Bakwata imesema muundo na mfumo wake tangu kuanzishwa ndiyo kiunganishi cha Waislamu nchini.
Baraza hilo limesema upatikanaji wa masheikh wa mikoa na wilaya awali ulikuwa kama mfumo wa kisiasa jambo lililosababisha kupatikana kiongozi wa kiroho asiyekuwa na sifa zinazohitajika.
Kwa mfumo mpya, Bakwata imesema sasa atakayeteuliwa atakuwa mwenye vigezo stahiki.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na mwenyekiti wa Halmashauri ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka katika mahojiano yaliyofanyika ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam.
Mabadiliko yaliyofanywa na Bakwata kupitia mkutano mkuu wa Machi 31 hadi Aprili Mosi mjini Dodoma, ambayo yalitangazwa Aprili 5 na Sheikh Mataka yanahusu namna ya kuwapata masheikh wa mikoa na wilaya ambao sasa watakuwa wakiteuliwa na Baraza la Ulamaa.
Katika mabadiliko hayo, masheikh wa kata watateuliwa na baraza la masheikh wa wilaya na maimamu wa misikiti.
Katika mahojiano na Mwananchi, Sheikh Mataka anasema suala hilo lilianza tangu mwaka 2015 kuangalia mfumo unaotumika kuwapata masheikh na maimamu na kubaini ulikuwa na kasoro.
Alisema baada ya tafakuri walibaini, “Usheikh ni taaluma na uchaguzi wake unahitaji vigezo vya kitaaluma, lakini waliokuwa wakiwachagua walikuwa wakichagua kama mfumo wa kisiasa; unaweza kumpata mtu ambaye hana vigezo na walikuwa wakimchagua wakati mwingine kihisia si kwa vigezo.”
Sheikh Mataka alisema kinachofanyika sasa wamepeleka mabadiliko hayo Wizara ya Mambo ya Ndani kwa hatua zaidi.
Alisema utekelezaji utaanza kwa kila ngazi kigezo cha elimu kikiwa ni elimu ya dini na kwamba, mabadiliko hayo hayatamhusu Mufti.
Akizungumzia namna Baraza la Ulamaa linavyopatikana, Sheikh Mataka alisema linateuliwa na Mufti. Awali, lilikuwa na wajumbe 11 akiwamo Mufti na sasa wameongezeka na kufikia 16.
Katika baraza hilo, katibu mkuu wa Bakwata ameondolewa kutokana na cheo hicho wakati mwingine huongozwa na mtu ambaye si sheikh.
Sheikh Mataka akizungumzia namna Baraza la Ulamaa litakavyopata majina ya masheikh wa kuwateua alisema: “Tuna mabaraza ya viongozi hadi ngazi ya chini, tutatumia njia mbalimbali kumpata yaani kama ambavyo Rais John Magufuli anavyofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa, wilaya na wengine anatumia vyanzo vyake ndivyo tutafanya.”
Shule za Bakwata
Katika mabadiliko ya muundo na mfumo, Sheikh Mataka alisema baraza hilo linamiliki shule zaidi ya 30, na 10 zimefanyiwa mabadiliko ya utawala ili kubaini ni kwa nini hazifanyi vizuri.
Alisema kwa kawaida, meneja wa shule ni katibu wa Bakwata wa mkoa au wilaya lakini uendeshaji wa shule unahitaji taaluma.
“Meneja anaweza kuwa hana taaluma hiyo, mfano mkuu wa shule awe na shahada ya uzamili huku meneja ni darasa la nne, hapa unaweza kuona tatizo linapoanzia,” alisema.
Alisema kwa utafiti waliofanya kupitia halmashauri na Baraza la Ulamaa, watabadilisha uendeshaji.
Alisema kuanzia Januari shule hizo 10 zitakuwa na menejimenti nyingine ambayo itazisimamia kwa miaka mitatu na baadaye watafanya tathmini.
Uwekezaji makao makuu
Sheikh Mataka alisema miongoni mwa mabadiliko yaliyofanywa ni kuyapa hadhi inayostahili makao makuu ya Bakwata kutokana na ofisi zilizokuwapo awali kuwa na vyumba 10.
“Kwa baraza kubwa kama hili kuwa na vyumba 10 vya ofisi, hata maofisa wengine walikuwa hawatoshi. Kati ya hizo, Mufti alikuwa anatumia hiyohiyo na pale kulikuwa na msikiti mdogo, sasa unajengwa mkubwa wa kuchukua watu takriban 600 kwa wakati mmoja, ukumbi wa mikutano, kwa hiyo tulitaka uwekezaji mkubwa ambao ndiyo unaendelea,” alisema Sheikh Mataka.
Alisema ujenzi utafanyika kwa miezi 20 tangu Oktoba mwaka juzi na unatarajia kukamilika Mei mwakani.
Ushirikiano na taasisi zingine
Sheikh Mataka alisema Waislamu wote wanaunganishwa na Bakwata kuanzia ngazi ya chini mpaka ya juu.
Alisema taasisi za Kiislamu zilizopo likiwamo Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, mdhamini wake wa kusajiliwa ni Bakwata.
“Bakwata ndiyo hutoa barua ya kusajili taasisi,” alisema.
Alisema kinachojitokeza ni baadhi ya taasisi kujiona sawa na Bakwata kwa kigezo cha wote kusajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani jambo ambalo kimuundo na kimfumo haliko hivyo tangu kuanzishwa kwake miaka 50 iliyopita.
“Kinachojitokeza sasa ni kuwa tunasajiliwa wote mambo ya ndani. Kama mama na mtoto; cheti cha mama cha kuzaliwa kinatolewa Rita na mtoto anapata cheti kutoka Rita, kwa hiyo kama mtoto na mama wanapata cheti kutoka Rita haiwafanyi wote kuwa sawa,” alisema.
Kuhusu hija, alisema Bakwata itaendelea kupeleka waumini na kuratibu taasisi zinazopeleka watu hija ili kuondoa matatizo ya baadhi kutelekezwa katika viwanja vya ndege.
No comments:
Post a Comment