Hivi karibuni halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ilifunga vibanda 1,000 vya wafanyabiasha baada ya kushindwa kulipa tozo mpya ya Sh50,000. Awali walikuwa wakilipa Sh15,000.
Hayo yalibainishwa jana na mwenyekiti wa wafanyabiasha mkoani hapa, Jumanne Chaurembo, katika viwanja vya Mwanga wakati wa ufunguzi wa maadhamisho ya wiki ya mlipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo amesema mfanyabiashara hana cha kijivunia kuhusu ulipaji wa kodi.
Amesema walitegemea wiki ya mlipa kodi wafanyabiashara wataonyeshwa ni jinsi gani wao na TRA wanashirikishwa na kuwa huru kueleza matatizo yao.
“Wakati kama huu wafanyabiashara wanalalamika biashara kuwa ngumu na wengine wanafunga maduka yao na kukimbia lakini ndo wanaadhimisha wiki ya mlipa kodi ambaye tulitegemea atakuwa anaboreshewa biashara yake ili aweze kupata mafanikio,” amesema Chaurembo
Meneja wa TRA mkoani hapa, Thadeo Kaliza, amesema wiki ya maadhamisho hayo ni fursa pekee ya wafanyabiashara na wakazi wote kujitokeza kwa wingi kwa kupata elimu pamoja na maelekezo mbalimbali kwani suala la kodi lina wigo mpana.
Amesema kwa mkoa wa Kigoma wana walipa kodi wanaofika 9,000 na kwamba kuna zoezi linaendelea kuwahakiki walipa kodi wapya 27,000 kufikia Juni 30 mwaka huu.
Kuhusu mashine za kielektroniki (EFD,s), amesema hawawezi kumlazimisha mfanyabiashara kutumia mashine hizo kama hajafikia kiwango cha Sh14 milioni.
Amesema suala la kuongezewa tozo za vibanda vya manispaa, wao kama TRA hawahusiki kwani zoezi hilo limefanywa na halmashauri husika.
Mmoja wa wafanyabiasha Hassani Jumanne, alisema kutokana na hali ya uchumi kuwa ngumu, wamelazimika kuuza biashara zao kwa bei ya hasara ili kulinda mitaji yao na si kupata faida kama siku za awali.
No comments:
Post a Comment