Inaonekana kama tumewatawala hivi lakini uhalisia ni kwamba tunawategemea wanawake kufahamu asilimia kubwa ya mambo tunayotaka kuyafahamu.
Kwa mfano juzi ilikuwa ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake – tukiwa kwenye makutano yetu wanaume likaibuka swali, kwa nini hakuna siku ya wanaume duniani? Wengine wakasema eti ni kwa sababu matatizo tuliyonayo wanaume hayawezi kutengewa siku moja maalum yakazungumzwa yakaisha, labda kungekuwa na mwaka wa wanaume duniani na bado ingebidi tuchague baadhi ya mambo ya kuyapa kipaumbele.
Mwingine ndio akatuua kabisa, akasema kuna siku ya wanawake pekee duniani kwa sababu matatizo na shida zote zinazoitesa dunia zina siku zake maalum; kwa mfano kuna siku ya Malaria Duniani, siku ya Ukimwi duniani na siku ya Saratani duniani.
Lakini tamati ya kikao hicho tukaja kufahamu kwamba kumbe kuna Siku ya Wanaume duniani kama ilivyo ya wanawake, na yetu ni Novemba 9—tusingeifahamu kama kusingekuwa na siku ya wanawake.
Achilia hiyo, ukitaka kuamini zaidi kwamba wanawake ndiyo wanaotufanya tufahamu mambo lukuki fikiria umelelewa zaidi na nani, utagundua kuwa ni mama – kwa hiyo mengi unayoyafahamu yanaanzia kwake.
Pia wanawake ndiyo wanaotufanya tugundue baa mpya—fikiria ni mara ngapi umeamua kwenda baa ili kukwepa kelele za mkeo ndani ya nyumba, na ili kufurahia zaidi unajikuta unalazimika kwenda baa tofauti tofauti – ugunduzi huu pia ni kwa hisani ya mwanamke.
Na kama ni bachela, mara kadhaa umejikuta ukilazimika kutafuta kiwanja kwenda kutulia na mwanamke; na ili usionekane hujui viwanja? Hapa ni lazima uwe mgunduzi wa kutafuta viwanja vipya kila siku—ugunduzi huu unachochewa na wanawake.
Lakini wanawake pia wametusaidia kuelewa kuwa google ina majibu mengi lakini siyo majibu ya kila kitu. Ulishawahi kuzozana na mwanamke kuhusu chochote na akakosa cha kukujibu? Wana majibu ya kila kitu.
Na wanawake ndiyo wanaofanya tujue thamani halisi ya fedha; unaweza kuwa na visenti vyako. Ukaona una pesa nyingi lakini ukikutana na mwanamke mmoja tu anayejua kutumia ndiyo utagundua kuwa kumbe ulikuwa na vichenji sio pesa.
Na kubwa zaidi ndiyo wanaofanya wagunduzi wanaendelea kugundua bidhaa mpya kila siku kwa sababu asilimia sabini ya bidhaa zinazozalishwa duniani, watumiaji wake wakuu ni wanawake kama vile nguo, vipodozi na simu nzuri. Lakini pia hata kama si kwa vitu wanavyovitumia wao moja kwa moja, bado vinagunduliwa kwa msukumo wao. Kwa mfano magari, hata kama si wanawake wengi wanatumia lakini magari mengi mazuri yanagunduliwa ili kuwavutia wao – wenye magari wanaelewa kinachozungumziwa hapa.
Kwa hiyo kiuhalisia si sisi ambao tunatawala dunia, kwa namna moja au nyingine ni wao, kwa sababu karibu kila kitu kinafanyika kwa ajili yao. Ni vile tu wanawake hawajagundua nguvu walizonazo.
No comments:
Post a Comment