Monday, March 12

Siri ya wanawake kufanikiwa katika viwanda Afrika: Wanawake watatu wasimulia

Wanawake watatu
Haki na usawa kwa ndio mambo makuu yanayoshinikizwa duniani wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake wiki hii.
Kwa kawaida siku hii huwa ni fursa ya kuchukua hatua, kufanya mabadiliko, kushinikiza, kuhimiza na kuwawezesha wanawake wa nyanja zote kujitambua uwezo wao.
Licha ya kwamba wanawake wanachangia ukuaji wa uchumi kote Afrika, ukandamizaji unatatiza nafasi wanazoweza kuwa nazo.
Kutokana na kuendelea kukithiri kwa umaskini, wanawake wengi wanajipata katika ajira zenye vipato vya chini na wanakuwa na nafasi finyu ya kujiendeleza.
Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa, ili kuyatimiza, malengo ya maendeleo endelevu kama sehemu ya ajenda ya mwaka 2030, kuna haja ya kulisaidia bara la Afrika katika kushinikiza ustawi endelevu wa kiviwanda na unaojumuisha kila mtu.
Na hiyo ni kumaanisha hakuna atakaye achwa nyuma, hususan wanawake.
Baadhi ya mataifa ya Afrika yanapania kuwa na nchi zilizoendelea kiviwanda, lakini kwa mara nyingi idadi kubwa ya wanawake wanaonekana kususia kujitosa katika sekta hiyo. Je ni kwanini?
Tumezungumza na wanawake watatu kutoka Afrika Mashariki ambao ni miongoni wanawake wengi waliolivuka daraja hili na kupata ufanisi. Siri yao ni gani?
Bertilda Niyibaho
Image captionBertilda Niyibaho, mmiliki wa kiwanda kinachozalisha unga unaotokana na uyoga

Bertilda Niyibaho - Mjasirimali nchini Rwanda:

Bi Niyibaho Bertilda ni mjasiriamali aliye na kiwanda kinachozalisha unga unaotokana na uyoga kufwatia mradi kabambe alioanzisha wa kuimarisha lishe bora miongoni mwa jamii.
Biashara yake imepanuka na kuvuka mipaka ya Rwanda.
Huku akionyesha kiwanda chake, ambayo sehemu kubwa ni maabara na sehemu nyingine inatumiwa katika kurutubisha zao la uyoga, anasema akianza alikuwa mkulima tu wa kawaida: "Nilianza shughuli zangu nikitengeneza pombe ya kienyeji itokanayo na ndizi, lakini nikaja kuona kwamba mabaki ya ndizi na mabaki ya mazao mengine yanatupwa tu kiholela ilhali yangeweza kuzalishwa mambo mengine yakawa na manufaa kwa jamii, basi nikajitosa katika kulima uyoga."
Sehemu ya kiwanda cha bi Niyibaho inatumiwa katika kurutubisha zao la uyoga
Image captionSehemu ya kiwanda cha bi Niyibaho inatumiwa katika kurutubisha zao la uyoga
Kiwanda chake kilikua na akaanza kutengeneza unga wa uyoga na mazao mengine. Biashara yake imekuwa kadri muda ulivyosogea na imepanuka na kuvuka mipaka.
Kwa sasa yeye husafirisha bidhaa zake hadi Tanzania, Kenya, Uganda na hata Burundi. Licha ya ufanisi huu anasema hakukosa changamoto:
"Shida niliyo nayo ni kwamba, bidhaa zangu zikifika huko mfano Uganda zinabandikwa leseni ya kwamba zilitengenezwa Uganda!
"Binafsi nilifuatilia nikatembelea wale wanaolangua bidhaa zangu nikashangaa nilipokuta kwamba wameandika eti 'Made in Uganda!'
Changamoto nyingine anasema ni kukosa uungwaji mkono wa serikali na kupata leseni ya ubora wa bidhaa kumwezesha kupenya katika masoko ya Ulaya na Marekani.
Jennifer Bash Tanzania
Mkurugenzi wa kampuni ya Alaska
JenniferHaki miliki ya pichaHISANI
Jennifer Bash ni mkurugenzi wa kampuni ya Alaska nchini Tanzania.
Kampuni yake imejikita katika kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo yanayo zalishwa na wakulima wa Tanzania, wengi wao wakiwa ni wanawake.
Kampuni hii pia inajishughulisha na uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za vyakula kama mayai, mchele, mafuta ya Alizeti, unga wa sembe na dona.
Je ni ipi siri ya ufanisi wake katika sekta ya viwanda? Jenifer anaamini kwamba mtaji sio kikwazo kwa kuwa wazo ndio mtaji.
'Mara nyingi watu wanakua na mawazo makubwa lakini washindwa kuyafanyia kazi wakidhani wanahitaji mtaji mkubwa kufanyia kazi wazo lao.

'Ubunifu ni muhimu'

Wakati kuwaza makubwa ni vyema, lakini tukubali kuanza na kidogo ili kufikia makubwa kulingana na mazingira yanayotuzunguka'.
Jennifer anasema ubunifu wa uendeshaji wa biashara ni jambo muhimu kwenye kufanikisha biashara yeyote ili kupata wateja.
Alaska Tanzania imebuni soko lake kwa kujikita kwenye programu iitwayo 'Mama Alaska" ambayo inamuwezesha mama ntilie (Mama Lishe) kupata bidhaa za Alaska kwa urahisi na bei nafuu.
Pia inawawezesha wakulima kupata elimu ya kukuza biashara yao na kuona thamani ya kile wanachokifanya kwa kuboresha huduma zao na kutengeneza mnyororo mpya wa thamani.

Lorna Rutto - Kenya

Mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Ecopost

LornaHaki miliki ya pichaHISANI
Lorna Rutto ni mwanzilishi na afisa mkuu mtendaji wa EcoPost, kampuni ambayo imekuwa ikitumia taka za plastiki kuunda bidhaa mbalimbali zikiwemo boriti za kutumiwa kwenye nyua na mabango.
Kampuni yake huunda pia bidhaa mbalimbali za kutumiwa katika ujenzi.
Lorna amepokea tuzo nyingi Kenya na kimataifa na alikuwa miongoni mwa wanawake vijana 20 wenye nguvu Afrika walioorodheshwa na jarida la Forbes.
Alipokuwa anaanzisha Ecopost, alikumbana na changamoto nyingi hasa katika kutafuta mtaji.
"Tulitazamwa kama biashara iliyo na hatari nyingi tukilinganishwa na biashara nyingine sokoni. Benki zilitaka taarifa za akaunti za benki kuthibitisha kwamba biashara yetu ilikuwa inafanya vyema ilhali tulikuwa tu ndio tunaanza," anasema.
"Tulitakiwa pia tunatakiwa kutoa dhamana ya mkopo lakini hatukuwa na chochote."
Waliwasilisha maombi katika mpango wa Enablis- uliofadhiliwa na Wakfu wa Safaricom na wakashinda na hapo wakafanikiwa kupata mtaji.
Kando na fedha, walikabiliwa pia na tatizo la mitambo ya kutumia ambayo walihitajika kuiagiza kutoka nje ya nchi, pamoja na wafanyakazi wenye ufundi uliohitajika kuendesha mitambo hiyo.
Gharama ya uzalishaji ilikuwa pia juu - gharama ya umeme, malighafi, kulipia leseni na kadhalika.
"Hatukupokea pia usaidizi kutoka kwa serikali na wanaounda sera. Wajasiriamali hasa walio katika sekta ya viwanda wanahitaji kichocheo na usaidizi pamoja na mazingira mahsusi ili kufanikiwa," anasema Bi Rutto.
Anasema amegundua kwamba "fursa zipo kila pahali".
"Niliigundua fursa yangu katika kutumia tena taka. Taka si taka hadi zitupwe. Kazi yote pia ni ya heshima. Nimejifunza pia kwamba ni muhimu kuwa mbunifu, kuvumbua na kuendelea kujiboresha kila wakati," anasema.
"Safari yangu haijakuwa rahisi lakini nimejifunza kutokata tamaa kamwe. Nimegundua pia kwamba kuomba usaidizi inapobidi ni muhimu," anasema Bi Rutto.

'Ni muhimu kuomba usaidizi'

"Wanawake wengi hufikiria kwamba kuomba usaidizi ni dalili ya udhaifu; ukweli ni kwamba ni ishara ya nguvu. Kupata washirika wafaao ni muhimu pia. Ukitaka kwenda haraka, nenda peke yako, ukitaka kwenda mbali, shirikiana na wengine."
Ushauri wake kwa wanawake ambao wangependa kufanikiwa katika viwanda ni kwamba lazima utafute soko la bidhaa zako kwanza.
"Ningewahimiza wanawake wawe wabunifu na kuvumbua mambo na pia kuingia katika sekta ambazo zimetawaliwa na wanaume kwa muda mrefu mfano viwanda wakiona kuna fursa.
"Usiige tu wengine au kuchagua biashara iliyo rahisi. Soko limejaa wahusika wengi na kuna changamoto katika kutafuta nafasi ya ukuaji."
Baadhi ya watu huogopa kutofanikiwa lakini Bi Rutto anasema ni muhimu kujiamini mwenyewe.
"Kuwa na ujasiri na anza bila kukawia. Usizuiwe na chochote, usizuiwe hata na mtaji. Ningewashauri wanawake kuacha na fedha walizo nazo na kuzitumia vyema."
Anasema katika kuanzisha biashara au kiwanda, ni vyema kufikiria mchango wa biashara hiyo kwa jamii.
"Moja ya yaliyosaidia ukuaji wa Ecopost ni nia yetu ya kutaka kuleta mabadiliko katika jamii, tukihifadhi mazingira pia."

No comments:

Post a Comment