Wanasiasa saba wa upinzani wakiwemo viongozi wa juu wa chama kikuu cha upinzani Tanzania Chadema wameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwapatia dhamana wanasiasa sita wiki iliyopita lakini waliendelea kubaki rumande kwa kuwa hawakuwepo mahakamani kukamilisha masharti ya dhamana yao.
Mtuhumiwa wa saba, Halima Mdee, ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, aliongezwa leo katika orodha ya washtakiwa na kufanya jumla ya washtakiwa kuwa saba.
Washtakiwa wote wanakabiliwa na mshtaka nane ambayo ni pamoja na kukusanyika na kufanya maandamano kinyume na sheria pamoja na kutoa maneno yanayoweza kusababisha vurugu na chuki miongoni mwa jamii.
Mwandishi wa BBC, Sammy Awami, aliyekuwepo mahakamani ameelezea kuwa upande wa mashtaka mwanzoni ulihoji kwamba kwa kuwa Halima alikiuka masharti ya dhamana ya polisi na kwamba hakuripoti kituoni kama alivyotakiwa basi anyimwe dhamana kwa kukosa uaminifu.
Lakini hakimu alijibu kwamba, Polisi ni taasisi nyingine na mahakama ni taasisi nyingine, hivyo kushindwa kwake kutii dhamana ya polisi hakumuondolei haki ya kupata dhamana ya mahakama.
Kwa msingi huo, Halima Mdee pia amepatiwa dhamana kwa masharti kama yale yale ya wenzake wa awali ambayo ni pamoja na wadhamini wawili, kila mdhamini asaini bondi ya shilingi za Kitanzania milioni 20 na kukaidhi vitambulisho vinavyotambulika kisheria.
Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi hiyo ametaja tarehe 16 April kuwa ndio siku ya Kusikilizwa kwa awali (preliminary hearing) kwa kesi ya wanasiasa hao.
Awali Eagan Salla, mwandishi wa BBC alielezea hali ya mazingira ya mahakama ya Kisutu, akisema, 'hali ya ulinzi mahakamani imeimarishwa ijapokuwa wafuasi wa Chadema nao wanaonekana nje ya mahakama wakisubiri hatima ya viongozi wao'
No comments:
Post a Comment