Tuesday, April 10

Rungwe aendelea kumsaka mpwa wake


Mwenyekiti wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), Hashim Rungwe bado anahaha kumsaka mpwa wake aliyotoweka hivi karibuni huku mmoja ambaye naye pia alitoweka amepatikana.
Ndugu wa mwanasiasa huyo, Abdalah Kutiku na mkewe, Saida Hilal walitoweka katika mazingira ya kutatanisha lakini baadaye Saida alipatikana na kurejea nyumbani wakati mumewe hajulikani alipo.
Akizungumzia matukio hayo, Rungwe amesema mjukuu wake huyo wa kike amerejea nyumbani akiwa salama lakini sehemu aliko mumewe bado haijulikani.
“Amepatikana na tukimuuliza sehemu alikuwa akishikiliwa anasema hajui ila yupo salama hapa nyumbani. Huyu mwingine bado hajapatikana na hatujui lini atapatikana,” amesema.
Hivi karibuni, Rungwe aliliomba jeshi la polisi kusaidia upatikanaji wa mpwa wake na mumewe ambao hawajaonekana tangu Machi 26, 2018 majira ya asubuhi.
“Kila nikienda polisi kujua wamefikia wapi wanasema bado....niko kwenye taharuki kubwa kutokana na tukio hili,” alisema Rungwe alipozungumza na gazeti hili.
Rungwe alisema  sehemu zote ambazo alikuwa anapenda kutembelea wamepita lakini hakuna kitu walichoambulia.
“Sehemu zote tumepita na hatujafanikiwa, tunaomba vyombo vya dola watusaidie kuwatafuta hawa wote na kama wanawashikilia kwa mujibu wa sheria tungeomba tufahamu ili iweze kutuondolea hofu kubwa tuliyonayo,” alisema.

No comments:

Post a Comment