Mwanasiasa wa upinzani aliyezuiwa kuingia Kenya wiki iliyopita na kusafirishwa kwa lazima hadi Dubai amewasili nchini Canada.
Bw Miguna Miguna, ambaye ni wakili, alisafiri kwa ndege iliyokuwa ikielekea Toronto, Canada, baada ya kukaa katika uwanja wa kimataifa wa Dubai kwa siku nne.
Mmoja wa mawakili wa mwanasiasa huyo Nelson Havi ameandika kwenye Twitter kwamba Bw Miguna amesafiri kwenda Canada kwa hiari kupitia usaidizi wa ubalozi wa Canada katika Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE).
Bw Havi amesema Miguna atafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na "atarejea baadaye".
Gazeti la Nation, limesema afisa mmoja wa serikali amewafahamisha kwamba Bw Miguna aliondoka Dubai akitumia ndege ya Air Canada 57 (ACA57) baada ya kuwasilisha pasipoti yake ya Canada.
Bw Miguna alikuwa amesema hakuwa na pasipoti hiyo alipowasili uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi Jumatatu wiki iliyopita.
Bw Miguna ndiye aliyeidhinisha kiapo cha Bw Raila Odinga alipokuwa anajiapisha kuwa 'Rais wa Wananchi' mwezi Januari.
Bw Miguna Miguna alijaribu kurejea Kenya Jumatatu lakini akazuiwa kuingia baada yake kudaiwa kutowasilisha pasipoti ya Canada ambayo ilitumiwa kumsafirisha kwa nguvu hadi Canada.
Wakili huyo alisisitiza kwamba ni raia wa Kenya na hafai kuzuiwa kurejea.
Taarifa zinasema Bw Miguna, ambaye pasipoti yake ya Kenya ilitwaliwa na polisi kabla ya kuondolewa kwake Kenya mwezi jana, alikuwa ametakiwa kuwasilisha ombi la kupata visa ya kukaa Kenya kwa miezi sita kwa kutumia pasipoti hiyo yake ya Canada.
Alikataa jaribio hilo na badala yake kutoa kitambulisho chake cha taifa kuonesha kwamba yeye ni Mkenya na kutaka aruhusiwe kuingia.
Bw Miguna, aliyekuwa amewasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mwendo wa saa nane adhuhuri, alikesha kwenye uwanja huo.
Maafisa walijaribu kumsafirisha kutoka uwanja huo mara ya kwanza kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates ambayo ilikuwa inaelekea Canada kupitia Dubai usiku huo wa Jumatatu lakini hawakufanikiwa.
Hata hivyo, walifanikiwa usiku wa kuamkia Jumatano.
Bw Miguna asubuhi aliandika kwenye Facebook kwamba aliamka na kujipata yuko Dubai na kwamba anahitaji matibabu.
Mwanasiasa huyo alisema alisindikizwa na afisa wa idara ya ujasusi na kwamba amemuona daktari uwanja wa ndege.
Bw Miguna alisisitiza kwamba hatasafiri kwenda popote ila kurejea Nairobi.
Serikali imechukua hatua hiyo licha ya kuwepo kwa maagizo ya mahakama ya kuzuia kutimuliwa kwake na ya kuitaka serikali kufanikisha kurejea kwake nchini humo.
Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga aliwapata na hatia waziri wa usalama nchini humo, mkuu wa polisi na mkuu wa idara ya uhamiaji ya kukaidi maagizo ya mahakama iwapo wangekataa kumwachilia huru.
Aliwatoza faini ya Sh200,000 (Dola 2,000) kila mmoja.
Kukamatwa kwa Miguna mara ya kwanza
Bw Miguna alikamatwa na polisi kwa mchango wake katika kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa "rais wa wananchi", hafla iliyofanyika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi mnamo 30 Januari.
Bw Miguna, ambaye pia ni wakili, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo ya Bw Odinga.
Serikali ilikuwa imeeleza hatua hiyo ya kiongozi huyo wa upinzani kuwa uhaini wa hali ya juu.
Bw Odinga anadai kwamba alimshinda Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 8 Agosti ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu kwa sababu ya kutokea kwa kasoro nyingi.
Mahakama iliamuru uchaguzi mpya ufanyike lakini Bw Odinga akasusia uchaguzi huo mnamo 26 Oktoba.
Chini ya Kifungu 17 cha Katiba ya Kenya, mtu aliyezaliwa nchini Kenya anaweza tu kuupoteza uraia wake iwapo itabainika kwamba aliupata uraia huo kwa njia ya ulaghai, au ibainike kwamba mtu huyo au wazazi wake walikuwa raia wa nchi nyingine, au ibainike kwamba mtu huyo alikuwa na umri wa zaidi ya miaka minane alipogunduliwa akiishi Kenya.
Serikali ya Kenya imekuwa ikisisitiza kwamba chini ya katiba ya zamani, Wakenya hawangekuwa na uraia wa nchi mbili.
Serikali inasema hatua ya Bw Miguna ya kupata pasipoti ya Canada mwaka 1988 ina maana kwamba aliupoteza uraia wa Kenya wakati huo.
Ingawa Bw Miguna aliwasilisha maombi na akapewa pasipoti ya Kenya mwaka 2009, serikali inasema pasipoti hiyo ya Kenya si halali kwa sababu hakufichua kwamba wakati huo alikuwa raia wa Canada pia.
Serikali imesema mwanasiasa huyo hakuwasilisha tena ombi la kuruhusiwa kuwa raia wa Kenya katiba ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2010 na Wakenya wakakubaliwa kuwa na uraia wa nchi mbili.
Bw Miguna amekuwa akisisitiza kwamba hakuwahi kuukana uraia wake wa Kenya na kamwe hawezi kufanya hivyo.
"Katiba iko wazi kabisa: hakuna mtu yeytoe anayeweza au anayeweza kudai kuufuta uraia wa Mkenya aliyezaliwa nchini Kenya," alisema awali.
Matukio makuu mzozo kuhusu Miguna
30 Januari: Miguna aidhinisha hati ya kiapo cha Raila Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi'
2 Februari: Atangaza kwamba amekamatwa na polisi Nairobi
6 Februari: Afurushwa kutoka Kenya na kupelekwa Canada
16 Machi: Odinga waambia wafuasi wake kwamba baada ya mapato yake na Bw Kenyatta, Miguna anafaa kuruhusiwa kurejea Kenya bila masharti
26 Machi: Arejea Kenya lakini azuiliwa uwanja wa ndege wa JKIA. Baadaye usiku, anusurika jaribio la kumpeleka Dubai.
28 Machi: Miguna apelekwa Dubai kwa nguvu. Asema anafahamu mipango ya kumpeleka hadi London.
Miguna Miguna ni nani?
Miguna alizaliwa katika kijiji cha Magina, katika jimbo la Kisumu, magharibi mwa Kenya.
Bw Miguna amekuwa kiongozi wa kundi linaloitwa National Resistance Movement (NRM, Vuguvugu la Taifa la Kupinga Serikali), ambalo liliundwa na muungano wa upinzani wa National Super Alliance siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ambao Bw Odinga alisusia mnamo 26 Oktoba mwaka jana.
"Utakuwa ni muungano wa ukombozi," alisema Bw Odinga akitangaza kuundwa kwa vuguvugu hilo.
"Tumesema hatutaheshimu serikali dhalimu."
Bw Miguna baadaye alijitangaza kuwa Jenerali wa NRM.
Mnamo 30 Januari, siku ya kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi', muungano huo uliorodheshwa kuwa kundi haramu na waziri wa usalama Dkt Fred Matiang'i.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Bw Miguna kujipata akikabiliana na serikali na nguvu zake.
Mwaka 1988, alikamatwa na serikali ya wakati huo ya Rais Daniel arap Moi.
Bw Miguna baadaye alitorokea Kenya ambapo alipata hifadhi kama mkimbizi wa kisiasa.
Alirejea nchini Kenya na akashiriki katika kampeni za uchaguzi za Bw Odinga na chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM) mwaka 2007.
Uchaguzi wa mwaka huo ulikumbwa na utata na baada ya serikali ya muungano kati ya Bw Odinga na Rais Mwai Kibaki kuundwa, ambapo Bw Odinga aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Bw Miguna alihudumu kama mmoja wa washauri wake kati ya 2009 na 2011
Wawili hao walizozana na Bw Miguna akawa mmoja wa wakosoaji wakuu wa Bw Odinga.
Aliandika kitabu kwa jina Peeling Back the Mask ambapo alimkosoa sana Bw Odinga na uongozi wake.
Mwaka 2013, alimuunga mkono Bw Kenyatta katika uchaguzi wa urais mwaka huo.
Lakini alibadilisha tena msimamo wake na kurejea upande wa Bw Odinga mwaka 2017, mwaka ambao aliwania pia wadhifa wa Gavana wa Nairobi katika uchaguzi uliofanyika Agosti ingawa kama mgombea ambaye hakuwa na chama.
Januari 30 mwaka huu, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo cha Bw Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi'.
Bw Odinga alipokutana na Bw Kenyatta mnamo 9 Machi na wakaahidi kuunganisha Kenya, Bw Miguna ni miongoni mwa waliomkosoa kiongozi huyo wa upinzani kwa hatua hiyo akisema huo ulikuwa sawa na usaliti.
No comments:
Post a Comment