital, with journalists and the curious surrounding it and entering wards, saw the South African military take charge of his care and the government control the information about his health.
Mandela has a history with lung problems. He fell ill with tuberculosis in 1988 toward the tail-end of his prison years. While doctors said it caused no permanent damage to his lungs, doctors and experts say it can cause problems years later for those infected.
Mandela was a leader in the struggle against racist white rule in South Africa and once he emerged from 27 years in prison in 1990, he won worldwide acclaim for urging reconciliation. He won South Africa's first truly democratic elections in 1994, serving one five-year term. The Nobel laureate later retired from public life to live in his remote village of Qunu, in the Eastern Cape, and last made a public appearance when his country hosted the 2010 World Cup soccer tournament.
Mandela disengaged himself from the country's politics over the last decade but continued campaigning against AIDS. He has grown increasing frail in recent years.

Friday, December 7

Familia ya Sharo yaibua mazito

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Teule Muheza, Dk Julius Mjema aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sharo Milionea alisema sababu ya kifo chake ni kichwa kupondeka.

“Mimi ndiye niliyefanyia ‘postmoterm’ (uchunguzi), mwili wa Sharo Milionea, ni kwamba kichwa kilikuwa kimepondeka huku mifupa ya kichwa ikiwa imepondeka pia,” alisema Dk Mjema.
FAMILIA ya msanii Hussein Ramadhani Mkiety (Sharo Milionea) aliyekufa katika ajali wilayani Muheza wiki iliyopita imedai kuwa haiamini kwamba kifo cha mtoto huyo kilitokana na ajali, hivyo kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli.
Mjomba wa marehemu , Mohamed Msenga alisema jana kwamba familia imekuwa na shaka juu ya mazingira ya kifo hicho baada ya kurejeshewa nguo za msanii huyo zilizokuwa zimeibwa baada ya ajali lakini hazikuwa na damu.

Msenga alisema muda mfupi baada ya mama mzazi wa Marehemu Zaina Mwaimu Mkiety (54), kuitwa polisi na kukabidhiwa  vitu mbalimbali zikiwamo nguo ambazo marehemu alikuwa amevaa siku ya ajali hawakuona hata alama ya damu jambo ambalo liliwashangaza.
Alisema shaka hiyo ilianzia katika eneo ambalo ajali hiyo ilitokea akisema walipofika na kuonyeshwa mahala alipokuwa ameangukia, hawakuona damu jambo ambalo liliwatia shaka.
Alisema begi la nguo za msanii huyo lilikuwa na udongo mwingi likionyesha kwamba walioiba walikuwa wamelifukia kabla ya kusalimisha lakini hakuna damu zilizoonekana.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Teule Muheza, Dk Julius Mjema aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sharo Milionea alisema sababu ya kifo chake ni kichwa kupondeka.
“Mimi ndiye niliyefanyia ‘postmoterm’ (uchunguzi), mwili wa Sharo Milionea, ni kwamba kichwa kilikuwa kimepondeka huku mifupa ya kichwa ikiwa imepondeka pia,” alisema Dk Mjema.

Kuhusu madai ya nguo kutokuwa na damu, alisema marehemu alipata mpasuko wa ndani kwa ndani na siyo wa  nje, ndiyo maana alipofikishwa chumba cha maiti damu zilionekana zikiwa zimeganda masikioni.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alipoulizwa kuhusu madai hayo ya familia  alisema: “Hiyo ni taarifa ambayo jeshi la polisi litaifanyia kazi kwa kuingia kwa kina katika kuchunguza ili kuridhisha pande zote.”

Mama yake alia kukosa mjukuu
Katika hatua nyingine, mama mzazi wa msanii huyo amesema kutoachiwa mjukuu na tarehe za mwisho wa mwezi ni alama ambazo zitasababisha awe akimkumbuka mwanaye huyo milele. Akizungumza nyumbani kwake, katika Kitongoji cha Jibandeni Kijiji cha Lusanga wilayani hapa alisema kila ulipokuwa ukifikia mwisho wa mwezi ulikuwa ni muda wake wa neema kwani Sharo Milionea alimtumia fedha za matumizi yake binafsi pamoja na familia nzima nyumbani hapo.

“Pamoja na kwamba kila mara alikuwa akinitumia fedha za kutatua shida zangu mbalimbali nilizokuwa nikimweleza lakini kila mwisho wa mwezi alikuwa akihakikisha anatuma fungu la matumizi yangu na ndugu zake hapa nyumbani,” alisema mama huyo. Alisema mwisho wa mwezi itakuwa ni alama ya kudumu ya kumbukumbu ya mwanawe kwa sababu ni wakati ambao alikuwa akimtumia fedha za matumizi yake pamoja na familia nzima.


Kuhusu mjukuu alisema: “Sharo ni mwanangu wa pekee wa kiume, amekufa bila kuniachia mjukuu.. hii inaniuma sana lakini namshukuru Mungu kwani amechukua kiumbe chake na ndiye ajuaye siri iliyofichika mbele yangu,” alisema.

Alisema hadi alipofariki hakuwahi kumdokeza juu ya kuwa na mtoto wala kumpa mimba msichana yeyote... “Unajua Sharo Milionea alizaliwa pacha na mwenzake Hassan lakini mwenzake alifariki dunia siku tano baada ya kuzaliwa kwa hiyo katika kizazi changu mwanangu pekee wa kiume alikuwa Sharo Milionea ambaye nilitumaini kwamba angeniletea wajukuu,” alisema Zaina.

Alisema Sharo Milionea amekufa kabla hajatekeleza ndoto yake ya kumjengea nyumba ya kisasa pamoja na kuweka miradi ya kuboresha maisha yake azma ambayo aliiweka mwezi mmoja kabla ya kupata ajali iliyotoa uhai wake.

Atoa ya moyoni kwa walioshiriki msiba
Zaina alitoa shukrani za pekee kwa Rais Jakaya Kikwete na mkewe, Salma kwa kutuma ujumbe maalumu pamoja na rambirambi kutokana na msiba wa mwanaye huyo. Pia alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, wasanii, waandishi wa habari na kampuni mbalimbali zilizoshiriki pamoja na kutuma salamu za rambirambi.



Jaji Mark Bomani awashukia polisi

ASEMA WANATUMIA ZAIDINGUVU KULIKO MAARIFA
KUJIRUDIA kwa matukio ya polisi kutumia silaha za moto dhidi ya raia, kumepokewa kwa hisia tofauti, huku Mwanasheria Mkuu wa Kwanza wa Serikali, Jaji Mark Bomani akilitaka jeshi hilo kuacha kutumia nguvu wanapokuwa katika operesheni zao.Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti kuhusu tukio la hivi karibuni la kupigwa risasi mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, watu wa kada mbalimbali walisema, kitendo cha polisi kutumia nguvu sio busara.
Jaji Bomani kitendo cha polisi kutumia nguvu badala ya busara katika operesheni zao kinaweza kuleta uhasama kati ya wananchi na jeshi hilo.
“Kwa ujumla matumizi ya nguvu kwa polisi si mazuri  na nadhani tunatakiwa kubadilika katika hilo.” alisema Jaji Bomani. 
Bomani alieleza kuwa  kwa ujumla polisi wanatumia vibaya silaha zao ingawa bado hajapata uhakika wa jinsi  tukio la kujeruhiwa kwa Matutu lilivyokuwa .
Alisema tukio la Mwangosi lilikuwa baya zaidi lakini picha anayoiona na kuihusisha na tukio la juzi, ni kuwa kuna matumizi mabaya ya mashambulizi ya polisi kwa raia.
Hata hivyo wakati Jaji Bomani akieleza hayo Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu Amiri Ramadhan Manento  alisema kila tukio linalofanywa na polisi linatakiwa kufanyiwa uchunguzi kabla ya kuanza kulizungumzia.
Jaji Manento alisema akiwa ni mwanasheria hawezi kutoa hitimisho ya tukio la kujeruhiwa kwa Matutu kabla ya uchunguzi wa kisheria kufanyika.
“Tunahitaji kujua mambo mengi, ya michakato ya makosa ya jinai, (criminal procedure) kwa mfano polisi walipoingia walifanya nini, walipotoka, ni maneno gani walimuuliza mtu wa kwanza waliyekutana naye.
Tunahitaji kujua iwapo walitumia kizuizi cha usalama(safe cage) katika silaha zao au la” alisema Jaji Manento
Alisema kulingana na taarifa zilizopo katika magazeti bado unahitajika uchunguzi wa kujua  ni namna gani polisi waliingia ndani ya nyumba hiyo.
Aidha Jaji huyo mstaafu alisema hawezi kuwahukumu polisi moja kwa moja kwani hakuna ushahidi kuwa walikuwa wakimwinda mwandishi, bali inawezekana waligundua kuwa ni mwandishi baada ya kumjeruhi.
Alisema hili ni tukio la tofauti na lile la kuuwa kwa Mwangosi kwani Mwangosi alikuwa kashika vifaa vyake vya kazi lakini hapa Matutu hakuwa na kitambulisho chochote kuwa ni Mwandishi.
“Unajua polisi wanafuata amri na sheria na wapo kwa ajili ya kulinda raia wake, hivyo hatuwezi kusema kuwa walikuwa wakimwinda mwandishi, kwa sababu hata polisi naye amejeruhiwa kwa panga katika tukio hilo,” alisema Jaji Manento
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dk Kitila Mkumbo alisema kuwa jeshi la Polisi limekuwa halifanyi kazi zake kwa kufuata weledi hali inayosababisha kuongezeka kwa matukio ya raia kupigwa risasi na Taasisi ya serikali yenye dhamana ya kuimarisha usalama wa raia hao.
“Matukio haya yanaweza kuathiri amani ya nchi kwa sababu wananchi wakikosa imani na serikali yao wanaweza kufanya jambo lolote bila kufuata sharia, matokeo yake amani inatoweka” alisema Dk Mkumbo.
Dk Mkumbo aliongeza kuwa ni vema IGP Saidi Mwema akatilia mkazo juu ya kufanya kazi kwa weledi ili kuimarisha utendaji kazi wa jeshi la polisi na kulipa taswira mpya katika jamii.
Mkuu wa Idara ya Fedha waskuli ya Biashara chuoni hapoDk Esther Ishengoma alisema kuwa jeshi la Polisi linadhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao, litaendelea kubeba dhamana hiyo, jambo la msingi ni kudhibiti nidhanu ya askari wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.

“Ukiangalia matukio yanayotokea utaona kuna baadhi ya askari polisi wanaolichafua jeshi kwa kufanya mambo kinyume cha sheria, ni vema suala la nidhamu likaimarishwa ili kuongeza ufanisi,” alisema Dk Ishengoma.
Mkazi wa Mbagala Mtongani Solomon Isaiah alisema matendo yanayofanywa na polisi ya kujeruhi na kuua raia  ndani ya kipindi kifupi ni dalili za kutokuwepo utawala bora nchini na usimamizi mzuri wa ngazi za juu ndani ya Polisi.
“Hawa polisi hawajitakii kufanya hivyo bali wanatekeleza amri za viongozi wao wa ngazi za juu, hivyo basi lawama, hatua za kisheria  na mabadiliko yafanyike kwenye ngazi hizo za juu za polisi ndipo wahamie kwa polisi wenyewe” alisema Isaiah.
Matukio ya kuua na kujeruhi raia yanayotekelezwa na jeshi la polisi yamezidi kuongezeka siku hadi siku nchini licha ya wadau na wananchi kupigia kelele matendo hayo hali ambayo imezidi kugharimu maisha ya Watanzania wengi wasio na hatia kwa kuchukua sheria mkononi.
Hivi karibuni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kiliazimia kuishtaki Serikali kwa Mahakama ya Kimataifa ya masuala yaUhalifu(ICC) ili ichukue hatua zaidi juu ya mfululizo wa matukio ya kutisha yanayofanywa na jeshi la polisi kwa Wananchi baada ya Serikali kushindwa kuchukua hatua stahiki.
Kauli hizo imekuja siku moja baada ya polisi kulizungumzia tukio hilo kwamba lilitokea wakati wakiwa wanajihami.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela akizungumzia tukio la mwandishi huyo kupigwa risasi alisema alijeruhiwa baada ya kuanza kumshambulia askari kwa Panga.
Hata hivyo ufafanuzi wa kamanda huyo unatofautiana na ule wa Matutu na mashuhuda wa tukio hilo, ambao walisema kuwa polisi walivamia nyumba ya mwandishi huyo iliyopo maeneo ya Kunduchi huku wakimtaka mwanamke mmoja waliyemtaja kwa jina la mama J.
Katika maelezo yake Matutu alisema polisi hao walifika nyumbani kwake wakimtaka mkewe baada ya kumfananisha na mtu mwingine, kwamba wakati akiwa katika harakati za kumtenganisha mke polisi hao baada ya kuhisi  huenda wakawa majambazi ndipo polisi hao wakampiga risasi ya b