Amesema Polisi Iringa watakapomaliza uchunguzi wao na yeye ataanzisha uchunguzi wake.
Nondo ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anadaiwa kutoweka Machi 6 lakini alijisalimisha mikononi mwa polisi wilayani Mafinga, Iringa Machi 7.
Kwa sasa amefunguliwa jalada la uchunguzi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire aliwaeleza wanahabari kuwa uchunguzi huo unalenga kubaini iwapo kweli alitekwa au alitoa taarifa za uongo kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kuvuruga amani.
Makonda akizungumza katika hafla ya kuwatunuku vyeti vya sifa maaskari 40 wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa utendaji uliotukuka mwaka 2017, alisema kijana huyo alitaka kuchafua sifa ya Mkoa wa Dar es Salaama na akaongeza kuwa hata taarifa zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari hazikuthibitishwa na mamlaka husika.
“Juzi nilisikia kuna mtu mmoja eti ametekwa, Nafikiri Iringa, wakimalizana naye wamlete Dar es Salaam asitake kutuchafulia sifa ya mkoa wetu. Halafu waandishi wa habari wanaandika tu bila kuwa na uhakika,” alisema Makonda.
Alisema taarifa za mtu huyo kutoweka ziliibuka wakati chuo kimefungwa na wanafunzi wanarudi nyumbani.
“Shule zilikuwa ndio zimefungwa, na wanafunzi wanarudi nyumbani, kwa hiyo hata mtandao ukikosekana tu kidogo mtu amepotea au ametekwa? Halafu mnaitisha waandishi wa habari kutoa tamko?” alihoji Makonda.
Aliwataka wanahabari kuangalia habari wanazopeleka kwa umma na kama hazijathibitishwa na mamlaka husika, alishauri ziwekwe pembeni kwa sababu taarifa nyingine huibua taharuki isiyokuwa na misingi.
Awapongeza askari
Katika hafla hiyo, Makonda aliwapongeza askari hao na kuwataka kuongeza juhudi zaidi katika kutekeleza majukumu. Aliwataka ambao hawamo kwenye orodha hiyo kutokata tamaa na badala yake wawe na ari ya kufanya kazi kwa bidii.
“Zawadi mlizopata ni kubwa lakini hazilingani na ukubwa wa kazi mliyoifanya. Mwaka ujao itakuwa kubwa zaidi ya hapa. Tukio kama hili litaandaliwa na kamati nzima ya ulinzi na usalama ili kuwapa hamasa tukizingatia kuwa mazingira yenu ya kufanya kazi muda mwingi yanakatisha tamaa,” alisema Makonda.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema askari wote wanaofanya kazi chini yake wako vizuri na utendaji wao unaridhisha na waliotambuliwa ni sampuli tu. “Tukio hili lipo kwa mujibu wa sheria, wapiganaji wengine hawatakiwi kuona wivu, bali kuongeza ari ili mwakani nao wawe miongoni mwa wazawadiwa,” alisema.
Askari 40 walitunukiwa zawadi mbalimbali. Askari 12 walipewa pikipiki kila mmoja, 16 walipewa jokofu na 12 walipewa mabati 60 kila mmoja.
Kwa polisi waliopewa mabati, Makonda aliahidi kuwapa na mifuko 100 ya saruji kila mmoja.
No comments:
Post a Comment