Wakati wa mvua, huwa ni kawaida kwa radi kutokea na kila mwaka watu huuawa katika maeneo mbalimbali duniani baada ya kupigwa na radi.
Jumamosi, watu 16 waliuawa radi ilipopiga kanisa moja la kidventista kusini mwa Rwanda.
Meya wa eneo hilo alsiema waumini 140 walijeruhiwa wakati wa kisa hicho katika kanisa la SDA.
Meya huyo alisema wanafunzi 18 walijeruhiwa baada ya kupigwa na radi eneo hilo Ijumaa. Mmoja wao alifariki.
Msimu wa mvua za masika unawadia na tayari idara za utabiri wa hali ya hewa zimeanza kutoa tahadhari.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tayari imetabiri kwamba kutatokea mvua kubwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara wiki hii.
"Wakazi wa maeneo yaliyotajwa wanashauriwa kuchukua tahadhari stahiki na kuendelea kufuatilia taarifa pamoja na tahadhari zinazotolewa," TMA imesema kupitia taarifa.
Kando na uharibifu unaotokana na mafuriko, kupigwa na radi kunaweza kusababisha maafisa.
Utawezaje kujikinga?
Radi ni nini?
Radi hutokana na kuachiliwa kwa umeme tuli, tukio ambalo hutokea kutokana na tofauti ya nguvu za umeme kati ya mawingu na ardhi.
Huwa ni cheche kubwa ya umeme kutoka angani, ambayo huwa na nguvu sana. Inaweza kusababisha moyo wa binadamu kuzima na kuacha kupiga na pia kuunguza viungo muhimu mwilini.
Zaidi ya robo tatu ya wanaonusurika baada ya kupigwa na radi hupata ulemavu wa aina fulani ambao hudumu maishani.
Radi hutoka wapi?
Mara nyingi radi hutokea kwenye sehemu ya chini ya anga, ambayo kwa Kiingereza hufahamika kama 'troposphere'.
Huwa inaenea kutoka kwa wingu moja hadi jingine au kutoka kwa wingu hadi ardhini.
Radi inaweza pia kupatikana katika mawingu ya majivu kutoka kwa volkano.
Wanaume hupigwa zaidi ya wanawake
Kwa mujibu wa Taasisi ya Serikali ya Kuzuia Ajali UIngereza (Rospa), wanaume wana uwezekano mara nne zaidi ya wanawake wa kupiwa na radi.
Hili inadhaniwa hutokana zaidi na aina ya shughuli ambazo wanaume hujihusisha nazo, ambapo uwezekano wao wa kuwa nje wakati wa mvua huwa juu mno.
Wachezaji gofu mara nyingi huwa kwenye hatari zaidi kwani ndio walio na uwezekano mkubwa wa kuwa maeneo ya wazi mbali na nyumba au eneo la kujikinga mvua.
Aina tatu za kupigwa na radi
Huwa kuna aina tatu za radi ambazo zinaweza kumpiga mtu.
Moja ni kupigwa moja kwa moja, ambapo radi hukupiga na nguvu za umeme kupitia ndani ya mwili wako hadi ardhini.
Pili ni kupigwa pembeni, ambapo huwa kitu kilichokaribu nawe kimepigwa na radi, nguvu zikaruka na kukufikia.
Tatu ni radi inapopiga ardhini na kisha kukufikia.
Utawezaje kujikinga?
- Tafuta hifadhi pahali ambapo kuna jumbwa kubwa au ndani ya gari. Kukiwa na jumba ambalo lina kifaa cha kukinga dhidi ya radi, utakuwa salama zaidi.
- Usiwe katika maeneo ya wazi, au kwenye mlima ulio wazi.
- Iwapo utakosa pahala pa kujikinga mvua, punguza uwezekano wako wa kupigwa kwa kujikunyata na kujifanya mdogo zaidi. Unaweza kuchutama, kuweka mikono yako kwenye magoti na kufichwa kichwa chako ndani.
- Usijikinge mvua chini ya miti.
- Iwapo upo pahala ambapo kuna maji, ondoka na kukwepa maeneo ya ufukweni yaliyo wazi.
- Utafiti umeonesha kwamba kuwa karibu na maji huongeza hatari ya mtu kupigwa na radi.
- Kwa kuwa radi huwa nguvu za umeme, unafaa kujiepusha na vitu vya chuma vyenye ncha kali ukiwa kwenye mvua.
Kumbuka, hatari ya kupigwa na radi inaweza kuwepo kwa muda hata baada ya mvua kubwa kuacha kunyesha.
No comments:
Post a Comment