Mzee aliona mbali sana. Alijua wazee wa bandari wangejifanya kuwa wao walikuwa wakinywa “chimpumu” na Mkwawa halafu wangemhoji jinsi alivyolipata jiwe hilo. Hatimaye wangemnyang’anya na kulitia sokoni kwa maelezo yaleyale yaliyoandikwa na babu. Hivyo dogo akaekti ububu.
Watu walimsimamisha na baada ya kusoma sifa za jiwe wakamuuliza bei. Dogo akanyoosha vidole vitatu hewani. Wakasema “aha! Buku tatu. Bei ya mwisho je? Je bei ya kuuzia?” Dogo akarudia vidole vilevile vitatu.
Walipotaka kununua dogo aliondoka na jiwe lake na kurudi kwa babu. Babu akamwambia, “Sasa hivi nenda mitaa ya uzunguni. Ukiulizwa bei ufanye kama nilivyokuagiza.” Dogo akaingia Oysterbay na Masaki. Aliponyoosha vidole vitatu wakasema “Elfu thelathini? Niuzie…”
Akarudi tena kwa babu. akaambiwa “Sasa tembea kwenye balozi za mamtoni ukafanye vilevile. Lakini sasa usirudi nalo, liuze huko.” Dogo akaingia ubalozini.
Kama kawaida alipoulizwa bei akanyoosha vidole vitatu. Balozi akasema “Laki tatu? Tafadhali niuzie…” Akachukua hela na kurudi kwa babu. Maisha yakaendelea. Yule balozi alilipeleka jiwe Ulaya na kuliweka kwenye soko la vitu vya kale vilivyovumbuliwa barani Afrika.
Siku moja dalali wa Kiswahili alipita kwenye soko hilo, akalinunua jiwe hilo kwa dola zenye thamani ya shilingi milioni tatu za Kitanzania. Alijua kwa sifa za jiwe hilo asingekosa shilingi milioni thelathini kutoka serikalini ili jiwe likahifadhiwe kwenye Makumbusho ya Taifa.
Tunajifunza kuwa thamani ya kitu hupandishwa na watu kulingana na mazingira ya soko. Kuna koti ulitaka kuuziwa pale Tandika lakini ukalikwepa kwa madai ya viwango. Likapelekwa dry cleaner na ukaletewa ofisini kwako kule Kivukoni ukalinunua kwa bei mara kumi ya ile uliyotajiwa Tandika.
Au hujui kwamba zile kauzu za pakti unazozinunua shilingi elfu mbili Posta na Feri ndio zilezile zinazouzwa kwenye genge la jirani tena kwa shilingi mia tano tu? Au ni kwa sababu kwenye pakti kuna tangazo linalosema dagaa wanaongeza kinga ya mwili na nguvu za kiume? Yaleyale ya “jiwe aliloogea Mkwawa”.
Kwa hili nawapongeza wajasiriamali. Wanajua kuwa uongo wa sangoma ndiyo tiba ya mgonjwa. Lakini kwa leo inanibidi nirudi kuwa mzalendo mwenye kutazama maslahi mapana ya Taifa langu kwanza.
Mtu yeyote mwenye busara hakosi bustani ya mboga nyumbani kwake. Akikosa basi ni kwa sababu iliyo nje ya uwezo wake; pengine kiwanja alichoweza kununua kilimtosha kuinua mjengo tu bila kuacha mahali pa kucheza watoto.
Bustani ingembeba akapata angalau mboga orijino maana hizi za mtaani hazieleweki kabisa. Vilevile atapata utelezi kidogo wakati vyu… wakati hali imekuwa ngumu. Unaweza kuamka na maganda ya karanga mfukoni bila senti ukasonga unga uliobaki jana kwa tembele la bustanini kuliko kumsomesha mgogo buchani. akukopeshe nyama. Mwaka 1985 Mwalimu Nyerere alizindua kiwanda cha kutengeneza karatasi huko Mufindi Mkoani Iringa. Bila shaka alizingatia mahitaji ya karatasi yalivyokuwa yakipanda. Kwanza wasomi walikuwa wakiongezeka kila muhula. Wasomi wote (kuanzia vyuoni hadi chekechea) hawakuweza kufanya lolote pasipokuwa na karatasi. Hata huku mtaani wakati vita ya taka sugu kama plastiki ikipamba moto, karatasi ilikuwa mkombozi kwenye mifuko, na mapambo.
Pia kuna mtu alinieleza kuwa bi mkubwa wake alikuwa akitumia mkaa wa karatasi tangu akiwa mwanamwali. Aliloweka karatasi na maboksi kwa siku kadhaa, akayachanachana ndani ya maji na kuyakamua katika mfano wa matonge ya ugali. Kisha akayaanika juani. Kitu tayari. Huyu atunukiwe shahada ya mazingira.
Kile kiwanda kilifanya kazi nzuri kiasi kwamba Tanzania iliuza karatasi hadi nje. Lakini pia tulipata vifungashio vya bidhaa za viwandani (kwa maana ya maboksi na mifuko).
Lakini mwaka 2004 kiwanda kikauzwa kimya kimya kwa Wakenya kwa madai ya kutozalisha vizuri. Sijui ni nani anayeukata mkono wa mtoto wake kwa sababu ati kaunyea! Lakini kwa sababu yaliyopita si ndwele, tutazame yanayotokea sasa. Ukiyakosa maji ndipo utajua umuhimu wake.
Hivi sasa tunategemea karatasi za Afrika Kusini, lakini hasa za China. Kutokana na desturi ya Wachina, kuanzia tarehe 23 mwezi wa 12 hadi tarehe 15 mwezi wa Januari Wao huwa likizoni kuadhimisha sikukuu ya mwaka mpya wa kijadi.
Hali hii inatuathiri sana kwa sababu hakuna mizigo inayoingia wakati sisi hutumia makontena mengi sana ya karatasi katika muda mfupi. Kwa uhaba huo bei hupanda hadi mara tatu ya bei elekezi. Wengi wanashindwa kununua na elimu ya watoto wao inayumba kwa sababu wakizikosa wanafukuzwa shuleni.
Huwa najiuliza Wakenya waliona nini ambacho sisi wenye kiwanda tulishindwa kukiona. Bila shaka wao wana upeo wa babu aliyeuza jiwe. Tangu enzi zile walitukimbiza sana na bidhaa zao kama mafuta ya Blue Band dhidi ya Tan Bond yetu kwa jinsi walivyojua kuongeza thamani.
Japokuwa hatushadadii yaliyopita lakini “Tanzania ya Viwanda” isipofanya “ndwele” sijui kama tutafika.
No comments:
Post a Comment