Saturday, March 3

Lukuvi, naibu wake wapishana msituni


Unaweza kusema ni mwendo wa mbio za nyika namna mambo yanavyokwenda katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wakati Waziri William Lukuvi akiwa ameanzia mkoani Kagera na Shinyanga ambako ameacha vumbi likitimka dhidi ya maofisa ardhi na matajiri waliokuwa wakionea maskini kwa kuwanyang’anya maeneo yao, naibu wake Angelina Mabula alianzia Mwanza baadaye Mara na sasa yupo Kilimanjaro.
Akiwa Kilimanjaro, juzi Mabula alikabidhiwa na CCM migogoro miwili ya ardhi mjini Moshi ikitaka asaidie kuipatia ufumbuzi.
Migogoro hiyo ni wa Pasua Block JJJ ambako zaidi ya watu 100 waligawiwa viwanja na Manispaa ya Moshi, lakini kampuni ya Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), inadai ni mali yake.
Septemba 14 mwaka jana, Rahco iliweka alama X katika nyumba hizo ikiwataka wazibomoe ndani ya siku 30, lakini halmashauri inadai Rahco hawajawahi kumiliki eneo hilo wala hawakuwahi kupewa na kwamba, halmashauri wakati ikiandaa mpango kabambe wa mji (master plan) mwaka 1962, ilitenga tu eneo la kujenga viwanda na ikatenga kipande cha ardhi cha kujenga reli kuhudumia viwanda hivyo.
Hata hivyo, viwanda hivyo havikujengwa na eneo lote kujengwa makazi hivyo halmashauri ikaomba kubadili matumizi ya kipande cha ardhi kilichokuwa kijengwe reli, maombi yaliyoridhiwa na wizara.
Akiwasilisha nyaraka za mgogoro huo ikiwamo hati miliki, katibu wa CCM Mkoa Kilimanjaro, Jonathan Mabhia alisema mgogoro huo ni kero inayohitaji majibu.
“Wananchi wangependa wapatiwe majibu ya uhakika wa kuendelea kuishi na unavyojua migogoro ya ardhi ni kero kubwa,” alisema Mabhia na kuongeza: “Maana tunaonekana kama hatushughuliki na matatizo ya wananchi. Ni matumaini yangu utatusaidia kushughulikia tatizo hilo ambalo kwa kweli ni kero kubwa kwa wananchi.”
Katibu huyo alisema kwa kutambua CCM ndio kimbilio la Watanzania, wapo wananchi waliompelekea barua yeye na wengine walituma barua hizo kwa katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Mgogoro mwingine aliouwasilisha ni wa Meresini katika mji mdogo wa Himo, ambako wananchi wananyimwa viwanja vikiwamo vya kujenga shule na kupewa watu wengine akiwamo mwekezaji.
Akijibu maombi hayo, Mabula alisema kwa kuwa mgogoro wa Pasua Block JJJ umewasilishwa ukiwa na nyaraka, atazipitia na kumkabidhi Kamishna wa Ardhi.
Kuhusu mgogoro wa Mieresini, alisema nalo amelichua ili alifuatilie aone namna ugawaji huo ulivyofanyika na kilio cha wananchi.

No comments:

Post a Comment