Sunday, March 11

Rais aagiza ajirini wazawa 'walionipigia kura'

Rais John Magufuli (kushoto) na Waziri Charles Mwijage (kulia)
Serikali ya Tanzania imetoa agizo kwa wamiliki wa viwanda nchini kuajiri wazawa.
Rais John Magufuli siku ya Jumapili amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha wamiliki wa viwanda vya ndani wanaajiri wazawa.
“Kama wewe ni waziri nimekuteua mimi, unaacha kuwaajiri wazawa walionipigia kura unaenda kuchukua watu wa nje hili halikubaliki,” amesema Rais.
Rais Magufuli amesema, “Nitoe wito kwa mawaziri wangu na wakurugenzi, hakikisheni viwanda mnavyovianzisha nchini mnaajiri Watanzania, hawa ndio walionipigia kura.”
Rais John Magufuli amesema wananchi wazawa ndio waliompigia kura, hivyo wanastahiki wapewe kipaumbele cha ajira.
Ametoa agizo hilo leo Jumapili Machi 11,2018 akizindua kiwanda cha kufua vyuma cha Kahama Oil Mill mjini Kahama, mkoa wa Shinyanga, limeripoti gazeti la Mwananchi.
Kadhalika amewataka wamiliki wa viwanda kuhakikisha wanatumia malighafi za ndani kutengeneza bidhaa badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
“Mwaka huu pamba nyingi imelimwa, Kahama Oil Mill pia mnatengeneza mafuta, hakuna haja ya kuagiza pamba kutoka nje wakati tuna pamba ya kutosha hapa,” amesema.
Kuhusu kiwanda cha chuma amesema malighafi inapatikana nchini, hivyo iwapo mkurugenzi wa Kahama Oil Mill anahitaji yuko tayari kumpa bure badala ya kuagiza nje.
Kadhalika amewataka Watanzania kununua bidhaa zinazozalishwa nchini, huku akisisitiza wamiliki wa viwanda kutengeneza vitu vilivyo na ubora ili kukabiliana na ushindani.

No comments:

Post a Comment