Saturday, March 3

Asilimia 90 ya wanyamapori watoweka kwa ujangili


Ujangili unaofanyika katika jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori Wami Mbiki iliyopo mkoa wa Pwani na Morogoro, haujawahi kufanyika hifadhi zingine zozote nchini, imeelezwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori, Omary Tofiki alisema miaka iliyopita hifadhi hiyo ilikuwa na wanyama wa aina zote kasoro faru, lakini kutokana na kukithiri kwa ujangili wanyama waliobaki asilimia kumi.
Tofiki alisema licha ya doria zinazofanywa mara kwa mara, wapo baadhi ya askari wamekuwa wakitoa taarifa kwa majangili hivyo kukwamisha mapambano. “Ujangili unaofanywa katika hifadhi hii haufanywi mahali popote nchini, mara kadhaa nimeshatoa taarifa za ujangili huu kwa viongozi mbalimbali lakini hali ni mbaya,” alisema Tofiki.
Naye ofisa wanyamapori mwandamizi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (Tawa), Abraham Jullu alisema hifadhi hiyo ni muhimu kwa ustawi wa wanyama kwani imekuwa ikitumika kama sehemu ya mazalia ya wanyama wanaotoka hifadhi za jirani ambazo ni Saadani, Mikumi na Selou.
Alisema kuwa kama hifadhi hiyo haitasimamiwa na kupewa ulinzi madhubuti idadi ya wanyama katika hifadhi hizo itapungua kwa kuwa wanyama wengi watauawa wakiwa Wami mbiki.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaji Majid Mwanga alisema kuwa sehemu ya hifadhi hiyo ya Wami mbiki iko kwenye wilaya yake na kwa kiasi kikubwa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo imefanyakazi ya kuendesha doria na misako katika hifadhi hiyo.
Alisema kuwa katika misako hiyo pia walifanikiwa kuwaondoa wafugaji waliovamia katika hifadhi hiyo hata hivyo kwa sasa wafugaji wameanza kurudi na kuweka makazi tena wakiwa na makundi makubwa ya mifugo.

No comments:

Post a Comment