Saturday, March 10

WANAOTAKA KUUZA FIGO ILI WAPATE FEDHA SASA WAPIGWA MARUFUKU



*Rais Chama cha Madaktari bingwa wa figo atoa sababu, atoa ushauri kwa Watanzania

Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii

CHAMA cha Madaktari Bingwa wa magonjwa ya figo Tanzania kimepiga marufuku biashara  ya uuzaji figo nchini na kueleza kuwa huo si utaratibu mzuri kwa madhara yake ni makubwa.

Pia kimeelezea hali ya ugonjwa wa figo nchini na kwamba kwa mwaka huu wanatarajia kupandikiza figo kwa wagonjwa 50 huku kikielezea jitihada za Serikali katika kuhamasisha wananchi kuzuia ugonjwa figo.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Rais wa Chama cha Madaktari bingwa ya figo Tanzania Dk.Onesmo Kisanga wakati anazungumza na Michuzi Blogu,ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Figo Duniani ambayo huadhimishwa kila Alhamis ya pili ya kila Machi.Siku hiyo hutumika kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa figo na hatua ambazo wanataalamu wanachukua ili kukabiliana nao.

Akizungumzia kuhusu tabia ya watu kuuza figo ili kupata fedha,Dk.Kisanga ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili amesema kuwa kwa sasa wamepiga marufuku biashara ya watu kuuza figo kwani ina madhara makubwa.

“Nikiri tunapokea maombi mengi pale Muhimbili kutoka kwa watu ambao wanataka kuuza figo ili wapate fedha.Nieleze tu hii biashara ya kuuza figo haitakiwi kabisa nchini Tanzania.Hata Chama cha madaktari bingwa duniani nacho kimepiga marufuku biashara ya figo,"amesema Dk.Kisanga.

Amesema kikubwa ambacho wanakifanya ni kuendelea kutoa elimu kwa wale ambao wanataka kuuza figo kuwa hairuhusiwi na kubwa zaidi ikifanywa ni biashara maana yake wale wasiokuwa na uwezo watashindwa kununua matokeo yake watokosa matibabu.


WATU 50 KUPANDAKIZWA FIGO MWAKA HUU

Wakati huo huo Dk.Kisanga amesema mwaka huu wanatarajia kupandikiza figo kwa wagonjwa 50 na huo ndio mkakati wao na kufafanua kuwa mwezi huu wanatarajia kupandikiza figo kwa wagonjwa watano na mwezi unaokuna watapandikiza kwa wagonjwa saba.Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kutoa kipaumbele kwenye sekta ya afya na hivyo kufanya idadi ya madaktari bingwa katika kutibu magonjwa ya figo kuongezeka.

"Kwa mara ya kwanza Tanzania tulipandikiza figo mwaka 2017 na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.Aliyepandikizwa figo yupo salama na aliyetoa figo naye yupo salama,"amesema Dk.Kisanga.


DALILI KWA MGONJWA WA FIGO

Dk.Kisanga amesema ni ngumu kubaini dalili za mgonjwa wa figo kwa haraka na wakati mwingine hadi unapoanza kuona dalili maana yake figo itakuwa imeharibika kwa asilimia 70 hadi 90.Ndio maana wanashauri Watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara.Hiyo itasaidia madaktari bingwa wa magonjwa ya figo kubaini mapema na kuzuia ugonjwa.
Ametaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo ni mwili kuchoka sana, kuvimba miguu, mikono, sura na tumbo na wakati mwingine kupata shida wakati wa kujisaidia haja ndogo.

AZUNGUMZIA ULAJI VYAKULA

Dk.Kisanga amesema kuna baadhi ya vyakula ambavyo mlaji anatakiwa kuwa makini navyo na kufafanua kuwa vyakula vyenye mafuta mengi vinaweza kusababisha matatizo ya figo.Hivyo chakula lazima kiwe bora na mlaji ale kwa kiasia.Kula kupita kiasi kuna madhara yake yakiwamo ya kuongezeka uzito, kupata shinikizo la damu na sukari na ugonjwa wa figo.

Pia amesema chakula kisiwe na chumvi nyingi kwani nayo huchangia ugonjwa figo na kufafanua wanapopima ili kubaini kama kuna ugonjwa wa figo pia wanapima na mkojo kwani hautakiwi kuwa na protini ambayo nayo ni hatari na si dalili nzuri kwani inaashiria ugonjwa wa figo.Amehimiza watu kufanya mazoezi ili kuweka miili yao katika afya njema.
Pia ameomba watu kutokuwa na tabia ya kupenda kula dawa aina ya Dicropa mara kwa mara kwani moja ya madhara yake ni kusababisha ugonjwa figo.

No comments:

Post a Comment