Thursday, April 26

Polisi na Waandamanaji: Je ni wakati gani silaha za moto zitumike?

Picha ya Akwelina Akwilini ilipambwa na maua katika ibada ya kuaga mwili wake
Image captionPicha ya Akwelina Akwilini ilipambwa na maua katika ibada ya kuaga mwili wake
Kisa cha mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu nchini Tanzania kuuwawa kwa risasi wakati polisi ya nchi hiyo ilipokuwa ikitawanya kile walichokiita mkutano usio halali wa wafuasi wa upinzani kimeibua maswali na hisia kali miongoni mwa umma juu ya kiwango cha nguvu ambacho polisi hutumia wanapokabiliano na waandamanaji.
Maelezo ya kifo cha msichana huyo yamedai hakulengwa moja kwa moja kwa sababu hakuwa sehemu ya waandamanaji wala kitisho kwa usalama
Lakini polisi wameshutumiwa kwa kutumia risasi za moto zilizosababusha kifo chake. Polisi wenyewe wanasema uchunguzi bado unaendelea kubaini aliyehusika na kifo hicho.
Lakini Tanzania haiko peke yake. Aghalabu idara za polisi katika nchi nyingi za Afrika zimejipata lawamani katika mikasa mingi ya aina hiyo kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa kudhibiti fujo na ghasia ikiwemo matumizi ya silaha za moto ambazo taathira zake huwa kifo au majeraha ya kudumu kwa aliyelengwa.
.
Image caption.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala juu ya iwapo maafisa wa polisi barani Afrika hupatiwa mafunzo madhubuti na vifaa vya kisasa kukabiliana na uhalifu, fujo na ghasia bila kuhatarisha usalama wao binafsi na wale wanao wadhibiti.
Polisi waliwatia mbarani watu 40 wanaodaiwa kushiriki kwenye maandamano wiki iliyopita nchini Tanzania
Image captionPolisi waliwatia mbarani watu 40 wanaodaiwa kushiriki kwenye maandamano wiki iliyopita nchini Tanzania
Mjadala wa aina hii umehanikiza zaidi juu ya namna polisi inavyodhibiti mikusanyiko ya kiraia kama maandamano ambayo inatazamwa kuwa haki za msingi za raia kuliko jinsi polisi inavyokabiliana na matukio kama ujambazi na uporaji.
Baadhi ya wapita njia walijipata katikati ya vurugu baina ya waandamanaji na polisi
Image captionBaadhi ya wapita njia walijipata katikati ya vurugu baina ya waandamanaji na polisi
Sehemu kubwa ya lawama kwa polisi karibu kwenye matukio yote hususan ya maandamano ya raia, wanakosolewa kwa kutumia nguvu kubwa dhidi ya watu wasio na silaha na tena katika mazingira ambayo mbinu nyepesi zingeweza kusaidia kurudisha utulivu.

Hali ikoje barani Afrika?

Ingawa suala la polisi kulenga raia kwa silaha za moto ni la kilimwengu ukipigia mfano wa matukio kama hayo nchini Marekani dhidi ya raia weusi, hali ni dhaifu zaidi kwenye nchi maskini na zaidi Afrika ambapo ni nadra makosa kama hayo kuripotiwa au wakosaji kushughulikiwa kisheria.
Polisi wavunja maandamano ya upinzani KenyaHaki miliki ya pichaAFP
Image captionPolisi wavunja maandamano ya upinzani Kenya, 2017
Kulingana na ripoti ya karibuni kabisa ya mwaka 2016/2017 ya shirika la Amnesty International, Kenya ndiyo nchi inayoongoza kusini mwa jangwa la Sahara kwa visa vya polisi kuua au kujeruhi raia kwa kutumia risasi za moto.
Karibu watu 122 waliuliwa na polisi katika matukio mbalimbali kati ya mwaka 2016 hadi mwanzoni mwa 2017.
Maandamano NairobiHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWafuasi wa upinzani Kenya walikutana na polisi wenye mabomu ya kutoa machozi walipoandamana kushinikiza mageuzi IEBC, 2017
Ripoti hiyo ilizitaja pia nchi nyingine tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za Tanzania, Burundi na Sudani Kusini kuwa miongoni mwa mataifa vinara ambayo polisi wanatumia nguvu kupita kiasi na kuwakandamiza zaidi wafuasi wa upinzani.
Maelezo ya taarifa hiyo yalifichua kwa jumla ukweli kwamba polisi katika nchi za Afrika ikiwemo Afrika mashariki hutumia nguvu kupita kiasi na huenda mbali zaidi ya kanuni za mifumo ya ulinzi iliyoboreshwa na jumuiya ya kimataifa zinazoweka kikomo cha matumizi ya nguvu na hasa silaha za moto dhidi ya raia.

Polisi wanaweza kutumia silaha za moto?

PolisiHaki miliki ya pichaREUTERS
Suala la wakati gani vyombo vya ulinzi wa raia hasa polisi unakubalika kutumia nguvu kubwa na hata silaha za moto kukabili uhalifu au ghasia limetolewa muongozo wa kiulimwengu na umoja wa mataifa na nguvu zaidi kuweka katika ama katiba au sheria za nchi husika.
Umoja wa Mataifa kupitia afisi yake ya masuala ya ulinzi wa Haki za Binadamu umeweka masharti katika azimio la Havana la mwaka 1990 la Matumizi ya Nguvu na silaha za moto kwa wasimamizi wa sheria.
Polisi walirusha gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji kadha waliokusanyika NairobiHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionPolisi wakirusha gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji kadha waliokusanyika Nairobi, 2017
Kwanza, Ibara ya 13 na 14 ya azimio hilo zinapiga marufuku vyombo vya kipolisi kutawanya maandamano yaliyoitishwa kisheria kwa kuwa ni sehemu ya haki msingi za raia.
'Iwapo polisi italazimika kutawanya mikusanyiko batili ambayo haina rapsha wala vurugu wanapaswa kujiepusha kutumia nguvu. Pindi italazimu nguvu kutumika basi iwe ya kiwango cha chini kadiri iwezekanavyo' inasema sehemu ya ibara hizo.
Polisi akishika doria
Kadhalika, azimio hilo limetoa pia muongozo kwa wasimamizi wa sheria kutumia nguvu ikiwemo silaha za moto pale TU wanapojilinda wenyewe au kuwalinda wengine dhidi ya kitisho cha wazi kinachoweza kusababisha kifo au majeraha makubwa'
Hata hivyo malalamiko makubwa ya watu ni kuwa masharti hayo ambayo yameorodheshwa pia kwenye sheria nyingi za nchi za afrika yamekuwa yakipuuzwa, na mara kadhaa polisi imeonekana kupendelea zaidi njia za kikatili za kutumia silaha za moto hata kama mikusanyiko na maandamano ni tulivu.

Polisi wanafunzwa nini vyuoni?

Kulingana na sera za mafunzo ya polisi zinazotumiwa na vyuo vingi vya polisi barani Afrika maafisa wa polisi wanapaswa kwanza kutathmini kitisho kilichopo katika kiwango cha madhara ya mwili au uhai kwao au kwa wengine kabla ya kutumia bunduki zao.
Polisi nchini Ghana wakiwa katika mazoeziHaki miliki ya pichaAFP
Image captionPolisi nchini Ghana wakiwa katika mazoezi
Mathalan, mwongozo wa mafunzo ya polisi nchini Kenya, unaelekeza kuwa 'matumizi ya silaha za moto yanapaswa mara zote kuwa ni jambo la mwisho kabisa' na pale silaha ya moto inapotumika basi iwe kwa mhalifu mwenye silaha ya kitisho na ilenge tu kuutia ganzi uwezo wa kusababisha madhara.
Lakini kuna wasiwasi iwapo maafisa wa polisi wanazingatia mafunzo haya.

Maafisa wa polisi wana mafunzo ya kutosha?

Mauaji ya raia 34 kwenye mgodi wa Marikana nchini Afrika Kusini yaliyofanywa na polisi kwa kutumia bunduki za rashasha yaliongeza miito ya kuitaka serikali ya nchi hiyo kulifanyia marekebisho jeshi la polisi la nchi hiyo ambayo limekuwa na rekodi mbaya katika udhibiti wa ghasia kwa kutumia silaha za moto.
Waandamanaji wakionesha mabango yanayoshutumu polisi kusababisha mauaji ya wachimba migodi Marikana, Afrika Kusini, Oktoba 21, 2012Haki miliki ya pichaAFP/ GETTY IMAGES
Image captionWaandamanaji wakionesha mabango yanayoshutumu polisi kusababisha mauaji ya wachimba migodi Marikana, Afrika Kusini, Oktoba 21, 2012
Wakati mmoja chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kilifichua siri nzito iliyoonesha kuwa askari 3500 wa jeshi la polisi nchi hawakuwa na mafunzo ya kutosha wala ithibati ya kutumia silaha ingawa walikabidhiwa bunduki. Waziri wa masuala ya polisi Fikile Mbalula alikiri kufahamu dosari hiyo na alitoa ahadi ya kuchukua hatua.
Polisi wakizingira miili ya wachimbaji baada ya mapambano baina yao na wachimbaji katika mgodi Marikana, Agosti 16, 2012.Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionPolisi wakizingira miili ya wachimbaji baada ya mapambano baina yao na wachimbaji katika mgodi Marikana, Agosti 16, 2012.
Hii ina maana kuwa askari wengi hawakuwa na uwezo wa kudhibiti mienendo yao wakiwa na silaha na mwishowe huishia kuzitumia bila sababu zinazokubalika kisheria.
Taarifa hizo ziliibua swali kubwa, ikiwa Afrika Kusini, moja ya nchi zilizopiga hatua muhimu za maendeleo hasa ya uchumi barani Afrika, ina tatizo la aina hiyo yumkini hali ni mbaya zaidi kwa nchi nyingine ambazo hutenga bajeti ndogo ya mafunzo ziada kwa maafisa wa polisi na wala hazitoi ithibati ya kukabidhiwa na kutumia silaha za moto.

Kuna njia mbadala?

.Haki miliki ya pichaGALLO IMAGES
Image caption.
Kwa kuwa ukweli ni kwamba siyo kila wakati mambo huwa shwari au si kila mkusanyiko wa raia huwa na nia njema, utulivu na unaofuata sheria, Polisi inao wajibu wa kutimiza majukumu yao ya kulinda amani lakini kwa kuwekeza nguvu zaidi kwenye mbinu za kiungwana za kudhibiti uvunjifu wa sheria badala ya silaha za moto
Mataifa yaliyoendela yanatumia njia kadhaa zinazokubalika kitaalamu kuwa haziwezi kuleta madhara makubwa au majeraha ya kudumu kwa mlengwa. Gesi za kutoa machozi, maji ya kuwasha, risasi za mpira na hata virungu vya plastiki vinaweza kusaidia.
Siyo kwamba vifaa na mafunzo ya kutumia mifumo haipo Afrika, laa! Ni vile tu polisi wa Afrika inazingatia nguvu na mabavu kuwa suluhu la kila jambo kwenye usimamizi wa sharia.

Polisi inaweza kubadilika Afrika

Kwa jumla itachukua muda kwa idara za polisi barani Afrika kubadilika kwa sababu nyingi hufanya kazi kwa shinikizo za viongozi wa siasa na watawala ambao ndiyo watoa amri wakuu kwa vyombo hivyo vya usalama.
Polisi akipoozwa na mwenzake baada ya kujeruhiwa na waandamanaji mjini Kampala , UgandaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionPolisi akipoozwa na mwenzake baada ya kujeruhiwa na waandamanaji mjini Kampala , Uganda
Pindi wanasiasa wa Afrika watatambua kuwa maandamano na haki ya kukusanya kwa amani au kupinga masuala fulani fulani kwa njia za wazi ni haki za kawaida za raia, polisi haitotiwa hatiani kwa kuua au kujeruhi watu kwa silaha za moto.
Utambuzi huo utasaidia kuzifanya idara za polisi zilenge zaidi kutoa huduma badala ya mabavu na watawala kujielekeza kwenye kutimiza ahadi za kampeni na Maisha bora ya watu badala ya kuwekeza mamilioni ya fedha kununua silaha au kugharamia mazishi ya raia wasio na hatia waliouwawa kwa risasi.

No comments:

Post a Comment