Saturday, March 10

JAJI MKUU: KIINGEREZA KINAZUIA WANANCHI KUPATA HAKI MAHAKAMANI




JAJI Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma, amesema lugha ya Kiingereza inayotumika mahakamani ni moja ya kikwazo kinachowazuia wananchi kupata haki kwa kuwa wengi wanatumia Kiswahili.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika kikao cha kazi kinachojumuisha watendaji na wataalamu wa mahakama wanaotathmini utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano (2015-2020) pamoja na utekelezaji wa mradi wa maboresho ya utoaji huduma za mahakama na changamoto ambazo WB ilizibaini na kuzitaja kuwa ndizo zilizosababisha ikubali kushirikiana na Serikali katika mradi wa kuifadhili Mahakama ya Tanzania.
“Andiko la WB lilirejea utafiti uliogundua asilimia 60 ya watumiaji wa mahakama, walisema tovuti za mahakama hazitoi taarifa za kutosha kuhusu mashauri yao.
“Tovuti zetu bado hazitumii lugha ya Kiswahili, jana nilitembelea tovuti ya mahakama nikakuta nyaraka tano kuhusu suala muhimu la mirathi.
“Nyaraka hizo zimewekwa katika lugha ya Kiingereza, lugha ambayo inawatenga watumiaji wengi wa mahakama lakini pia imelenga matumizi ya wanasheria zaidi ya wananchi. Tovuti zetu ziongee lugha ya wananchi na ziwe zenye msaada kwa mwananchi wa kawaida,” alisema Profesa Juma.
Pia aliwataka watendaji wa mahakama kuacha kuficha upungufu na makosa waliyonayo kwa sababu WB huangalia wananchi wa kawaida, wafanyabiashara na wanyonge katika jamii.
Aliwataka watendaji hao kuhakikisha wanafanya tathmini ya wazi kuhusu makosa na upungufu waliofanya kwa miaka miwili na nusu ya uhai wa mpango mkakati wa mwaka 2015/2016 na 2019/2020.
“Tusipokubali makosa hatutapata nafasi ya kujirekebisha na tutarudia makosa hayo hayo wakati wabia wetu Benki ya Dunia na Serikali wanatutathmini pia,” alisema Profesa Juma na kuongeza:
“Hapa ni lazima tutambue WB itafanya tathmini yake kama mbia. Hapana shaka, itarejea itatathmini kwa kiasi gani zile changamoto zilizozitaja katika andiko lake la mradi zinatekelezwa.
“Baadhi yake zinagusa upatikanaji taarifa kwa wananchi, zinaweza kuchukuliwa kuwa suala dogo. Lakini kwa mwananchi wa kawaida upatikanaji wa taarifa ni nyenzo muhimu katika kumuwezesha kupata haki yake mahakamani.”
Aliyataja maandiko yaliyo katika mradi kuwa WB iligusia wananchi na wafanyabiashara ambao hukosa taarifa za kimahakama kuwaongoza kufungua mashauri, ada stahiki na kutopata taarifa namna ya kupata rekodi za mashauri.
Pia alisema hawajui sekta mbalimbali za kisheria zinahusikaje katika uendeshaji mashauri na utoaji wa haki kwa sababu andiko lilitarajia kila mahakama kuwa na miongozo kwa watumiaji kuwaongoza wanapotafuta huduma za mahakama.
Alisema WB ilionyesha kutambua upungufu wa stadi na utaalamu umepunguza uwezo wa mahakama kutoka haki kwa weledi na wakati, ambapo andiko lilibaini mfumo wa upimaji na utendaji unahusu watumishi wasio mahakimu au majaji na hakuna upimaji kwa majaji, wasajili na mahakimu.
“Kutokuwapo kwa mfumo wa kupima utendaji wa majaji, mahakimu na wasajili kutaulizwa na WB katika tathmini yake,” alisema Jaji Mkuu Prof. Juma.
Aliyataja maeneo mengine yaliyoonyesha wasiwasi wa WB na kuhitajika kufanyiwa kazi ni pamoja na matumizi madogo ya suluhu nje ya mahakama na upatanishi, gharama za huduma za mawakili hazidhibitiwi kikamilifu.
Pia kuwapo kwa ukubwa wa gharama za madalali kunakofikia hadi asilimia 22 ya thamani ya mali inayobishaniwa mahakamani.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga, alisema zipo changamoto zinazoikabili mahakama ikiwamo upangaji na uendeshaji wa kesi hususani mahakama za chini hatua inayohitaji kutiliwa mkazo.

No comments:

Post a Comment