Saturday, March 3

Shule yafungwa baada ya wanafunzi kuvamia, kuharibu nyumba ya mwalimu


Katika hali isiyo ya kawaida, Shule ya Sekondari ya Lyamungo wilayani Hai imefungwa kwa wiki mbili baada ya kutokea vurugu zilizofanywa na wanafunzi na kusababisha uharibifu wa nyumba ya mwalimu wa nidhamu, Safari Rasin.
Taarifa ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo aliyoitoa jana inaeleza kuwa shule hiyo imefungwa baada ya wanafunzi zaidi ya 400 kuvamia nyumba ya mwalimu huyo na kufanya uharibifu kwa madai kuwa amekuwa akiwatukana matusi ya nguoni jambo ambalo limekuwa likiwakera.
Sintoo alisema Februari 27, wanafunzi hao walikuwa na uchaguzi wa serikali yao na mmoja wao aliandika matusi kwenye karatasi ya kura, hali iliyowafanya walimu kuwataka kila mmoja achukue karatasi yake ili kumbaini mhusika.
Alisema karatasi zilichukuliwa na ikabaki moja iliyoandikwa matusi, huku mwanafunzi mmoja akikosa karatasi yake aliyopigia kura, na katika kufuatilia walibaini iliyobaki ni ya kwake hivyo taratibu za nidhamu zilichukuliwa ikiwamo kumsimamisha shule.
Sintoo alisema mwanafunzi aliyeandika matusi aliadhibiwa kwa kusimamishwa masomo kwa muda, hali iliyoibua taharuki kwa wenzake na kwenda kuvamia nyumba ya mwalimu huyo kwa madai kuwa ndiye amekuwa akiwatolea matusi.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamisi Issah alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:00 asubuhi.
Issah alisema miongoni mwa mali zilizoharibiwa ni milango, madirisha, mabati na migomba yote inayozunguka nyumba hiyo ambayo ipo eneo la shule.

No comments:

Post a Comment