Rais wa zamani wa Afrika kusini Jacob Zuma amefika mahakamani kujibu mashtaka ya ulaji wa rushwa yanayohusishwa na mkataba wa ununuzi wa silaha miaka ya tisini.
Hayuko peke yake kwani Rais wa zamani wa Korea Kusini Park Geuin Hye, naye amehukumiwa kifungo cha miaka 24, baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi, iliyomuondoa madarakani.
Hapa, tunawaangazia viongozi wa zamani ambao wameishia kujipata kizimbani.
Jacob Zuma, Afrika Kusini
Rais wa zamani wa Afrika kusini Jacob Zuma amefika mahakamani kujibu mashtaka ya ulaji wa rushwa yanayohusishwa na mkataba wa ununuzi wa silaha miaka ya tisini.
Baada ya Zuma ,75, kufika mbele ya Mahakama Kuu kwa dakika 15 huko Durban, kesi hiyo iliahirishwa hadi tarehe 8 mwezi Juni.
Ameshtakiwa kwa makosa kumi na sita ya ulaji wa rushwa , ufisadi, ulaghai na ulanguzi wa fedha, aliyoyaepuka wakati wa utawala wake na kurejeshwa tena mwaka 2016.
Bw Zuma alitolewa mamlakani kwa nguvu mwezi Februari, akipinga kufanya kosa lolote.
Wafuasi wake walikusanyika katika mji huo kupinga uamuzi huo lakini wakosoaji wake wanadhani mahakama ya korti itachukua muda mrefu.
Baada ya kesi yake kusikilizwa, Bw Zuma alihutubia umati wa watu waliokuwa wameandamana naye kutoka nyumbani mwake.
Rais wa zamani wa Korea Kusini Park Geuin Hye
Aliyekuwa rais wa Korea Kusini, Park Geuin Hye, amehukumiwa kifungo cha miaka 24 jela, baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi, iliyomuondoa madarakani.
Mahakama hiyo pia imempiga faini ya takriban dola milioni 17 baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka kumi na sita zikiwemo, kupokea hongo, matumizi mabaya ya madaraka na kutawala kwa vitisho.
Mahakama iliamua kuwa Bi Park, alitumia wadhifa wake vibaya kushawishi kampuni kuchangia fedha wakfu kadhaa zilizoongozwa na mshirika wake.
Lula da Silva, Brazil
Mahakama ya rufaa nchini Brazil Alhamisi nayo iliagiza kuwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Luiz Inacio Lula da Silva, ni sharti aanze kutumikia kifungo chake cha miaka kumi na miwili gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na ufisadi.
Majaji watano kati ya kumi na mmoja wa mahakama ya rufaa walipinga rufaa hiyo huku watatu kati yao wakimuunga mkono. Kesi hiyo imezua hali ya wasiwasi kisiasa nchini humo.
Mengistu Haile Mariam, Ethiopia
Rais wa zamani wa Ethiopia Mengistu Haile Mariam, alitoroka mwezi Mei mwaka 1991 akiiacha nchi yake katika hali mbaya ya kiuchumi, ukosefu wa chakula na ukosefu wa mgawanyiko wa kisiasa.
Miaka 15 baadaye alihukumiwa kwa vifo na kupotea kwa raia wa Ethiopia wakati wa miaka ya 1970 wakati unaofamika kama Red Teror ambapo Mengistu aliongoza nchi hiyo kwa kupitia kamati ya jeshi linalofahamika kama Dergue.
Alihukumiwa akiwa hayupo mahakamani.
Mengistu amekuwa akiishi uhamishoni Zimbabwe.
Mohammed Morsi, Misri
Rais wa zamani wa Misri Mohammed Morsi amekuwa gerezani tangu mwaka 2013 na Desemba mwaka uliopita aliongezeka kifungo cha miaka mitatu jela kwa kuikosea heshima mahakama.
Bw Morsi alikuwa awali anatumikia vifungo vingine, kikiwemo kifungo cha maisha jela.
Aidha, anasubiri kusikizwa upya kwa kesi nyingine ya njama ya kutekeleza vitendo vya kigaidi kosa ambalo awali alikuwa amehukumiwa kifo lakini baadaye mahakama ya rufaa ikaondoa hukumu hiyo baada yake kukata rufaa.
Bw Morsi aliondolewa madarakani mwaka 2013 na jeshi baada ya maandamano dhidi ya utawala wake na amezuiliwa tangu wakati huo.
Alitozwa pia faini ya dola milioni moja za Misri (£42,000; $56,000) kutokana na hotuba aliyoitoa mwaka 2013.
Kundi la Muslim Brotherhood lake Bw Morsi lilipigwa marufuku nchini humo.
Frederick Chiluba, Zambia
Rais wa zamani wa Zambia, Frederick Chiluba aliiongoza Zambia kwa mwongo mzima katika miaka ya 1990, na baada ya kustaafu alishtakiwa kwa sababu ya rushwa.
Frederick Chiluba aliingia madarakani Zambia mwaka wa 1991, wakati Afrika ilikuwa inaanza kuingia katika demokrasia ya siasa za vyama vingi.
Baada ya kuondoka madarakani mwaka wa 2001, mrithi wake, Levy Mwanawasa, alimshtaki kwa shutuma za rushwa.
Baada ya kesi ya miaka 6 kuhusu ubadhirifu wa mali ya taifa, Frederick Chiluba aliambiwa hakuwa na makosa.
Lakini katika kesi nyingine iliyofanywa katika mahakama kuu ya London, Chiluba alipatwa na hatia ya kuiba mamilioni ya dola ya fedha za serikali ya Zambia, kwa kutumia akaunti kwenye mabenki ya London.
Hosni Mubarak, Misri
Mnamo mwezi Mei mwaka wa 2014, Hosni Mubarak alihukumiwa jela miaka mitatu kwa kupora mamilioni ya dola pesa ambazo zilinuiwa kuikarabati ikulu ya Rais pamoja na wanawe ambayo walitumikia kifungo jela cha miaka minne.
Hosni Mubarak, aliongoza nchini Misri kwa miaka 30, alikuwa kiongozi mwenye nguvu, madaraka, mamlaka kwa nchi yake ya Misri.Bw Mubarak alikuwa akifikishwa mahakamani akiwa kwenye kitanda cha hospitali kwa kuugua.
Hissene Habre, Chad
Rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre amekuwa akitumikia kifungo cha nyumbani tangu mwaka wa 2005, nchini Senegal, ambako alitorokea baada ya kuondolewa madarakani mwaka 1990.
Habre aliongoza nchini Chad kwa miaka minane anadaiwa kuhusika na mauaji na dhuluma dhidi ya maelfu ya wapinzani wake kisiasa na kuwaadhibu watu nchini Chad kati ya miaka ya 1982 na 1990.
Charles Taylor, Liberia
Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor anadaiwa kuhusika na vita hivyo vilivyodumu miaka 10 nchini humo.
Taylor pia alikabiliwa na mashtaka 11 ikiwemo ubakaji na mauaji ya raia wa Sierra Leone na hata kuwafadhili waasi wa RUF.
Inakadiriwa kuwa zaidi wa watu elfu 50 waliuawa na wengine wakiwemo wanawake na watoto walibakwa na kukatwa mikono au miguu na waasi wa RUF ambao walipata usaidizi wa silaha kutoka kwa Bw Taylor.
Taylor alikuwa kiungo muhimu katika biashara haramu ya almasi kutoka Sierra Leone.
Pasteur Bizimungu, Rwanda
Rais wa zamani wa Rwanda, Pasteur Bizimungu alikuwa rais mwaka wa 1994 baada ya mauaji wa kimbari ambapo jamii ya Watutsi 800,000 na Wahutu waliuawa.
Pasteur Bizimungu alifungwa jela kwa miaka 15 kwa madai ya uchochezi, kuhusishwa na uhalifu na utumiaji mbaya wa fedha.
Bw Bizimungu alikamwatwa mwaka 2002 baada ya kujaribu kuanzisha chama kipya cha kisisa.
Laurent Gbagbo, Ivory Coast
Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo amefikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kwa madai ya uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu kwa kuhusishwa na umwagikaji damu uliotokea baada ya uchaguzi wenye utata wa mwaka 2010.
Alikuwa rais wa kwanza kukabiliwa na mashtaka hayo na kufikishwa kwenye mahakama hiyo ya ICC.
Hata mke wake Simone Gbagbo alifikishwa mahakamani kutokana na mashtaka ya kuhusika kwenye ghasia za baada ya uchaguzi ambapo zaidi ya watu 300 waliuawa.
Alisomewa makosa yake chini ya sheria za Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment