Wednesday, March 7

Ujenzi Kinyerezi II wakamilika kwa asilimia 90

Ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II umekamilika kwa asilimia 90 huku ukielezwa kukamilika kwake utaongeza nishati hiyo katika gridi ya Taifa.
Hayo yamesemwa leo Machi 7, 2018 na  meneja wa Kinyerezi II, Stephen Manda wakati akitoa maelezo kwa ujumbe wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) waliotemebelea mradi huo.
"Mradi huu ni wa megawatt 240 ambao utakamilika rasmi Septemba. Ukijumulisha na Kinyerezi I wenye megawatt 150 tutakuwa na megawati 390," amesema Manda.
Amesema mahitaji kwa nchi nzima ni megawatt 1,100 huku uwezo mara baada ya kukamilika kwa Kinyerezi II itakuwa ni megawati 1,400 hivyo kuwa na akiba ya megawatt 300.
"Tanzania ya viwanda inahitaji umeme, umeme upo wa kutosha kwa hiyo wawekezaji wachangamkie fursa ya uwekezaji," amesema Manda
Naye kaimu msajili wa ERB, Patrick Barozi amesema kwa sasa Tanzania inahitaji umeme wa kutosha kwa ajili ya kutekeleza sera ya viwanda na nishati hiyo ipo hivyo ni wawekezaji kujitokeza kwa wingi.
Kuhusu miundombinu ya usafirishaji umeme, Barozi amesema ni wakati wa Tanesco kuboresha miundombinu hiyo ili kuondoa tatizo la nishati hiyo kukatika pindi mvua zinaponyesha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wahandisi, Profesa Ninatubu Lema amesema ni jambo jemba kwamba mradi huo unakwenda kama ulivyopangwa na unasimamiwa kwa sehemu kuwa na wazawa.
"Tumesikia kuwa miradi ya Tanesco kuwa umeme ni mwingi na kubwa nitoe wito kwa  wahandisi tuwekeze katika viwanda kwani umeme upo wa kutosha," amesema Profesa Lema

No comments:

Post a Comment