Tuesday, April 10

Mfumuko wa bei wapungua


Kasi ndogo ya mabadiliko ya bidhaa za vyakula imesababisha mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi uliopita Machi kupungua kwa asilimia 0.2 kutoka asilimia 4.1 mwezi Februari hadi asilimia 3.9.
Mkurugenzi wa sensa na takwimu za jamii Ephraim Kwisegabo wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) amesema mara ya mwisho kiwango hicho cha kasi ya kuongezeka kwa bei chini ya asilimia 4 kilishuhudiwa  Mei mwaka 2004.
“Bidhaa za vyakula ambazo ndizo huchukulia mzania mkubwa kwa ujumla kasi yake ya ongezeko la bei ipo chini. Kati ya kipindi cha Machi 2017 hadi Machi 2018 kasi ya bei ya mtama imepungua kwa asilimia 7.1, unga wa mhogo asilimia 6.7, maharage asilimia 3.9 mihogo kwa asilimia 16.6 na ndizi kwa asilimia 16.7,”amesema Kwisegabo.
Aidha hali ya mfumuko wa bei katika nchi za Afrika Mashariki nayo imepungua katika kipindi hicho, Uganda umepungua kwa asilimia 0.1 kutoka asilimia 2.1 hadi asilimia 2.0, Kenya umepungua kwa asilimia 0.28 kutoka asilimia 4.46 hadi asilimia 4.18.
Hata hivyo Kwisegabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei haimaanishi moja kwa moja kuwa gharama za maisha zimepungua ila kuna uhusiano wa karibu.
Kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta na mfumuko wa uchumi Kwisegabo amesema, mafuta yamepanda bei mwezi huu hivyo athari yake itaonekana katika ripoti ya mwezi unaofuata.

No comments:

Post a Comment