Saturday, March 3

Taasisi tatu nchini zatupiana mpira mabasi 70 Dart kuingia barabarani


 Taasisi tatu zote zikiwa na masilahi katika usafiri na usafirishaji zimegongana huku Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (Sumatra) wakidai hawajapata maombi ya kibali cha kuruhusu magari mapya 70 kuingia barabarani.
Dart na Sumatra zimelaumiwa kupitia taarifa iliyotolewa juzi baada ya Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), kusema kuchelewa kuingia barabarani kwa mabasi hayo waliyoyaleta hivi karibuni kunatokana na uchelewaji wa kibali kutoka Sumatra na Dart.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Udart, Deus Bugaywa alisema mabasi hayo yataingia barabarani mara tu baada ya kupata vibali kwa mamlaka zinazohusika.
Alizitaja mamlaka hizo kuwa ni Dart ambao anadai ndio hasa wasimamizi wa mradi na Sumatra wenye mamlaka ya kutoa leseni za mabasi kuingia barabarani.
“Ni imani yetu kwamba vibali hivyo vikitoka, basi tutawaondolea kero abiria wetu na tunawaomba kuwa na subira kwani ili mradi mabasi hayo tayari yapo hapa nchini hakuna litakaloshindikana, ni muda tu,” alisema.
Hata hivyo, gazeti hili liliwatafuta kwa nyakati tofauti na kwa njia ya simu wakurugenzi wa mamlaka hizo ili kujua sababu ya kuchelewa kutoa vibali hivyo, ikizingatiwa mabasi hayo yana wiki mbili hadi sasa tangu yaingizwe nchini ambapo yule wa Dart, Ronald Lwakatare alisema anachojua ni kuwa hajapata maombi ya kuombwa kibali kwa ajili ya mabasi hayo na kuahidi kwamba endapo yatamfikia ataharakisha kukitoa. “Hapa wewe ndio unaniambia kuwa mabasi hayo hayajaingia barabarani kwa sababu ya kibali, lakini kwa kumbukumbu yangu mpaka sasa sijaona maombi yoyote mezani kwangu yanayohusu mabasi hayo kutaka kuruhusiwa kuingia barabarani, labda kama yamekuja muda huu ambao nipo nje ya ofisi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema hajapata maombi yoyote na kwamba, kwa kawaida wanayapata kupitia Dart ambao ndio wasimamizi wakuu wa mradi.

No comments:

Post a Comment